Miundombinu ya usafirishaji Ziwa Viktoria iimarishwe

Nuzulack Dausen
April 14, 2017

Peter Saramba, Mwananchi; [email protected]
Wajasiriamali wanaotaka kuwekeza katika sekta ya uchukuzi nchini wana fursa lukuki ndani ya Ziwa Viktoriabaada ya mahitaji ya usafiri wa majini kupaa wakati idadi ya meli kubwa ikizidi kupungua.

Hadi Machi mwaka huu, kati ya meli tisa za Kampuni ya Huduma za Meli nchini (MSCL) zilizotakiwa kufanya kazi katika ziwa hilo, ni moja tu ya MV Claris inayofanya kazi ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 293 na tani 10 za mizigo.

Iwapo meli zote za MSCL zingekuwa zinafanya kazi zingesaidia kuwasafirisha abiria 2,286 na tani 3,050 za mizigo kwa kila safari moja jambo ambalo lingepunguza shuruba ya usafiri wanayokabiliana nayo wananchi wa ukanda huo. Pamoja na meli za Serikali kususua, uwekezaji uliofanywa na sekta binafsi bado haukidhi mahitaji na usajili wa meli mpya hauridhishi kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra).

Takwimu za Sumatra zinaonyesha ndani ya miaka 16 iliyopita mamlaka hiyo imesajili vyombo 28 tu ndani ya Ziwa Viktoria vyenye uwezo wa kubeba zaidi ya tani 50 licha ya idadi ya watu na mahitaji ya bidhaa kupaa.
“Kati ya vyombo hivyo, 15 ni kwa ajili ya abiria na mizigo wakati 13 ni vya mizigo pekee,” anasema Ofisa Mfawidhi wa Sumatra Mkoa wa Mwanza, Michael Rogers.

“Hivi sasa, ni vyombo tisa pekee ndivyo vinatoa huduma ya kusafirisha abiria na mizigo baada ya vyombo sita kusimamisha huduma kutokana na uchakavu na kuharibika.”

Kwa upande wa mizigo, ni vyombo tisa ndivyo vinatoa huduma baada ya vinne kuharibika. Kati ya mwaka 2006 hadi 2016, Sumatra imesajili mitumbwi 12,224 yenye urefu kuanzia mita nne hadi 24 ambayo, hata hivyo, bado haikidhi mahitaji.

Rogers anasema kuna fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya usafirishaji ndani ya Ziwa Viktoria zikiwamo ujenzi wa meli, uendeshaji wa meli za kusafirisha abiria na mizigo na ujenzi wa maghala kati ya jiji la Mwanza na mji wa Bukoba na nchi jirani za Uganda na Kenya.

“Hadi sasa hakuna meli ya kubeba makontena ndani ya ziwa hili. Hii ni fursa ya kuchangamkiwa na watu wenye uwezo wa kuwekeza katika eneo hilo,” anasema Rogers.

Anasema mahitaji ya meli ya kubeba makontena yanaongezeka kutokana na mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge), itakayotumika kusafirisha mizigo kutoka jijini Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa na Uganda.

Licha ya kuongezeka mahitaji mapya ya huduma za usafiri wa majini, bado mahitaji ya zamani  hayajatimizwa na kila mwaka idadi ya abiria na mizigo inayosafirishwa inazidi kuporomoka kutokana na vyombo kuzidi kupungua.

1,010: Idadi ya meli za abiria zinazomilikiwa na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) .

Malengo ya awali ya Serikali wakati inaanzisha bandari katika Ziwa Victoria mwaka 2006 yalikuwa ni kusafirisha abiria milioni moja na tani za mizigo kwa hicho hicho kwa mwaka.

Lakini takwimu za Mamlaka ya Bandari Tanzania (Kanda ya Ziwa) zinaonyesha lengo hilo halijawahi kufikiwa kwa miaka 11 iliyopita. Badala yake, idadi ya abiria imeshuka mara nne kutoka watu 892,000 mwaka 2006/07 hadi abiria 209,000 mwaka 2015/16.

Mizigo inayosafirishwa kupitia bandari za ziwa hilo zilizopo katika miji ya Mwanza, Bukoba na Musoma imeporomoka kutoka tani 480,000 mwaka 2006/07 hadi tani 126, 000 mwaka 2015/16.

Meneja wa Bandari Kanda ya Ziwa, Abel Moyo anataja kusuasua kwa MSCL kusafirisha mizigo na abiria kuwa miongoni mwa sababu za kudorora kwa huduma za usafiri ndani ya ziwa hilo.

Uhaba wa meli ziwani humo umesababisha ufanyaji biashara katika ukanda huo kuwa ghali. Wafanyabiashara wa kanda hii wanaililia Serikali iongeze uwekezaji katika sekta ya usafirishaji wakisema ndiyo uti wa mgongo wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

“Uchumi wa Mji wa Bukoba na Mkoa wa Kagera kwa ujumla umeyumba kutokana na kukosekana kwa usafiri wa uhakika wa meli kati ya Bukoba na jiji la Mwanza,” anasema Julius Kaizer, mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi mjini Bukoba.

Anasema licha ya baadhi ya wafanyabiashara wadogo na kati kushindwa kuhimili gharama za usafirishaji kwa njia ya barabara, wafanyabiashara wakubwa pia wanalazimika kuongeza bei ya bidhaa jambo linaloongeza mzigo kwa wananchi ambao ndiyo walaji wa mwisho.

“Mzigo tuliokuwa tukiusafirisha kwa Sh2 milioni kwa njia ya maji hivi sasa unatugharimu zaidi ya Sh4 milioni kutoka Mwanza hadi Bukoba kwa barabara,” anasema.

Fursa iliyolala

Mtaalamu wa Uchumi na Uwekezaji, Bonventura Mehendeka anasema usafirishaji majini ndani ya Ziwa Victoria ni fursa ya uchumi iliyokufa ambayo wawekezaji wazawa na wageni wanaweza kuichangamkia.

Habari inayohusiana: Serikali inavyopoteza mabilioni kitengo cha mizigo bandarini

“Kufufuka kwa sekta hii siyo tu itaongeza pato la mwananchi mmoja mmoja, bali Serikali kupitia ushuru na kodi mbalimbali,” anasema Mahendeka.

Baada ya hali hiyo kuwapo kwa muda mrefu, Serikali ipo mbioni kuifufua MSCL ili kupunguza tatizo la usafiri katika ziwa hilo.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, meli zote 14 za abiria na mizigo zinazomilikiwa na MSCL zimeundwa kati ya mwaka 1938 hadi 1988 huku tatu pekee zikiwa zinafanya kazi moja kwa kila ziwa yaani Victoria, Tanganyika na Nyasa.

Mikakati

Serikali imetenga zaidi ya Sh50 bilioni katika bajeti iliyopo kwa ajili ya kuanza kwa mchakato wa kujenga meli mpya itakayosafirisha abiria na mizigo kati ya Mwanza na Bukoba.

Kaimu Meneja Mkuu wa MSCL, Eric Hamis anasema tayari mchakato wa kutafuta Mshauri Mwelekezi umeshaanza na kampuni 10 zimejitokeza kuomba kazi hiyo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa anasema ni azma ya Serikali kuboresha na kuimarisha huduma hiyo ili pamoja na kuwaondolea adha ya usafiri wananchi, pia kuongeza mapato kutokana na kodi na ushuru mbalimbali.

Katika mkakati huo, anasema Serikali itakarabati meli zake na kujenga zingine mpya na mkakati huo utahusisha meli zote zinazotoa huduma katika Ziwa Victoria, Nyasa na Tanganyika.

“Kwa upande wa Ziwa Viktoria tutaanza na ukarabati wa meli za Mv Viktoria na Mv Serengeti pamoja na ununuzi wa meli mpya ya kisasa kutekeleza ahadi ya Rais John Magufuli,” anasema Profesa Mbarawa.

Serikali pia imelazimika kubeba dhamana ya kuisaidia MSCL kwa kutoa Sh100 milioni kati ya Sh126 milioni zinazohitajika kila mwezi kulipa malimbikizo ya mishahara wanayoodai wafanyakazi kwa zaidi ya mwaka mmoja.

“Hadi Desemba mwaka jana, wafanyakazi hao walikuwa wanadai malimbikizo ya zaidi ya Sh1.2 bilioni,” anasema Hamis.

Nini kifanyike?

Pamoja na kukarabati, kununua meli mpya na kujenga Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa, Serikali italazimika kuzipanua bandari za Mwanza, Musoma na Bukoba kukidhi mahitaji ya sasa na baadaye.

Licha ya kutotumika kwa kiwango chake, bandari hizo zina kina kifupi kutokana na kujaa mchanga unaosababishwa na shughuli za kibinadamu katika kingo na bonde la Ziwa Victoria jambo linalokwamisha meli kubwa kutia nanga.

Mvuvi akitumia mtumbwi uliotengenezwa kwa matete katika Ziwa Victoria. Matumizi ya vyombo visivyokuwa salama kama hiki ni hatari kwa maisha ya wengi.
Mvuvi akitumia mtumbwi uliotengenezwa kwa matete katika Ziwa Victoria. Matumizi ya vyombo visivyokuwa salama kama hiki ni hatari kwa maisha ya wengi. Picha ya Maktaba

Moyo anasema kuna tishio la bandari bubu kadhaa ndani ya Ziwa Victoria ambazo zinaikosesha Serikali mapato. “Bandari bubu hizo pia zinaweza kutumika kusafirisha au kuingiza bidhaa haramu zikiwamo zana haramu za uvuvi, wahamiaji haramu na silaha,” anasema Moyo

Katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella aliziagiza mamlaka zinazohusika kudhibiti bandari bubu ili kuimarisha mapato ya Serikali, ulinzi na usalama.

“Hatuwezi kukubali kila mwenye fedha ajianzishie bandari yake na meli kuingia na kutoka bila ukaguzi wala mamlaka husika kujua kinachoendelea huko. Hapana! Hatuwezi kuweka rehani usalama wa nchi yetu kiasi hicho,” anasema Mongella.

Habari inayohusiana: Tutaendelea kukalia kimya uvuvi haramu hadi lini?

Pia, Serikali haina budi kuifanyia marekebisho Sheria ya Bandari ya mwaka 2004 inayoruhusu meli za MSCL kutolipia huduma za bandari kwani inapunguza mapato ya Mamlaka ya Bandari za Ziwa Victoria inayotegemea malipo ya kodi na ushuru kutoka kwenye meli zinazotia nanga bandarini.

Tanzania ya viwanda yenye uchumi wa kati kufikia mwaka 2025 inawezekana, iwapo uwekezaji utafanyika kwa kuboresha huduma ya usafirishaji kwa njia ya maji kupitia bandari za Ziwa Victoria, Nyasa, Tanganyika na Bahari ya Hindi.

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania