Hali sasa ngumu mikopo ya elimu ya juu

Nuzulack Dausen
May 15, 2017

 

  • Wanafunzi saba kwa kila 10 waliiomba mwaka huu wamekosa.
  • Tahliso yaomba Serikali iwahishe utoaji wa majina wanaostahili kupata mikopo ili kupunguza usumbufu.

Nuzulack Dausen na Kalunde Jamal, Mwananchi

[email protected]

Dar es Salaam/Dodoma. Wanafunzi wanaotegemea mkopo wa Serikali kugharamia elimu ya juu nchini watafute mbadala mapema kutokana na idadi ya wanaokosa huduma hizo za kifedha kupaa mwaka hadi mwaka jambo linalopunguza uwekezano wa kuupata.

Mikopo hiyo imekuwa ikiwasaidia wanafunzi wengi wasio na uwezo kuweza kumudu gharama za masomo yao ambayo katika baadhi ya vyuo vikuu nchini hutolewa kwa gharama kubwa hususan katika vyuo binafsi.

Wanafunzi wanaosoma shahada huenda wakaathirika zaidi na mwenendo huo baada ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kuanza kujikita kutoa mikopo kwa wanafunzi wa ngazi za stashahada ili kuongeza uwiano wa wataalamu wa kati watakaosaidia kutekeleza sera ya uchumi wa viwanda.

Mwananchi limebaini kuwa licha ya Serikali kuongeza wanufaikaji miaka minne iliyopita hadi wanafunzi 124,711 mwaka jana, idadi yao imeshindwa kupunguza uwiano wa wanaokosa huku hali ikiwa mbaya zaidi mwaka huu.

Idadi ya wanaohitaji mikopo kutoka HESLB inaongezeka kwa kasi kiasi cha kuzidi hata wale wanaodahiliwa kila mwaka na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), jambo linaloonyesha kuwa Watanzania wengi wanahaha kugharamia elimu hiyo ya juu.
Hata hivyo, Serikali imesema siyo lazima kila anayeomba mkopo apate kwa kuwa jukumu la kusomesha mtoto ni la mzazi au mlezi na bajeti ya elimu ina vipaumbele vingi zaidi ya kugharamia masomo ya elimu ya juu.

Uchambuzi wa takwimu za miaka mitano kutoka HESLB za hadi Machi 31 mwaka huu umeonyesha kuwa watu wawili kwa kila watatu walioomba mkopo katika mwaka wa masomo wa 2016/17 wamekosa huduma hiyo, kiwango ambacho ni kikubwa kuwahi kurekodiwa.

Hali hiyo imefanya baadhi ya wanafunzi waliokosa mkopo na vyanzo vingine vya kugharamia masomo yao kushindwa kujiunga na elimu hiyo ya juu huku wale waliobahatika kufanya usajili wakiahirisha masomo ili kusubiri bahati yao miaka ijayo.

Uchunguzi huo uliofanywa katika baadhi ya vyuo vikubwa nchini na kuhusisha uchambuzi wa kina wa takwimu kutoka HESLB na TCU, unaonyesha wale walioamua kuendelea na masomo bila ya kuwa na fedha za kutosha wamejikuta wakiishi kwa shida ikiwemo kuombaomba chakula kwa wanafunzi wenzao.

Namba hazidanganyi
Kuongezeka kwa idadi ya vyuo vikuu nchini na urahisi wa kupata mikopo miaka ya hivi karibuni kulichochea Watanzania wengi kujiendeleza na elimu ya juu kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Hata hivyo, kadri siku zinavyoenda uwingi wa wanafunzi hao wanaodahiliwa kila mwaka umefanya HESLB kuzidiwa kiasi cha kushindwa hata kuwahudumia wanafunzi wenye mahitaji ambao ni miongoni waombaji wenye kipaumbele.

Kwa takwimu zilizopo, tangu mwaka 2012/13 idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo ilikuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka na kufanya wanaokosa huduma hizo za kifedha wawe wastani wa theluthi ya walioomba au ya waliodahiliwa na TCU kabla ya kupanda tena kwa kasi mwaka 2014/15.

Mwaka 2014/15, idadi ya waliokosa ilikuwa ni nusu ya watu walioomba mkopo huo na hata wale waliodahiliwa.
Ujio wa serikali mpya ya Rais John Magufuli Novemba, 2015 ulisaidia kupunguza kiwango cha wanaokosa mikopo kutoka nusu ya waliomba hadi theluthi moja baada ya kuanza kutekeleza ahadi yake ya kuhakikisha wanafunzi wote wenye uhitaji wanapata huduma hiyo.

Uamuzi huo wa Serikali ambao Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-razaq Badru alisema ulilenga “kuongeza walimu ili kuendana na mahitaji ya sera ya elimu bure” ulifanya idadi ya wanafunzi wapya waliopata mkopo kwa mwaka wa masomo 2015/16 kuongezeka hadi 54,072, kiwango cha juu kuwahi kufikiwa.

Hii ilifanya idadi ya waliokosa mikopo dhidi ya walioomba kuwa asilimia 32, kiwango cha chini zaidi ndani ya miaka mitano.

Hata hivyo, hali inaonekana kuwa mbaya zaidi katika mwaka wa masomo unaoendelea wa 2016/17 baada ya idadi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopatiwa mikopo kushuka kwa takriban mara mbili kutoka 54,072 mwaka 2015/16 hadi kufikia wanafunzi 28,354 Machi 31 mwaka huu. Imebaki miezi mitatu kumaliza mwaka wa masomo.

HESLB inasema kuwa watu 83,255 waliomba mikopo hiyo ikijumuisha wenye sifa na wasio na sifa ikiwa ni ongezeko la takriban mara mbili ikilinganishwa na waliomba mwaka 2012/13. Hii ina maana kuwa kwa kila wanafunzi 10 waliomba mikopo HESLB katika mwaka wa masomo 2016/17, saba wamekosa.

Hata iwapo uchambuzi utafanywa kwa kutumia idadi ya waliodailiwa na TCU katika vyuo vikuu mbalimbali mwaka huu kama Badru anavyoshauri ambao ni 69,539 bado wanafunzi 41,185 sawa na watu sita kwa kila 10 waliodahiliwa wamekosa mikopo.

Katika miaka yote mitano idadi ya waliodahiliwa mwaka wa kwanza ni ndogo kuliko walioomba kupatiwa mikopo hiyo.

Mwananchi limebaini kuwa mabadiliko ya kimkakati na mabadiliko ya vipaumbele vya bajeti yaliyofanywa na Serikali na uwepo wa vyanzo vichache mbadala vya kugharamia elimu ya juu vinazidi kuwaweka kando baadhi ya Watanzania kupata elimu hiyo.

Hadi sasa bodi ya mikopo ndiyo chanzo kikuu cha fedha za kugharamia masomo ya elimu ya juu nchini ukiachana wafadhili wachache au mifuko ya pensheni inayotoa huduma kwa wanachama wake.

Miongoni mwa walioathirika zaidi ni wale waliosoma shule binafsi kwa ama kusomeshwa na wazazi au walezi wao au mashirika katika ngazi za chini lakini kutokana na hali zao kiuchumi kubadilika baadaye wamejikuta wakitemwa na mfumo wa HESLB.

“Nilidhani ningepata mkopo kwa kuwa niliomba kama wengine lakini majina ya waliopata mikopo yalipotangazwa sikuwepo na awali sikujulishwa kuwa kulikuwa na makosa katika uombaji. Hivyo ilibidi niondoke chuo kwa kuwa sikuwa nimedahiliwa kutokana na kukosa fedha za usajili,” alisema Zakia Hussein aliyeacha masomo Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) mwanzoni mwa mwaka huu.

Zakia anayekaa kwa dadake Area D mjini Dodoma, alisema kwa sasa anabangaiza maisha angalau apate nauli ya kurudi kwao Bukoba mkoani Kagera kwa kuwa hata akiendelea kubaki mkoani hapo hana uhakika wa kurudi chuo.
“Ndoto zangu za kwenda chuo zimeshazimika,” alisema Zakia aliyetakiwa kusomea shahada ya elimu huku akitoa machozi na kuongeza kuwa “kosa langu ni kusaidiwa kusoma shule binafsi kidato cha tano na sita na ndugu baada ya wazazi kukosa uwezo”.
Ukiachana na wanaoacha vyuo kama Zakia, wapo baadhi waliobahatika kusajiliwa na kuamua kuahirisha masomo yao ili wasubiri iwapo HESLB itawafikiria au watafute vyanzo vingine vya kugharamia elimu yao.

Katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu John cha Dodoma, wanafunzi 72 kati ya 1,712 waliodahiliwa mwaka huu wameshaahirisha masomo kutokana na kushindwa kumudu gharama au kucheleweshewa mikopo huku zaidi ya theluthi mbili wakiwa ni wa Shahada ya Sayansi ya Elimu.

Wanafunzi hao walioahirisha masomo, kwa mujibu wa takwimu za chuo hicho, ni sawa na jumla ya wanafunzi wanaotakiwa kudahiliwa katika shule za Famasia na ile ya theolojia na mafunzo ya kidini.

Hata wakati wengine wakiahirisha kwa kukosa kabisa fedha, wapo wengine waliopambana kwa kukata rufaa lakini walipata mikopo hiyo wakiwa tayari wameshakosa baadhi ya mitihani ikiwemo ya kufungua muhula kama ilivyomtokea Samuel Kitinya (21).

“Nilisoma shule zote za kata na wazazi ni maskini wapo Wotta wilayani Mpwapwa lakini nilishangaa nilivyokosa mkopo na nilipokata rufaa waliniambia nipeleke uthibitisho kuwa wazazi wangu hawana uwezo.

“Lakini mkopo ulikuja Februari mwaka huu wakati tayari nimeshakosa majaribio mengi na mtihani wa kumaliza muhula uliofanywa Januari hivyo niliomba niahirishe tu masomo hadi mwakani,” alisema Kitinya aliyekuwa anasoma Shahada ya Menejimenti ya Rasilimali watu katika Taasisi ya Uhasibu (TIA) jijini Dar es Salaam.

Habari inayohusiana

Walioamua kuendelea na elimu hiyo bila mikopo au chanzo kingine cha kifedha wamejikuta wakiishi kwa shida huku baadhi ya wasichana wakituhumiwa kujiuza kumudu gharama za maisha.

Aliabadi Salim anayesoma shahada ya ualimu UDOM alisema huishi kwa kuombaomba ilimradi aendelee na masomo na serikali ya wanafunzi wa chuo hicho imewatafutia sehemu ya kula mtaani kuwakinga na njaa.

“Hatuna namna ya kuwasaidia wasio na fedha ila tatizo kubwa tumeona ni chakula hivyo wapo wanafunzi watano ambao tuliwaombea chakula kwa mama lishe wa huko Ujasi (kijiji jirani na Udom) ambao huwasaidia kila siku,” alisema Mujibu Abeid, Mwenyekiti wa mawaziri wa mikopo wa Udom.

Badru, bosi wa HESLB, alieleza kuwa idadi ya wanafunzi waliopata mikopo mwaka huu imeshuka kwa sababu ya mabadiliko ya mgawanyo wa rasilimali fedha yanayofanywa kila mwaka kwa kuzingatia vipaumbele vya bajeti ya wizara ya elimu.

Hata hivyo, alipoulizwa kama HESLB inakabiliwa na ukata wa fedha ndiyo maana wanafunzi wengi wamekosa mikopo, alisema hawana tatizo la fedha kwa kuwa bajeti yao hutolewa yote na Serikali kama ilivyoombwa.

Mbali na mabadiliko ya vipaumbele, alisema wanaopata mikopo wamepungua kwa kuwa ni maandalizi ya kuimarisha mfumo wa msonge ambao unahitaji wataalamu wengi wa kada ya kati na chini wenye elimu ya stashahada na cheti.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu )(HESLB), Abdul-razaq Badru. Picha ya Maktaba.

“Tumesharekebisha sheria ili kuwapa mikopo wanafunzi wenye stashahada kwa kuwa awali tuliwapa watu wa elimu pekee yao.

“Sasa tutatoa kwa kada zote za kati ambazo zitakuwa zinahitajika kwa wakati husika kujenga uchumi wa viwanda kama uhandisi wa kilimo, umwagiliaji na uchukuzi…hii itasaidia kuleta uwiano wa ujuzi kati ya wenye shahada ambao ni wengi kwa sasa na wale wa ngazi za chini,” alisema Badru.

Kuhusu baadhi ya wanafunzi waliosoma shule binafsi lakini sasa wana mahitaji, alisema tatizo kubwa lililojitokeza ni wengi kushindwa kuthibitisha uhitaji wao lakini wapo takriban 5,000 waliosomeshwa na mashirika au taasisi wamepatiwa mikopo baada ya kuthibitisha.

Alisema wanafunzi wenye mahitaji ambao wamekosa mikopo imetokana na wao kushindwa kuambatanisha nyaraka muhimu zinazothibitisha uhitaji wao na wapo baadhi waliotoswa baada ya kufoji vyeti vya vifo ili kupata fedha hizo.

Wachambuzi wa elimu ya juu wameliambia gazeti hili kuwa idadi ya wanaoomba mikopo inaongezeka kwa sababu ya wingi wa vyuo vikuu na baadhi ya watoto wa wenye uwezo kuiomba jambo linalofanya wenye uhitaji kukosa.

Mhadhili wa Chuo cha Kilimo cha Sokoine, Dk Josiah Katani alisema kosa kubwa lilifanywa na Serikali baada ya kuacha vyuo vya ufundi mchundo kufa huku ikiruhusu kushamiri vyuo vikuu vikiwemo vyenye sifa hafifu wakati ikijua haina uwezo wa kugharamia idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiunga na taasisi hizo.

“Kosa jingine ni la kuruhusu watoto wa viongozi serikalini na wafanyabiashara kupatiwa mkopo wakati wana uwezo. Hii ilichochea watu wengi kuomba mkopo kana kwamba ni bure wakati wazazi wao wana uwezo…hii iwe fundisho na haifai kurudi huko,” alisema.

Dk Katani alisema wadau wanapaswa kujadili kwa kina ili kupata njia rafiki ya kugawana gharama za elimu ya juu kati ya Serikali, wazazi na walezi itakayofanya watoto wa maskini waende vyuoni na ikiwezekana Serikali itoe mikopo kwa wanafunzi wote ila iwabane kwenye urejeshaji.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya alisema “siyo kweli kuwa idadi ya wanafunzi imepungua badala yake tangu kuanza kwa uongozi wa awamu ya tano imeongezeka na kufikia wanafunzi 123,000.”
Hata hivyo, Mwananchi linajua kupitia takwimu za HESLB kuwa hadi Machi 31 mwaka huu, idadi ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea ilishuka hadi 114,621 kutoka wanafunzi 124, 711 mwaka jana.

Manyanya alisema sio wanafunzi wote wanaoomba wanahitaji mikopo, hivyo wanawalenga zaidi wale wenye uhitaji maalumu ndiyo maana waliweka vigezo.

“Bajeti ya Wizara ya Elimu siyo kwamba inatolewa kwa ajili ya mikopo pekee, inatumika pia kwa ajili ya kuboresha miundombinu, walimu, vifaa vya kusomea, kufundishia.

“Wazazi wasikwepe jukumu hili kwa kuwa haitakuwa na maana kama tutawapa mikopo wanafunzi wote wa elimu ya juu halafu hakuna walimu na mabweni,”alisema Manyanya.

Kuhusu mbadala wa kugharamia masomo ya elimu ya juu, Manyanya alisema kuwa Serikali imefungua milango ya mabenki na sekta nyingine za fedha kukopesha wanafunzi, hivyo wenye hizo taasisi kama wataona umuhimu wa kufanya hivyo ni jukumu lao.
Mwisho.

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania