Nuzulack Dausen April 3, 2017
Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]
Dar es Salaam. Mbunge wa Igunga, Dk Dalaly Kafumu amesema uamuzi wa kupiga marufuku usafirishaji mchanga nje umekuwa wa haraka na unaweza kuipotezea nchi mapato.
Pia, ameitaka Serikali kuacha kuegemea dhana kuwa kampuni za nje zinazochimba madini ya dhahabu zinaiibia nchi kutokana na kusafirisha mchanga nje.
Dk Kafumu amesema kuna dhana potofu inayoendelea kuenea kuwa kampuni hizo zinasafirisha mchanga wote zinaouchimba badala ya kuchenjua kwanza na kuutenganisha na dhahabu kwenye migodi yao ya hapa nchini.
Mtaalamu huyo wa miamba na madini amesema Tanzania inaweza kujenga kinu chake cha kuyeyusha mchanga huo, lakini baada ya kufanya maandalizi ya kutosha tofauti na hatua za sasa za kupiga marufuku kusafirisha nje mchanga huo kabla ya kupata uwezo wa kuuchakata.<img src="http://” alt=”Mbunge wa Igunga, Dk Dalaly Kafumu” />
Kampuni ya Acacia, inayomiliki migodi ya dhahabu ya Bulyanhulu na Buzwagi, husafirisha mchanga huo kwenda nje kwa ajili ya kuuyeyusha kupata masalia ya madini, na hasa shaba ambayo ni zaidi ya asilimia 16 ya mchanga huo, huku dhahabu na fedha zikiwa na asilimia 0.02 kila moja.
Serikali, ambayo ilishawahi kuunda kamati kuangalia uwezekano wa kujenga kinu hicho hapa nchini, haijashawishika na maelezo ya wawekezaji hao na Mamlaka ya Ukaguzi na Udhibiti wa Madini (TMAA) kuhusu kiwango cha madini kwenye mchanga huo na juzi Rais John Magufuli aliunda timu ya wataalamu kuchunguza, huku Spika John Ndugai akiahidi kuunda kamati itakayoangalia mchakato mzima.
Kwa mujibu wa tangazo la Machi 28 la Acacia, tangu kutolewa kwa amri ya kuzuia mchanga kusafirishwa nje, makontena 256 yamezuiwa katika bandari kavu ya kampuni ya ZamCargo (awali ikijulikana kama Mofed, Customs Freight Services, CFS). Acacia pia imesema makontena 21 yako Bandari ya Dar es Salaam ambako yalikuwa yakisubiri kusafirishwa baada ya taratibu zote za kodi na ushuru kukamilika.
Dk Kafumu atoa ufafanuzi
Akizungumza na Mwananchi jana, Dk Kafumu alisema Serikali haina budi kuacha kuegemea zaidi katika dhana kuwa Taifa linaibiwa dhahabu.
Dk Kafumu alisema si sahihi kudhani madini yanaibiwa kutokana na mchanga kusafirishwa nje kwenda kuyeyushwa ili kupata madini yaliyosalia baada ya dhahabu kuondolewa wakati wa kuchenjua mchanga kwenye vinu vilivyo katika migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi.
Dk Kafumu aliyejiuzulu hivi karibuni uenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, alisema zuio hilo linaweza kusababisha wawekezaji hao kuondoka nchini.
“Serikali imekaa katikati ya wananchi na mwekezaji, hivyo ikiegemea tu kwenye dhana ya wananchi, mwekezaji lazima aumie. Kwa mfano Serikali kwa sasa imeegemea kabisa kwa wananchi, kwa dhana kwamba tunaibiwa dhahabu, kwa hiyo huyu mwekezaji hata-survive lazima aondoke,” alisema Dk Kafumu.
Alisema hatua ya kupiga marufuku kusafirisha mchanga nje imekuwa ya dharura na hivyo inaweza kusababisha nchi kuathirika.
Alisema kitendo hicho kinaweza kusababisha kuharibu uhusiano wa Tanzania na kampuni za nje.
“Hili linaweza hata kutupotezea mapato. Nia njema na nzuri ya Rais ni lazima iendelezwe kwa kumshauri. Tena (Rais) aangalie namna bora zaidi ya kufikia malengo haya mazuri ya Sera ya Madini ya mwaka 2009,” alisema Dk Kafumu.
Alisema sera hiyo inataka Serikali ishirikiane na sekta binafsi, kanda na mashirika ya kimataifa kuweka mkakati ya kuwekeza mtambo wa kuyeyusha mchanga kwa ajili ya kupata shaba na madini mengine ambayo yalishindikana kupatikana katika uchenjuaji wa awali unaofanywa hapa nchini.
Dk Kafumu alisema wakati akiwa kamishna wa madini, alipokea ripoti kutoka jopo la wasomi waliozunguka nchi za Canada, Afrika Kusini na Japan na baadaye aliunda kamati ndogo ya kufanya uchambuzi ili kuangalia uwezekano wa kufanya marekebisho katika sekta hiyo.
“Walinipa ripoti hiyo kama ushauri, nikasoma na tukaona kuna mambo ya kurekebisha mara moja. Lakini huwezi kurekebisha kwa mdomo ni lazima utengeneze sera mpya. Tukaanza kurekebisha sera ya madini ya mwaka 1997 na tukapata sera ya 2009,” alisema.
“Lakini pia tukarekebisha sheria ya mwaka 2010 na kanuni zake,”
Dk Kafumu alisema kutokana mvutano wa sakata la usafirishaji wa mchanga huo, walipendekeza mambo kadhaa katika sera, kama kuhamasisha ujenzi wa kinu cha kuchenjua mchanga.
“Kwamba Serikali ikishirikiana na taasisi za nje zenye taaluma, na kampuni zihamasishe ujenzi wa smelter (kinu cha kuyeyusha mchanga) nchini,” alisema.
“Sasa sera huwa inatafsiriwa na sheria, kwa hivyo sheria ilitakiwa itafsiri hili jambo, lakini si kwa haraka. Ilitakiwa tuanze mazungumzo, kwamba jamani tunawezaje kuianzisha hii smelter.
“Ikishindikana, nilivyokuwa nafikiria mimi, wangeweza wakazungumza na nchi nyingine za Afrika, kama tatizo ni material (nyenzo) au ni teknolojia, tungewashawishi wangeweza kuleta hapa.”
Dk Kafumu alisema aliachia nafasi hiyo mwaka 2011 wakati akiwa ameshajipanga kufanya majadiliano na kampuni za madini.
Alisema baada ya kufanya marekebisho ya sheria ya madini, walianza kushawishi kampuni hizo kukubaliana na mabadiliko ya sheria kwa kujenga kwanza kinu cha kuyeyusha mchanga kabla ya kuzuia usafirishaji nje ya nchi. “Tulianza kuzungumza nao waingie kwenye mfumo mpya. Kwa mfano walikubali kulipa mrabaha, kujisajili soko la hisa,” alisema
Alipoulizwa inakuwaje zuio linafanyika kwa sasa angali bado hata mchakato wa ujenzi haujafahamika, Dk Kafumu alisema hiyo ni changamoto kwa taifa.
“Hiyo ndiyo changamoto sasa tulikuwa tunaizungumza hapa, yaani unaamua jambo ambalo rules (kanuni) zake ziko kinyume. Lakini ukishaambiwa uache, inabidi uache!” alisema.
Alipendekeza kuwa pamoja na uchunguzi unaofanywa na Serikali kwa sasa, upo uwezekano wa kujenga kinu hicho nchini kwa kufanya mazungumzo na nchi zinazofanya shughuli hizo barani Afrika.
Kuhusu mazingira magumu ya kuwekeza mtambo huo hapa nchini, Dk Kafumu alisema haiondoi uwezekano wa majadiliano ili kusimika mtambo huo nchini.
“Kama material yetu hayatoshi tunaweza kuzungumza na Ghana na DRC (Congo) tukajenga hapa nchini mtambo huo. Kwa mfano, Mzee Thabo Mbeki akiwa Rais wa Afrka Kusini alifanya mazungumzo na kampuni na akafanikiwa kujenga smelter kubwa ya alminium. Sasa hata sisi tunaweza kuzungumza ili tusiwe tunapeleka huko mbali, inawezekana,” alisema.
Kwa mujibu wa tafiti, kinu cha kuyeyusha mchanga wa shaba kinagharimu kuanzia dola 500 milioni za Kimarekani na ili kiweze kufanya kazi kibiashara, ni lazima kiwe kinapata mchanga wa kuanzia tani 150,000 kwa mwaka.
Uwezo wa Tanzania ni kuzalisha takriban asilimia 30 ya mahitaji ya kinu kama hicho, jambo litakalolazimisha nchi kuagiza asilimia nyingine 60 au 70 ya mchanga kutoka nje iwapo itaamua kujenga kinu chake hapa nchini.
Pia ili kujenga kinu hicho, kunahitaji umeme wa kutosha na teknolojia ya kusafisha kemikali zinazotumika ili zisiharibu mazingira.
Kuhusu mawazo kuwa wawekezaji wanaiibia nchi kwa kusafirisha mchanga wote inayochimba bila ya kuondoa dhahabu kwanza na kufanya mchanga huo kuwa na asilimia 90 ya dhahabu, Dk Kafumu alisema hiyo ni dhana potofu.
Alisema tangu mwaka 2001 mgodi wa Bulyanhulu ulipoanza kusafirisha makinia hayo, sheria imekuwa ikilazimisha mchanga uchenjuliwa katika mitambo ya hapa nchini.
“Maelekezo katika Sheria ya Madini ya Mwaka 1998, yaliagiza kwamba usafirishaji huo utafanyika baada ya mchanga unaochimbwa kuchakatwa. Hawezi kusafirisha mchanga bila kuuchakata kwanza katika mitambo hapa nchini (kupata dhahabu). Na ule si mchanga wa madini, bali ni copper concentrate (mchanga wa shaba),” alisema.
Habari zinazohusiana:
Agizo la JPM lazuia makontena 262 ya mchanga
Waziri Mkuu achukua sampuli za mchanga wa madini
Taarifa ya Acacia
Katika taarifa yake ya juzi, Acacia imesema kuwa kila inachofanya kinakaguliwa na TMAA na kila kontena linalotakiwa kusafirishwa huchukuliwa sampuli chini ya usimamizi wa wakala huo na kampuni ya SGS ili Acacia na Serikali ziweze kukisia kiwango cha shaba, dhahabu na fedha kilichomo.
“Matokeo ya mchakato huo wa upimaji hupelekwa TMAA, Mamlaka ya Mapato, Acacia na kampuni inayoyeyusha kwa ajili ya kuamua kuamua kiwango cha mrabaha kinachotakiwa kulipwa kabla ya kusafirishwa,” inasema taarifa hiyo ya Acacia.
“Ni pale tu uchukuaji sampuli na mrabaha kulipwa kwa Serikali, ndipo makontena hufungwa na kuwekwa lakiri rasmi na TMAA, MEM na TRA, na mchanga wetu wa dhahabu/shaba unaweza kuondoka mgodini.
“Baadaye makonteina husafirishwa kwa malori kwenda ofisi za ushuru za TRA zilizoko Isaka ambako nyaraka za mwisho za kusafirishwa nje hutolewa na MEM na TRA na makontena kukaguliwa kwa ajili ya kupelekwa Bandari ya Dar es Salaam.
“Baada ya utoaji huo wa nyaraka na kuthibitishwa na maofisa wa forodha, kila kontena hukaguliwa kwa vifaa maalumu bandarini na maofisa wa TRA na forodha kuhakikisha kuwa hayajachanganywa na vitu vingine.”
Acacia pia imesema iko tayari kuongea na Serikali kuhusu uwezekano wa kujenga kinu hicho hapa nchini.
“Acacia inaendelea kuwa tayari kushirikiana na Serikali kutathmini uwezekano wa kuwa na kuyeyusha kibiashara hapa nchini, kitu ambacho kitaongeza ajira na kuendeleza sekta,” inasema taarifa hiyo.
Nuzulack Dausen
Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.