Bajeti ya maendeleo, serikali yatoa theluthi moja

Nuzulack Dausen
March 29, 2017

Sharon Sauwa, Mwananchi

[email protected]

Dodoma. Miradi mingi ya maendeleo nchini huenda ikakwama kutokana na Serikali kutoa theluthi moja tu ya fedha zilizotengwa kwa ajili hiyo katika bajeti yake ya mwaka 2016/17.
Kuchelewa kutolewa kwa fedha hizo ikiwa imebaki miezi minne kwa bajeti hiyo kumalizika, kunatokana na sababu mbalimbali ikiwamo kuchelewa kwa misaada na mikopo kutoka nchi wahisani.
Wakati hali ikiwa hivyo, Serikali katika mwaka ujao wa fedha imepanga kukusanya na kutumia Sh31.69 trilioni ikilinganishwa na Sh29.5 trilioni za bajeti ya mwaka huu huku uwiano wa bajeti ya maendeleo ukishuka hadi kufikia asilimia 38 kutoka 40 ya mwaka huu.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliwaeleza wabunge jana kuwa hadi Februari mwaka huu, fedha zilizokuwa zimetolewa kwa ajili ya maendeleo ni Sh3.97 trilioni kati ya Sh11.8trilioni zilizopitishwa na Bunge Juni, mwaka jana kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Dk Mpango aliyekuwa akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa, Kiwango na Ukomo wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2017/18, alisema fedha hizo zilizotolewa ni sawa na asilimia 34 ya zinazotakiwa hadi Juni. Fedha zilizotolewa zinajumuisha Sh871.8 bilioni kutoka nje.


Serikali kukosa mkopo
Dk Mpango alisema Serikali imeshindwa kupata mkopo wa nje wenye masharti ya kibiashara katika bajeti ya mwaka 2016/17 kutokana na hali ya soko la fedha la kimataifa kutokuwa nzuri hasa katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka huo wa fedha. Katika kikao hicho kilichofanyika bungeni na kuongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, waziri huyo alisema katika mwaka wa fedha unaomalizika, Serikali ilipanga kukopa katika vyanzo vya kibiashara Sh2.1 tirioni ili kugharamia miradi ya maendeleo nchini.

Hata wakati wakipanga hivyo, alisema ndani ya kipindi hicho riba ilipaa kutoka wastani wa asilimia sita hadi asilimia tisa.
“Kutokana na sababu hiyo Serikali iliahirisha mchakato wa kukopa kutoka kwenye masoko hayo,” alisema.
Hata hivyo, Dk Mpango aliwaeleza wawakilishi hao kuwa gharama ya ukopaji katika masoko ya Ulaya imeanza kuimarika.
Alisema Serikali imeshasaini mkataba na Kuwait Fund wa Dola 51 milioni za Marekani kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Chaya hadi Nyahua.

Pia, alisema Serikali itasaini hivi karibuni mkataba na Opec Fund wa Dola 18 milioni za Marekani na Abu Dhabi Fund For Development (ADFD) wa Dola 15 za Marekani kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Uvinza – Ilunde – Malagarasi.

Bajeti ya Sh31.6 trilioni
Dk Mpango alisema Serikali katika mwaka wa fedha 2017/18 inatarajiwa kukusanya na kutumia kiasi cha Sh31.6 trilioni.
Bajeti hiyo ni sawa na ongezeko la Sh2.6 trilioni ya bajeti iliyopitishwa na Bunge katika mwaka wa bajeti 2016/17.
Pia katika bajeti hiyo, fedha za maendeleo zimeongezeka kutoka Sh11.8 trilioni bajeti ya mwaka 2016/17 hadi Sh11.9 trilioni mwaka 2017/2018 sawa na asilimia 38 ya bajeti yote inayopendekezwa.

Wahisani kuchangia asilimia 12
Dk Mpango alisema washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh3.971.1 trilioni ambayo ni sawa na asilimia 12.6 ya bajeti yote.
“Misaada na mikopo hii inajumuisha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, mifuko ya pamoja ya kisekta na kibajeti (GBS),” alisema.

Alisema Serikali inatarajia kukopa Sh6,156.7 bilioni kutoka soko la ndani na Sh4,948.2 bilioni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zilizoiva na Sh1208.4 bilioni sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

Alisema ili kuongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu, Serikali inatarajia kukopa Sh1.595 trilioni kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara.

Habari zaidi kuhusu bajeti

Vipaumbele
Dk Mpango alitaja vipaumbele vya mpango huo kuwa ni ujenzi wa reli hususan kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro (kilomita 205), kumpata mkandarasi wa kusanifu ujenzi kwa maeneo ya Morogoro hadi Makutopora (kilomita 336), Makutopora hadi Tabora (kilomita 294), Tabora hadi Isaka (kilomita 133) na Isaka hadi Mwanza (kilomita 249).

Pia kupata maeneo ya ardhi ya kuunganisha na kuanzisha treni kati ya Mpiji na Soga mkoani Pwani, Buhongwa (Mwanza) na Ihumwa Dodoma kwa ajili ya kituo kikubwa cha treni za mizigo na makasha.

Vipaumbe vingine ni kuhuisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kukamilisha ununuzi wa ndege tatu, mradi wa Liganga, makaa ya mawe Mchuchuma, kuanzisha kanda maalumu za kiuchumi, mradi wa Liquified Natural Gas, shamba la kilimo na sukari Mkulazi na kuhamishia shughuli za Serikali kuu Dodoma.

Habari zinazohusiana

Bajeti ya JPM mwanzo, mwisho

Changamoto za bajeti
Dk Mpango alisema changamoto za bajeti hiyo ni pamoja na utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/2017 hadi kufikia Februari, mwamko mdogo wa kulipa kodi hususan kuzingatia matumizi ya mashine ya kielektroniki.

Alisema nyingine ni kuchelewa kupatikana kwa mikopo yenye masharti nafuu na ya kibiashara kutoka nje na majadiliano ya muda mrefu yaliyosababisha kuchelewa kupatikana kwa fedha za washirika wa maendeleo.

Alisema Serikali itachukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kusimamia dhana ya kulipa kodi kwa hiari kupitia udhibiti wa matumizi ya EFD na kuendelea na majadiliano baina ya Serikali na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha fedha za misaada na mikopo nafuu zinapatikana kama zilivyoahidiwa.

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania