Nuzulack Dausen July 21, 2017
- Mikoa hiyo ina kuku wengi wa kienyeji kiasi cha kuwa kitovu cha wachuuzi wa bidhaa hiyo.
[email protected]
Dar es Salaam. Kwa wakazi wengi wa Dar es Salaam wakisikia kuku wa kienyeji wazo la kwanza mara nyingi ni huwa ni wale waliotoka Singida au Dodoma. Sehemu kubwa ya wakazi wa jiji hili wanaamini mikoa hiyo ndiyo inayozalisha kuku hao kwa wingi.
Hata hivyo, walichokuwa wanafikiri sicho. Mikoa hiyo haipo hata kwenye orodha ya mikoa 10 inayozalisha zaidi kuku wa kienyeji. Lakini Dodoma ina sifa kinyume na inaongoza kuzalisha kuku wa kisasa.
Takwimu za utafiti wa kilimo kwa mwaka 2014-15 ziliotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) Februari mwaka huu zinaonyesha kuwa mkoa wa Mbeya ndiyo unaongeza kwa kuwa na kuku wengi wa kienyeji ambao ni zaidi ya milioni 2.5.
Idadi ya kuku wa kienyeji waliopo katika mkoa huo wa Nyanda za Juu Kusini ni takriban mara mbili ya wale waliopo mkoani Dodoma ambao ni milioni 1.4.
Mbeya inafuatiwa kwa karibu na Tabora yenye kuku wa aina hiyo zaidi ya milioni 2.49.
Uwepo wa idadi kubwa ya mifugo hiyo ni fursa ya kibiashara kwa wafugaji wa mikoa hiyo iwapo watatumia vizuri rasilimali hizo kujitangaza ili kujiingizia kipato.
Pia, kufahamika kwa mikoa yenye kuku wengi wa kienyeji ni fursa ya soko kwa wafanyabiashara wa mifugo hiyo inayopendwa zaidi na watu wasiopenda kutumia wale wa kisasa.
Kwa mujibu wa utafiti wa masuala ya chakula na magonjwa uliofanyika Novemba, 2010 nchini Marekani, kuku wa kienyeji wana faida lukuki ikiwemo ladha nzuri tofauti na wale wa kisasa.
Ripoti ya utafiti huo unaoitwa kwa kiingereza ‘Foodborne Pathogens and Disease study’ inaeleza kuwa nyama ya kuku hao ina kiwango kidogo cha sumu kwa kuwa hazitumii dawa nyingi za kuwakuza na pia haina mafuta mengi ikilinganishwa na wale wa kisasa.
Kuku wa kienyeji ni miongoni mwa vitoweo ghali jijini Dar es Salaam akiuzwa kuanzia Sh18,000 kwa kuku wadogo huku wakubwa wakiuzwa hadi kufikia Sh40,000.
Pamoja na Dar es Salaam kuwa na bei ya juu ya kuku, Dodoma kuku wa kienyeji kati ya Sh9, 000 hadi Sh12, 000 bei inayoelekeana na ile ya mkoani Mbeya.
Kuku wa kisasa wa nyama huuzwa wa wastani wa Sh5,000 hadi Sh7,000 inategemea na ukubwa na uzito.
Lakini hali ni tofauti kwa kuku wa kisasa. Utafiti uliofanywa na Kevin Queenan na wenzie watano hapa nchini na Zambia na kuchapishwa mwaka jana, unaonyesha kuwa bei ya kuku wa kisasa inafanana kabisa kati ya Dar es Salaam na Dodoma kwa sababu gharama za uendeshaji zinafanana.
Utafiti huo uliochapishwa kwenye jarida la kilimo liitwalo Utafiti wa Mifugo kwa Maendeleo Vijijini toleo la 28, (Livestock Research for Rural Development 28 (10) 2016), unaeleza kuwa sehemu kubwa ya kuku hao wa kienyeji wanafugwa kwa ajili ya kitoweo nyumbani na wachache hufugwa kwa ajili ya biashara.
Hata wakati baadhi ya mikoa ya Tanzania kuongoza kwa kuku hao wa kienyeji bado sehemu kubwa ya wafugaji wanafuga kienyeji zaidi jambo linalofanya wapate mavuno kidogo na yasiyo na afya imara.
Nuzulack Dausen
Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.