Nuzulack Dausen September 3, 2017
*Madaktari washauri Watanzania kuendelea kujikinga na ugonjwa huo hatari duniani.
Dar es Salaam. Licha ya kuwepo kampeni lukuki za kukabiliana na Ukimwi, wilaya za Mbarali na Kyela zinaongoza kwa kuwa na viwango vikubwa vya wanawake wajawazito wenye virusi vya ugonjwa huo mkoani Mbeya.
Takwimu za program ya Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR) za kati ya Oktoba mosi, 2014 hadi Septemba 30, 2015 zinaonyesha kuwa wilaya ya Mbarali iliongoza kuwa na idadi kubwa ya kina mama wajawazito waliobainika na virusi vya Ukimwi baada ya kuwa na asilimia 12 ikifuatiwa na Kyela iliyokuwa na asilimia 11.
Hii ina maana kuwa kwa mujibu wa PEPFAR, Mbarali ilikuwa na wajawazito 12 kwa kila 100 waliobainika kuwa na VVU wakati Kyela ilikuwa na wajawazito 11 kati ya 100, takriban mara tatu ya wastani wa mkoa wa Mbeya.
Takwimu hizo zilizochapishwa katika tovuti ya takwimu huru ya Hurumap (tanzania.hurumamap.org) zinaonyesha kuwa ni wajawazito wanne tu kati ya 100 (asilimia nne) ya waliopima walibainika kuwa na VVU.
Viwango hivyo pia ni mara mbili ya kile cha wilaya ya Mbeya mjini ambacho ni watu sita tu kati ya 100 ndiyo walibainika kuwa na VVU.
Hata hivyo, hadi mwaka 2014 takwimu kutoka kituo huru cha takwimu cha Serikali (opendata) zinaonyesha kuwa Kyela ilikuwa na vituo vinne zaidi vinavyotoa huduma za kupima na kutoa matibabu ya Ukimwi (VTC) kuliko Mbeya Mjini iliyokuwa na vituo 27.
Serikali inasema kuwa kwa sasa hawawezi kutumia takwimu hizo kufafanua au kufanyia uamuzi kwa kuwa tayari utafiti wa kina kubaini hali ya VVU umeshafanywa nchi nzima na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Seif Mhina ameiambia MwananchiData kuwa Serikali inaendelea na mikakati ya kukabiliana na Ukimwi mkoani humo ikiwamo kushawishi watu wapime damu kwa hiari kutambua hali zao, watumie kinga wakati wa tendo la ndoa na wale waliobainika kuwa na VVU watumie dawa za kufubaza makali ya virusi.
“Tusubiri takwimu za NBS waliofanya utafiti tangu Juni. Matokeo yao yatatoa picha kamili kwa sababu wamempima mtu mara moja tu tofauti na hayo ya kwenye vituo ambayo mtu anaweza kupima mara tano katika vituo tofauti na taarifa zake zikarekodiwa kama mgonjwa mpya,” anasema Dk Mhina.
“Kuna mtu anatoka Chunya alishawahi kupima na kubainika na VVU halafu akifika Kyela anawaambia sijawahi kupima na kupimwa tena nakuambiwa tena anaumwa jambo linalofanywa tushindwe kupata picha kamili,” anaongeza.
Dk Mhina alisema huenda hadi Oktoba majibu ya utafiti wa VVU wa NBS yatakuwa tayari huku akiwasihi Watanzania kujihadhari na ugonjwa huo unaoendelea kumaliza nguvukazi nchini.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee hadi mwaka jana Mbeya ilikuwa ni miongoni mwa mikoa mitatu inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wenye miaka kati ya 15 hadi 49 wanaoishi na VVU ikiwa na asilimia tisa nyuma ya Iringa (asilimia 9.1) na Njombe asilimia 14.8.
Shirika la Kimataifa la kupambana na Ukimwi (UNAIDS) linabainisha katika ripoti yake ya mwaka 2017 iliyotolewa miezi miwili iliyopita kuwa wastani wa idadi ya wajawazito wenye VVU wanaopata dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo (ARV) nchini imeongezeka kutoka asilimia 75 mwaka 2010 hadi asilimia 84 mwaka jana.
Licha ya ripoti hiyo ya UNAIDS kubainisha kuwa vifo vitokanavyo na Ukimwi vimepungua kutoka 71,000 mwaka 2010 hadi 33,000 mwaka jana, bado idadi ya wanaoishi na virusi vya Ukimwi inaongezeka.
Wataalamu wa masuala ya afya wanaeleza kuwa kinamama wajawazito wenye VVU wanaweza kuwakinga watoto wao wasipate maambukizi iwapo watafuata taratibu za kimatibabu na kinga za kuwalinda viumbe wao.
Mganga wa Hospitali Teule ya Manispaa ya Kigoma Ujiji Baptis, Kilawa Shindo anasema mara baada ya mama mjazito kubainika ana VVU huanzishiwa dawa na baada ya kujifungua mtoto naye hupatiwa dawa kumkinga na virusi hivyo.
“Mtoto anatakiwa anyonyeshwe kwa miezi sita na akianza kutoa meno inabidi asimamishwe ili asije mng’ata mama kwa bahati mbaya na kupata VVU. Baada ya kuachishwa kunyonya anatakiwa kupatiwa maziwa ya kopo Lactogene 1 na 2,” anasema.
Dk Shindo anasema kuwa kwa sasa muamko wa kujizuia na maambuki ya VVU ni mkubwa japo baadhi wanajisahau na kujikuta wanatumbukia kwenye vishawishi jambo ambalo linatakiwa kuzuiwa hususan kwa wale waotumia vilevi.
Kuhusu kupungua kwa idadi ya vifo wakati idadi ya wagonjwa inaongezeka, Dk Shindo anasema takwimu za UNAIDS zinaonyesha watu wanaoishi na VVU ni wengi kwa sababu kwa sasa kuna mwamko wa kupima kuliko miaka ya nyuma.
“Watu wengi wanavyojitokeza kupima ndivyo tunavyozidi kufahamu hali yao. Lakini vifo vinapungua kwa sababu wagonjwa wengi wanawahi kupatiwa matibabu kuliko kipindi cha nyuma ambacho watu walikuwa wanakuja wakiwa hati hali mbaya ya ugonjwa,” anasema.
Nuzulack Dausen
Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.