Transparency International: Ufisadi waanza kupungua Tanzania

Nuzulack Dausen
January 26, 2017

Vita dhidi ya ufisadi inayoongozwa na Rais John Magufuli imesaidia Tanzania kupaa kwa alama mbili katika viwango vya mapambano ya rushwa ulimwenguni ikiwa ni mwaka mmoja tangu aingie madarakani.

Ripoti mpya ya hali rushwa duniani ya Shirika la Kimataifa la Transparency International iliyotolewa jana inaonyesha kuwa Tanzania ilipata alama 32 mwaka 2016 kutoka 30 mwaka juzi.

Kiwango hicho ni kikubwa kufikiwa ndani ya miaka miwili iliyopita. Katika viwango hivyo, shirika hilo linapima kuanzia alama sifuri ikimaanisha nchi imekithiri kwa rushwa wakati alama 100 ikimaanisha taifa husika halina rushwa.

Kupanda kwa alama hizo, kumefanya Tanzania ipande nafasi moja hadi ya 116 kati ya nchi 176 zilizofanyiwa utafiti kutoka 117 mwaka juzi ikiwa nyuma ya Rwanda katika ukanda wa Afrika Mashariki ambayo ni ya 50 ulimwenguni. Mwaka juzi nchi 167 zilifanyiwa utafiti.

Pamoja na mafanikio hayo, Transparency International bado imeiweka Tanzania katika kundi la “nchi kubwa za Afrika ambazo hazikupiga hatua yoyote katika mapambano dhidi ya rushwa” sanjari na Kenya, Afrika Kusini na Nigeria.

Tanzania bado ipo chini ya wastani wa kiwango cha rushwa ulimwenguni ambacho ni alama 43 kinachoonyesha ufisadi umeenea katika utumishi wa umma katika nchi husika.

Mshauri wa sera wa asasi ya kiraia ya KEPA, Bakar Khamis Bakar alisema kupaa kwa alama hizo ni hatua njema kutokana na jitihada zilizopo za kupambana na ufisadi katika Serikali ya awamu ya tano.

Hata hivyo, alisema bado rushwa kubwa hazijachukuliwa hatua ipasavyo na kwamba iwapo Serikali ikiweka nguvu zaidi huko Tanzania itapaa maradufu katika viwango hivyo.

“Tumefanya vizuri lakini bado tupo chini ya wastani kwa sababu rushwa kubwa, ambazo hutumika kupima jitihada za Serikali kupambana na rushwa, hazijadhibitiwa kikamilifu,” alisema.

“Na vita dhidi ya rushwa siyo suala la mtu mmoja ni la kimfumo hivyo kuna haja ya taasisi mbalimbali zinazoshughulika na ufisadi kushirikiana kikamilifu zikihusisha wananchi, asasi za kiraia na vyombo vya habari.”

Kwa Afrika, Botswana imeendelea kuwa nchi yenye kiwango kidogo cha rushwa wakati Sudani ya Kusini na Somalia zikitajwa kukithiri ufisadi.

Mratibu Mwandamizi wa Transparency International kwa ukanda wa Afrika, Paul Banoba alisema viongozi wa Afrika wanaoingia madarakani kwa kutumia “sera ya kupambana na ufisadi” wanapaswa kutekeleza ahadi zao kwa kutoa huduma kwa wananchi bila mlungula.

“Wanatakiwa kutekeleza ahadi zao kuzingatia misingi ya utawala bora, demokrasia na haki za binadamu.

“Hii ni pamoja na kuimarisha taasisi zitakazofanya wawajibike zaidi na kuwa na mifumo rafiki na huru ya uchaguzi itakayoruhusu wananchi kuwachagua au kutafuta viongozi wengine,” alisema Banoba katika uchambuzi wa ripoti hiyo uliohusu Afrika.

Katika ripoti hiyo, Denmark imeendelea na kuwa kinara kwa kuwa na kiwango kidogo cha rushwa duniani baada ya kupata alama 90 ikiwa ni alama moja chini ya utafiti wa mwaka juzi.

Somalia ndiyo nchi iliyokithiri kwa rushwa ulimwenguni baada ya kushika mkia katika nafasi ya 176 katika viwango hivyo ambavyo hutumika kupima utendaji wa serikali mbalimbali dhidi ya kuendeleza utawala bora.

Transparency International imesema kuwa theruthi mbili ya nchi 176 zilizofanyiwa utafiti hazikuvuka alama 50. Wastani wa kiwango cha rushwa ulimwenguni ni 43 ambayo bado ni kiwango kikubwa cha rushwa.

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania