Uhaba wa meli Ziwa Victoria warudisha nyuma maendeleo Kanda ya Ziwa

Nuzulack Dausen
March 27, 2017

Peter Saramba, Mwananchi

[email protected]

Mwanza. Huduma za uchukuzi ndani ya Ziwa Victoria zinaendelea kuzorota mwaka hadi mwaka licha ya mahitaji ya kusafirisha abiria na mizigo kupaa.

Wakati Bandari ya Kanda ya Ziwa inaanzishwa mwaka 2006, kwa mujibu wa Meneja wa Bandari Kanda ya Ziwa, Abel Moyo lengo lilikuwa kuhudumia abiria milioni moja kwa mwaka. Kiwango hicho pia kiliwekwa katika kusafirisha tani za mizigo.

Hata hivyo, siyo tu lengo hilo halijafikiwa, bali pia idadi ya abiria na mizigo inayosafirishwa kwa njia ya maji inapungua kila mwaka.

Kuzorota kwa huduma ya usafirishaji majini

Uchambuzi wa takwimu kutoka Bandari za Ziwa Victoria unaonyesha kuwa abiria 892, 000 walisafirishwa Mwaka 2006/7, kiwango cha juu kuwahi kufikiwa.

Lakini idadi hiyo imeporomoka zaidi ya mara nne ndani ya kipindi cha miaka kumi hadi kufikia abiria 209, 000 mwaka 2015/16, licha ya wananchi na wafanyabiashara kuzihitaji huduma hizo kwa hali na mali.

Sanjari na abiria, mizigo inayosafirishwa kupitia bandari za ziwa hilo kubwa kuliko yote Afrika, pia imepungua takriban mara nne.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa shehena hiyo imepungua kutoka tani 480, 000 mwaka 2006/7 hadi kufikia tani 126, 000 pekee mwaka 2015/16 licha ya usafiri huo kuwa nafuu kuliko barabara na ndege.

Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wanasema iwapo hali hiyo itaendelea itasababisha kushuka kwa biashara na kuikosesha Serikali mapato kutoka katika kanda hiyo muhimu inayounganisha mataifa jirani ya Uganda na Kenya.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa miongoni mwa sababu zilizosababisha hali hiyo ni kuyumba kwa huduma za usafirishaji zinazotolewa na Kampuni ya Huduma za Meli nchini (MSCL), kunakochagizwa na uchakavu wa meli zake zinazoharibika mara kwa mara.

“Usafirishaji wa abiria na mizigo ndani ya Ziwa Victoria kunategemea ufanisi wa huduma za MSCL. Kuyumba kwa MSCL ni kuyumba kwa kila kitu kwenye sekta ya usafirishaji majini,” alisema Moyo

Hivi sasa, bandari za Ziwa Victoria zinategemea zaidi huduma za meli binafsi na zile zinazotoka nje ya nchi ambazo hata hivyo, idadi yake ni ndogo kulinganisha na mahitaji halisi.

Vyombo vya usafiri majini vyenye uwezo wa kubeba mzigo kuanzia tani 50 na kuendelea vilivyosajiliwa kutoa huduma ndani ya Ziwa Victoria kwa kipindi cha miaka 16 iliyopita ni 38 tu.

Ofisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra) Mkoa wa Mwanza, Michael Rogers alisema vyombo 15 kati ya hivyo ni kwa ajili ya kubeba abiria pamoja na mizigo wakati 13 ni vya kubeba mizigo pekee.

Wakati vyombo tisa vya abiria na mizigo vikiwa vinatoa huduma, sita havifanyi kazi kutokana na sababu kadhaa ikiwemo uharibifu.

Hali ni vivyo hivyo kwa upande wa vyombo vya mizigo pekee ambapo ni tisa ndivyo vinatoa huduma huku vinne vikiwa vimesimama.

Katika kipindi hicho kinachoanzia mwaka 2006 hadi mwaka jana, Sumtra pia ilisajili mitumbwi 12, 224 zenye ukubwa/urefu kuanzia mita nne hadi 24 ambayo bado haikidhi mahitaji.

“Usajili wa meli huwa hauongezeki mara kwa mara. Wakati mwingine unaweza kuchukua miaka mitatu hadi minne ndipo tunasajili meli moja,” alisema Rogers

Alipoulizwa iwapo vyombo vilivyopo vinakidhi mahitaji au kinyume chake, Ofisa huyo wa Sumatra alisema bado kuna uhitaji mkubwa huku akitolea mfano kutokuwepo meli inayosafirisha abiria kati ya jiji la Mwanza na Bukoba kama pengo kwenye sekta ya usafirishaji majini.

Ukosefu wa vyombo hivyo unawagharimu wananchi kiuchumi na kijamii.

Leticia Lusato, mmoja wa abiria aliyekuwa akisafiri pamoja na mwandishi wetu kwenye meli ya Mv Nyehunge kutoka jijini Mwanza kwenda Visiwa vya Ukerewe Machi 3, mwaka huu alisema ukosefu wa usafiri wa uhakika ndani ya ziwa hilo siyo tu kunafifisha uchumi, bali pia ni kikwazo kwa huduma za dharura za afya kwa wakazi ukanda huo.

“Kwa mfano, kuna safari mbili pekee kwa siku kutoka na kwenda Ukerewe.

“Baada ya Saa 6:00 mchana ambao ndio muda wa mwisho kwa meli kutoka na kwenda Ukerewe mgonjwa anayehitaji dharura ya rufaa kwenda hospitali ya Rufaa ya Bugando atalazimika kusubiri siku inayofuata,” alisema Lusato.

Mkazi huyo wa kijiji cha Mugu, wilaya ya Ukerewe anashauri angalau ziwepo safari nne kwa siku kutoka na kwenda Ukerewe badala ya mbili za sasa.

Uchakavu, ubovu wa Meli za MSCL

Tangu mwaka 1988, hakuna meli mpya iliyoundwa. Meli zote 14 za abiria na mizigo zinazomilikiwa na Kampuni ya Meli nchini zimeundwa kati ya mwaka 1938 hadi 1988.

Meneja wa MSCL tawi la Mwanza, Philemon Bagambilana alisema kati ya meli 14 walizonazo, ni tatu pekee zinazotoa huduma hivi sasa ambazo ni Mv Crarias (Ziwa Victoria- kituo cha Mwanza), Mv Songea (Ziwa Nyasa- kituo cha Kyela) na Mv Liemba inayotoa huduma Ziwa Tanganyika-kituo cha Kigoma.

Tazama video hii kupata habari zaidi kuhusu tatizo la usafiri Ziwa Victoria

Pamoja na Ziwa Victoria, Kampuni ya Meli yenye Makao yake Makuu jijini Mwanza, pia ina dhamana ya kusimamia na kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo ndani ya Nyasa na Tanganyika.

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Meneja Mkuu, Eric Hamisi, Bagambilana alisema MSCL pia inadhamana ya usafirishaji wa abiria na mizigo inayokwenda na kutoka katika nchi jirani za Kenya, Uganda na Malawi kupitia Maziwa Makuu ya Victoria, Nyasa na Tanganyika.

Kitakwimu, Meli za MSCL zina uwezo wa kubeba abiria 3, 970 na tani 3, 915 za mizigo kwa wakati mmoja iwapo zote zitatoa huduma kulingana na uwezo.

Meli mpya, Kete ya kisiasa Kanda ya Ziwa

Shida ya uchukuzi inayowakabili wananchi kanda ya ziwa hasa mikoa ya Mwanza na Kagera ni moja ya kete za kisiasa zilizotumika mara nyingi na vyama na wagombea wao nyakati za kampeni.

Katika kampeni za uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, wagombea urais kupitia vyama vya CCM, John Magufuli aliyeibuka mshindi, na aliyekuwa mshindani wake Mkuu, Edward Lowassa wa Chadema wote kwa nyakati tofauti walitoa ahadi ya Meli mpya kwa wakazi wa mikoa ya Mwanza na Kagera.

Rais Magufuli amerejea ahadi hiyo alipohutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza mwezi Agosti, mwaka jana.

Iwapo mambo yataenda kama alivyoahidi Rais Magufuli, meli mpya inatarajiwa kupatikana na kuanza kutoa huduma ifikapo mwaka 2018 na kuwapunguzia adha wananchi wa ukanda huo.

Katika bajeti ya sasa ya 2016/2017, Bunge lilipitisha Sh50.5 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli mbili zinazomilikiwa wa MSCL.

Kutokuwepo kwa usafiri wa uhakika wa abiria na mizigo ndani ya Ziwa Victoria siyo tu ni adha kwa abiria na wafanyabiashara ambao sasa hutumia usafiri wa barabara na anga wenye gharama kubwa kuliko wa majini, bali pia kunaikosesha Serikali mapato yatokanayo na kodi na ushuru mbalimbali.

Hali hiyo inafanya baadhi ya bidhaa kuuzwa bei ya juu kuliko kawaida jambo linalowafanya wakazi wa maeneo hayo kutoboa zaidi mifuko yao kumudu kupata mahitaji yao muhimu.

Gharama za usafiri, usafirishaji

Mfanyabiashara wa ndizi kati ya Bukoba na Mwanza, Christina Mshomi alisema hivi sasa anauza mkungu mmoja wa ndizi kati Sh25, 000 hadi Sh35, 000 ili kumudu gharama na kupata faida kutokana na kulazimika kusafirisha mizigo yao kwa njia ya barabara.

“Wakati tukitumia usafiri wa meli kusafirisha mizigo tulikuwa tukiuza mkungu mmoja ndizi kati Sh15, 000 hadi Sh20, 000,” alisema Mshomi.

Fabian Kaijage ambaye pia ni mfanyabiashara wa duka la rejareja mjini Bukoba alisema bei kubwa ya nauli na gharama ya usafirishaji inawalazimu kuuza bidhaa kwa bei ya juu kulinganisha na wanapotumia njia ya maji kuagiza bidhaa hizo.

“Nauli ya meli kati ya Bukoba na Mwanza ni Sh16, 500 kulinganisha na Sh20, 000 hadi Sh25, 000 ya basi,” Kaijage anasema

Kushuka kwa mapato ya Bandari Ziwa Victoria

Bandari za Ziwa Victoria pia inakabiliwa na changamoto ya kupoteza mapato hali ambayo imechochewa na kushuka kwa shehena ya mizigo na abiria.

Bosi wa Bandari Kanda ya Ziwa, Moyo analia na kuzoroto kwa huduma za Kampuni ya Meli nchini (MSCL), Kampuni ya Reli nchini (TRL), pamoja na uwepo wa bandari binafsi kuwa miongoni mwa sababu kuu za mapato ya bandari kupungua.

Alisema kutokuwepo meli na usafiri wa uhakika wa reli kumepunguza idadi ya abiria na mizigo inayosafirishwa kwa njia ya maji siyo tu mikoa ya Kanda ya Ziwa, bali pia nchi jirani za Kenya na Uganda.

“Bandari bubu zinazotoza gharama kulingana na makubaliano kati yao na wasafirishaji badala ya viwango vya Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), siyo tu zinapunguza ufanisi wa bandari Kanda ya Ziwa, bali pia mapato ya serikali,” alisema Moyo

Alisema bandari bubu hizo pia ni tishio kiusalama kwa sababu zinaweza kutumiwa kusafirisha au kuingiza bidhaa haramu zikiwemo zana haramu za uvuvi, wahamiaji na silaha.

Sheria ya bandari ya mwaka 2004 inayoruhusu Meli za MSCL kutolipia huduma za bandari pia inatajwa na Moyo kuwa ni miongoni mwa vikwazo vya mapato yanayotokana na idadi ya meli zinazotia nanga katika bandari za Ziwa Victoria.

Meli kubwa kushindwa kutia nanga

Hata wakati kukiwa na upungufu wa meli zinazofanya safari katika ziwa hilo, bado baadhi ya vyombo vikubwa vinashindwa kutia nanga kutokana na kujaa mchanga.

Hali hiyo inatajwa na mamlaka ya bandari kuwa inachangia pia kushusha mapato yake kwa kuwa meli kubwa hubeba shehena kubwa kwa wakati mmoja.

Mtaalam wa masuala ya uchumi na uwekezaji, Bonventura Mendeka alisema sekta ya usafirishaji majini Kanda ya Ziwa ni fursa ya kiuchumi iliyolala.

Alisema iwapo itaimarishwa na kutumiwa vyema siyo tu itaongeza pato la mwananchi mmoja mmoja, bali pia itatunisha hazina za Serikali za Mitaa na Serikali Kuu ambazo zimekuwa zikihaha kupata fedha za kugharamia miradi ya maendeleo.

Serikali inajua tatizo la usafiri linalowakabili wakazi wa kanda ya ziwa.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa anasema kuanzia mwaka ujao wa fedha, Serikali itatenga bajeti ya kukarabati meli zake na kujenga zingine mpya katika Maziwa yote matatu ya Victoria, Nyasa na Tanganyika.

“Kwa upande wa Ziwa Victoria tutaanza na ukarabati wa meli za Mv Victoria na Mv Serengeti pamoja na ununuzi wa meli mpya ya kisasa aliyoahidi Rais John Magufuli,” anasema Profesa Mbarawa

Kwa mujibu wa Profesa Mbarawa, Serikali pia imelazimika kubeba dhamana ya kuisaidia MSCL kwa kutoa Sh100 milioni kati ya Sh126 milioni zinazohitajika kulipia mishahara ya wafanyakazi wanaodai malimbikizo ya zaidi ya mwaka mmoja.

 

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania