Hii ndiyo tofauti ya walimu wa mijini na vijijini

Nuzulack Dausen
February 1, 2017

Saumu Mwalimu na Nuzulack Dausen

Muhula wa kwanza wa masomo mwaka 2017 umeanza, walimu wa vijijini wanaingia katika kipindi kingine cha kukabiliana na changamoto za kikazi tofauti na wenzao waliopo maeneo ya mijini.

Pamoja na kwamba changamoto wanazokutana nazo walimu zinafanana kwa kiasi kikubwa, wale wanaofundisha shule za vijijini wanakabiliwa na matatizo mengi zaidi, ambayo ikiwa yatatuliwa mapema, yatakuza ubora wa elimu nchini.

Hadi kufikia Disemba 2016, takwimu kutoka Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) zinaeleza kuwa kulikuwa na walimu 272,264 wa shule za msingi na sekondari kutoka 153, 767 mwaka 2005. Hata hivyo, idadi kubwa ya walimu hawa wanafundisha shule za mijini.

Pamoja na ongezeko hilo la walimu, uchambuzi wa takwimu kutoka kituo cha takwimu huru cha Serikali kuhusu uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi kwa mwaka 2016 uliofanywa na gazeti hili, umebaini shule nyingi za vijijini zina uhaba mkubwa wa walimu.

Gazeti hili lilifanikiwa kutembelea baadhi ya shule zilizopo vijijini katika mikoa ya Morogoro, Tabora na Kigoma ili kujionea namna walimu wanavyoweza kumudu majukumu yao na njia zinazoweza kuboresha elimu katika shule hizo, baada ya takwimu kuonyesha zina uhaba mkubwa wa walimu.

Tofauti za walimu wenzao waliopo mjini, walimu wa vijijini wanakumbana na changamoto lukuki zikiwemo kukosekana kwa makazi, shule kujengwa katika maeneo yasiyofikika, kukosekana kwa huduma za jamii zilizopo karibu.

Hata hivyo, pamoja na yote haya, walimu katika shule hizo hufanikiwa kutimiza majukumu yao.

Katika Shule ya Msingi Igombe, iliyopo wilayani Kaliua, Tabora walimu wanaopangiwa kazi katika shule hii hulazimika kujenga nyumba zao za udongo kutokana na kata ya Zugimlole ilipo shule hiyo kukosa nyumba inayofaa kupangishwa.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Kasseka Iddy, ambaye ndiye mtumishi pekee anayeishi kwenye nyumba ya umma, anasema mwalimu mpya anapowasili katika shule hiyo hulazimika kukaa na mwenzake katika kipindi anachojenga nyumba yake.

Igombe ina walimu 12 wakiwemo 10 wa kiume na wa kike mmoja ambaye tayari ameshaomba uhamisho.

Uhaba wa makazi ya walimu bado ni tatizo kubwa katika sekta ya elimu pamoja na jitihada za Serikali kulitatua.

Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha ndani ya miaka sita, Serikali imefanikiwa kujenga nyumba 16,613 ikiwa ni ongezeko kutoka nyumba 41,835 mwaka 2010 hadi 58, 448 mwezi Februari mwaka jana. Idadi hiyo ni sawa na wastani wa nyumba 2,769 kwa mwaka.

Licha ya jitihada hizo, bado kuna maeneo yana uhaba mkubwa wa nyumba ikiwamo Kaliua yenye upungufu wa asilimia 95. Kwa mujibu wa Ofisa Elimu wa Wilaya, Flavian Nchimbi, mahitaji halisi ni nyumba 1,824 lakini zilizopo ni 324 tu.

Mbali na makazi, baadhi ya shule zipo pembezoni kiasi cha kuwalazimu walimu hutumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya safari za kiofisi ama safari zao binafsi na wakati mwingine hulazimika kutembea kwa miguu kwa kuwa magari hayafiki maeneo wanayoishi.

“Maisha ni magumu kwa sababu wakati mwingine inanipasa kutumia hadi Sh120, 000 kwa mwezi kwa ajili ya safari za kiofisi. Gharama za chini ni Sh40, 000 ambayo ni lazima kwa ajili ya ratiba ya kupeleka ripoti ya mwezi ya shule,” anasema Iddy na kuongeza:

“Kiasi hiki siyo sehemu ya bajeti ya shule na hivyo huwa inanipa changamoto wakati mwingine. Japokuwa nina changamoto nyingi hapa shuleni lakini tukipatiwa hata pikipiki moja tu itatusaidia.’’

Katika kata ya Zugimlole ilipo shule hii, hakuna kituo cha afya cha karibu, hivyo wakazi wake hulazimika kutumia kituo cha afya kilichopo kijiji cha pili. Pia, katika kata hiyo iliyopo katikati ya Hifadhi ya msitu wa Igombe, hakuna umeme huku wakazi wake wakitegemea maji yatokanayo na visima vifupi.

Mbunge wa jimbo la Kaliua, Magdalena Sakaya anasema hizo ni sehemu ya changamoto zinazowakabili wananchi wa eneo hilo, kwa kuwa kuna wakati njia hazipitiki na wengi hulazimika kutumia baiskeli.

Walimu katika shule hizi hufanya kazi kupita kiasi kutokana na uchache wao na hivyo kuathiri utendaji wao wa kazi.

Shule yenye walimu wawili

Katika Shule ya Msingi Chohero iliyopo Mvomero mkoani Morogoro, walimu wawili hulazimika kufundisha wanafunzi kuanzia awali mpaka darasa la saba.

Shule hiyo iliyokuwa na wanafunzi 510 kabla ya darasa la saba kuhitimu mwaka jana, imekuwa ikifanya vibaya katika mitihani ya Taifa na mwaka jana ilikuwa miongoni mwa shule 10 za mwisho katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Benard Pius anasema tatizo siyo wingi wa wanafunzi bali idadi ya masomo na vipindi ambavyo husababisha walimu kutumia muda mrefu zaidi kusahihisha madaftari hivyo kuathiri shughuli za kuandaa maandalio ya masomo.

“Inakubidi sasa ufundishe vipindi utakavyoweza kuvimudu. Mimi huwa nahakikisha wanafunzi katika madarasa haya wanajua kusoma, kuandika na kuhesabu. Vipindi vingine kama afya na michezo tunavifundisha mara chache ,” anasema mwalimu Pius.

Walimu katika shule hii hutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 20, kutokana na shule kujengwa milimani sehemu ambayo magari hayawezi kufika.

Shule za Kigoma

Changamoto hizi zinawakumba pia walimu wanaofundisha katika baadhi ya shule za msingi mkoani Kigoma.

Kwa mfano, licha ya Shule ya Msingi Muhamani kutokuwa mbali na Kigoma mjini, walimu katika shule hii wanakumbana na changamoto zilezile wanazokumbana nazo walimu wa shule nyingi za vijijini.

Tofauti na wenzao wa mjini, walimu katika shule ya Muhamani wanalazimika kuandaa kila kitu ikiwamo ripoti za shule kwa kuziandika kwa mkono, kwao kompyuta ni ‘anasa’.

Wakati mwandishi wetu anamtembelea, Mwalimu Mkuu wa Muhamani, Michael Kipara alikuwa amemalizia kuandaa taarifa ya mwezi yenye kurasa sita iliyokuwa imeandikwa kwa ustadi mkubwa kupitia kalamu ya wino.

“Hatuna namna zaidi ya kuzoea hali hii, inampasa mwandaa ripoti kuandika karatasi nyingi zilizokosewa kabla ya kuwa na moja iliyokaa vizuri. Hapa kwetu kila kitu kinaandikwa kwa mkono ikiwamo mitihani isipokuwa ile ya kitaifa,” anasema.

Shule hiyo ina vyumba vinne vya matofali vinavyotumika kufundishia darasa la pili hadi la saba, huku darasa la kwanza wakisomea katika darasa la miti lililoezekwa kwa nyasi. Wanafunzi wa awali wanajifunzia chini ya mti wa mwembe.

Kwa walimu wa shule ya msingi Bondo ambayo pia ipo Wilaya ya Kigoma vijijini, walimu hulazimika kutumia ofisi ndogo yenye viti vitano tu ambayo shule huifanya pia kama ghala.

Shule hiyo yenye walimu 10 kwa mujibu wa Mwalimu Mkuu, Seth Bigera, ilianzishwa baada ya kugawanywa kwa Shule ya Msingi Kasuku ambayo ilikua na wanafunzi wengi.

Hadi sasa Bondo inaendelea kutumia madarasa na vyoo vya Kasuku, huku ikiwa ina chumba kimoja kidogo kinachotumiwa kama ofisi ya walimu na stoo.

“Unisamehe bure kama unavyoiona ofisi yetu,” alisema Bigera huku akimkaribisha mwandishi wetu alipowasili shuleni hapo.

Kimuonekano, ofisi hii ndogo yenye dirisha moja ni kama stoo kutokana na kujaa vitu vya kufanyia usafi, bustani, vitabu na vyombo vya jikoni.

Pamoja na changamoto hiyo, Mwalimu Bigera ana furaha kuifanya shule hiyo kuwa na kiwango kizuri cha ufaulu. Katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi wa mwaka 2016, wanafunzi wote waliofanya mtihani walifaulu, kiwango kilichopanda kutoka asilimia nane mwaka 2012.

Tofauti walimu wa mjini na vijijini

Ijapokuwa ni ukweli kwamba changamoto zinazowakabili walimu nchini zinafanana, kuna tofauti kubwa kati ya walimu wanaofundisha shule za mijini ukilinganisha na mjini.

Wakati usafiri ni shida Chohero au matumizi ya kompyuta ni anasa huko Muhamani, walimu wa Ahule ya Msingi Mzinga au Kongowe jijini Dar es Salaam hutumia dakika tatu tu kufika kituo cha daladala. Wakati huo huo, walimu hao kutumia kompyuta kuandaa taarifa zao za maendeleo ya shule na hata kama hawana, hutumia huduma za kiofisi zinazotolewa jirani na shule.

Katibu wa Chama cha Walimu (CWT), Ezekiel Olouch anasema matatizo ya upungufu wa nyumba, walimu na vifaa vya kufundishia ni sehemu tu ya changamoto za walimu wa vijijini.

‘’Kuna baadhi ya mikoa walimu huchapwa, hurogwa na hata kufukuzwa na wananchi kutoka katika vijiji wanavyofundisha,” anaeleza.

Anasema Serikali haina budi kuandaa posho ya mazingira magumu kazini kwa walimu wa vijijini ili kuwapa motisha ya kazi.

“Unajua asilimia 75 ya idadi ya watu nchini wanaishi mikoani (vijijini) hii ina maana hata wingi wa shule zipo huko, lakini cha ajabu idadi kubwa ya walimu wapo mijini na hata huduma bora za jamii zipo mijini. Pia, hii inasababisha shule zetu za pembezoni kuendelea kupokea walimu wachache,” anasema.

‘’Kama changamoto hizi hazitaboreshwa, ufaulu katika shule za vijijini utakua ni ndoto,’’ anasema Meneja wa Utafiti na Uchambuzi wa asasi ya kiraia ya HakiElimu, Godfrey Boniventura.

Anashauri Serikali kufikiria katika bajeti zijazo kuhakikisha inasogeza huduma za jamii na kuboresha miundombinu katika maeneo karibu na shule zilizopo pembezoni ili kutoa ahueni kwa wananchi na watumishi hao.

“Mwalimu huyu ambaye tangu anaanza shule ya msingi anasoma katika shule na vyuo binafsi huku akiwa anapata huduma muhimu kwa urahisi, anapangiwa kwenda kufudisha shule ambayo kupata dawa ya kupigia mswaki inampasa kutembea kilomita 20. Kwa hali hii, hakuna mwalimu anayeweza kuhimili haya,” anasema Boniventura.

Kauli ya Serikali

Mkurugenzi Usimamizi wa Elimu wa Ofisi ya Raisi-Tamisemi, Juma Kaponda, anasema Serikali inazifanyia kazi changamoto hizi na tayari mwaka huu ina mpango wa kuajiri walimu 40,000 wa shule za msingi na 10,169 wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa shule za sekondari ambao wengi wataelekezwa katika shule za pembezoni.

“Hawa walimu safari hii hawatapelekwa kwenye halmashauri, bali watapangiwa moja kwa moja vituo vya kazi kutoka wizarani; lengo ni kupunguza uhaba katika shule zetu za mikoani.

“Halmashauri pia zimetakiwa kuhakikisha zinagawanya walimu kutoka maeneo ambayo yana ziada na kupeleka maeneo yenye upungufu,” anasema Kaponda.

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania