Mwigulu aibua mkakati kudhibiti mauaji Pwani

Nuzulack Dausen
May 10, 2017

Sharon Sauwa, Mwananchi, [email protected]

Dodoma. Mauaji mfululizo ya viongozi wa vijiji na askari wa Jeshi la Polisi yamechukua nafasi katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani, ambayo imebainisha ongezeko la uhalifu kwa asilimia saba.

Hotuba hiyo iliyosomwa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba imeweka mikakati minne ya kuboresha usalama nchini, ukiwamo wa kuunda mkoa wa kipolisi wa wilaya hizo tatu ambazo zimeshapoteza watu 29 kuanzia Mei mwaka jana.

Mikakati mingine ni Jeshi la Polisi kuajiri watumishi 4,235, kati yao polisi 2,573 Mamlaka ya Vitambulisho (Nida) kutoa vitambulisho milioni 22.7 na Polisi kununua magari 596.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba

Lakini suala la mauaji katika wilaya hizo tatu, ambalo limekuwa likiamsha mijadala mara kwa mara, lilichukua nafasi ya kipekee.

“Kutokana na ongezeko la matukio makubwa ya uhalifu katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji, katika mwaka 2017/18 Serikali inatarajia kuanzisha mkoa mpya wa kipolisi Rufiji ili kusogeza huduma ya polisi karibu zaidi na wananchi na kurejesha amani na utulivu katika maeneo hayo,” alisema.

Mwigulu alisema Wilaya ya Mafia itakuwa ndani ya mkoa huo mpya.

Viongozi 12 wa vijiji na vitongoji, askari kumi wakiwemo maofisa wawili, wafanyakazi wawili wa Idara ya Maliasili, mwanachama mmoja wa CCM  wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana, huku watu wengine watatu waliovalia nguo za kike wakiuawa na polisi katika wilaya hizo.

Video inayohusiana: MAUAJI YA POLISI: RAIS MAGUFULI ATOA NENO

Habari inayohusiana:  Askari aliyeuawa aacha mke anayetarajia kujifungua

Kuhusu ongezeko la uhalifu, Mwigulu alisema takwimu zinaonyesha kuwa makosa ya jinai yameongezeka kwa asilimia saba, ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2015/16.

“Ongezeko hilo linatokana na sababu mbalimbali, zikiwemo ukuaji wa miji, utandawazi na kuongezeka kwa mbinu za uhalifu,” alisema Mwigulu.

Alisema katika kipindi cha Julai mwaka 2016 hadi Machi 2017 kulikuwa na matukio 56,913 ambapo makosa 53, 850 yaliripotiwa kutoka Tanzania Bara na mengine 3063 yaliripotiwa kutoka Zanzibar.

Mwigulu alisema katika kipindi cha kati ya Julai mwaka 2016 hadi Machi 2017 jumla ya kilogramu 16 na gramu 223 za Cocaine pamoja na kilo 37 na gramu 118 za heroine zilikamatwa.

‘Watuhumiwa 1241 walikamatwa na kufikishwa mahakamani.Pia katika kipindi hicho kilo 36,337 na gramu 426.76 za bangi zilikamatwa na watuhumiwa 12,691 walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Alisema katika mwaka mpya wa fedha, wizara itaajiri watumishi 4,339 na kwamba mgawanyo ni 26 Makao Makuu ya Wizara, Jeshi la Polisi 2,573, Magereza 500, Zimamoto na Uokoaji 600, Idara ya Uhamiaji 600 na Nida 40.

Alisema hadi Desemba mwaka 2018, Nida itakuwa imetoa vitambulisho milioni 22.7, wakati Jeshi la Polisi linatarajia kununua magari 596 mwaka huu.

Mwigulu aliliomba Bunge limuidhinishie Sh 930.3 bilioni na kati ya hizo Sh 890.38 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ambapo Sh 367.7 bilioni ni kwa ajili ya matumizi mengineyo na Sh 522.6 ni mishahara.

Hatua za kinidhamu

Mwigulu alisema katika kipindi cha Julai mwaka 2016 hadi Machi 2017, Jeshi la Polisi lilipokea malalamiko 206 na kati ya hayo 203 yalitoka kwa wananchi na matatu ni ndani ya jeshi hilo.

“Takwimu zinaonyesha ongezeko la malalamiko 138 ikilinganishwa na kipindi kama hicho katika mwaka 2015/16 ambacho kilikua na jumla ya malalamiko 68,” alisema Mwigulu.

Waziri huyo alisema katika mwaka wa fedha 2016/17 askari 14 na maofisa wawili walifukuzwa kazi kwa makosa mbalimbali.

Aliyataja makosa hayo ni rushwa, wizi, kubaka, utoro kazini, kughushi nyaraka na kujipa likizo.

Kadhalika wakaguzi na maofisa 16 walipewa barua za onyo, kumi walishtakiwa na wanne walishushwa vyeo.

Wafungwa wenye sifa

Mwigulu alisema kwa sasa idara ya promosheni na huduma kwa jamii ina uwezo wa kuwatoa gerezani na kuwasimamia wafungwa 6,000 wenye sifa za kutumikia vifungo vya nje kwa mwaka na hivyo kuokoa  takribani Sh 3.28 bilioni kwa mwaka, fedha ambazo zingetumika kwa chakula na huduma nyingine wakiwa gerezani.

Alisema kwa kuzingatia hiyo, bajeti mpya imetenga Sh1.04 bilioni ili kuongeza idadi ya wafungwa wanaotumikia vifungo nje ya magereza hadi kufikia takribani 4,000.

Habari inayohusiana: JPM atoa msamaha kwa wafungwa 2,219

Awali, akichangia mjadala huo, mbunge wa Babati Mjini (Chadema), Pauline Gekul alisema bila wabunge kuacha unafiki na kuisimamia Serikali kuongeza fedha za maendeleo kwenye wizara hiyo, matatizo ya majeshi katika maeneo yao hayataisha.

Alisema kati ya bajeti ya Sh900 bilioni fedha za maendeleo ni Sh40 bilioni tu, ambazo hazitoshi.

Mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali alisema Rais Magufuli alitoa maelekezo kuwa wafungwa waliokuwa magerezani wasile bure bali wahenyeke.

Video inayohusiana:
Nchemba ataka utaratibu mpya kushikilia mahabusu

“Kuna wafungwa walioko magerezani kwa sababu ya kuonewa kama mimi, ukisema wahenyeke utakuwa huwatendei haki wafungwa ambao wako magerezani kwa sababu ya kuonewa,” alisema Lijualikali.

Waziri Mwigulu alifanya majumuisho jana jioni kwa kujibu hoja mbalimbali za wabunge.

Habari ya ziada na Reginald Miruko

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania