Unataka kujua uchumi unaendeleaje? Wiki hii si ya kukosa

Nuzulack Dausen
April 7, 2017

[email protected]

Siyo wiki ya kukosa. Kama wewe hupenda kufahamu mwenendo wa uchumi na maendeleo ya nchini basi wiki ijayo inayoanzia Aprili 10, 2017 haupaswi kukaa mbali na vyanzo vya taarifa mbalimbali nchini.

Ni wiki itakayokuwa na ripoti muhimu zinazoweza kutoa mwanga wa mahali tulipo na tunapoelekea kiuchumi ikiwemo bajeti ya pili ya Serikali ya Rais John Magufuli.

Katika wiki hiyo, Benki ya Dunia (WB) itatoa ripoti ya mwenendo wa uchumi iitwayo ‘Money within reach: extending financial inclusion in Tanzania (Fedha ndani ya ulingo: Uboreshaji wa huduma jumuishi za kifedha Tanzania). Ripoti hiyo inatarajiwa kuzinduliwa Aprili 11.

Pamoja na kwamba WB haijaweka bayana muhtasari wa ripoti hiyo bila shaka kama zilizopita itakuja na mapitio ya mwenendo wa uchumi, matarajio na mapendekezo kutokana na inavyoutazama uchumi kwa sasa.

Taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa (UN) huhusika pia kushauri nchi mwanachama juu sera na mikakati mizuri ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo mbali na kutoa mikopo na misaada ya kifedha.

Ripoti hiyo inakuja wakati sekta binafsi ikipitia wakati mgumu baada ya mabadiliko ya mikakati ya kiuchumi ambayo yameshuhudia baadhi ya kampuni zikiripoti hasara na hata kupunguza wanyakazi.

Mbali na ripoti hiyo ya WB, pia Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) itakuwa ikitoa ripoti ya mwenendo wa mfumuko wa bei ambayo kiutaratibu hutolewa kila tarehe 8 ya mwezi. Hata hivyo, tarehe hiyo mwezi huu imeangukia wikiendi hivyo kuilazimu NBS kutoa ripoti hiyo Jumatatu.

Mfumuko wa bei umekuwa ukipanda mwezi hadi mwezi kutokana na kupanda kwa gharama za bidhaa na huduma hususan chakula. Hata hivyo, bado mfumuko huo upo ndani ya tarakimu moja.

Katika mwaka unaoishia Februari 2017, NBS ilieleza kuwa kasi ya mfumuko wa bei ilipaa hadi kufikia asilimia 5.5 kutoka 5.3 kwa mwaka ulioishia Januari.

Hata hivyo, kuna kila dalili ya kasi ya mfumuko huo kuendelea kupanda kwa mwaka ulioishia Machi, 2017 hivyo kuwafanya wananchi watoboe zaidi mifuko yao kununua bidhaa na huduma.

Mbali na ripoti hizo, huko mjini Dodoma Bunge linaendelea na vikao vya bajeti ambapo bajeti mbalimbali zinaendelea kusomwa na tayari bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ilisomwa Alhamis na itaanza kujadiliwa Jumatatu ya Aprili 10.

Ikiwa ni bajeti ya kwanza kuwasilishwa katika mwaka 2017/18, huenda wabunge wakaihoji zaidi juu ya mwenendo wa utekelezaji wa bajeti inayomalizika Juni mwaka huu. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameliomba Bunge liidhinishe Sh171.6 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo katika mwaka ujao wa fedha.

MwananchiData itakueletea uchambuzi wa ripoti hizi kwa kina.

 

 

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania