Nuzulack Dausen September 20, 2017
*Takwimu zaonyesha wanafunzi takriban tisa kwa kila 10 waliokariri darasa mwaka 2016 wanatoka darasa la kwanza hadi la tatu.
[email protected]
Dar es Salaam. Licha ya idadi ya wanafunzi wanaokariri madarasa katika elimu ya msingi kushuka mwaka jana bado kiwango cha wanafunzi wanaorudia katika ngazi za chini ni kikubwa kuliko wale wa ngazi za juu.
Uchambuzi wa takwimu za msingi za elimu mwaka 2016 (Best 2012-2016, Kiingereza PDF) umebainisha kuwa idadi ya wanafunzi waliokariri madarasa mwaka huo walikuwa ni 389,840 ikilinganishwa na wanafunzi 404,896 mwaka 2015.
Kiwango hicho cha wanaorudia madarasa kimepungua licha ya idadi ya wanafunzi wanaojiunga elimu ya msingi kuongezeka kila mwaka.
Hata hivyo, idadi ya waliokariri wakiwa darasa la kwanza hadi la tatu asilimia 86 sawa na wanafunzi tisa kwa 10 ya wanafunzi wote waliorudia madarasa mwaka huo.
Ripoti ya takwimu hizo zilizotolewa na Ofisi ya Rais-Tamisemi inaeleza kuwa kiwango cha waliokariri darasa mwaka jana kilikuwa kikubwa katika madarasa ya chini kwa sababu wanafunzi wengi walikuwa hawamudu stadi za kusoma, kuhesabu na kuandika (KKK).
“Hata hivyo, idadi ya waliokariri darasa la sita ni kubwa karibu miaka yote kuanzia mwaka 2011 hadi mwaka 2016 kasoro mwaka 2013; ni kwa sababu baadhi ya wanafunzi hukosa utayari wa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE),” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo iliyochapishwa Oktoba mwaka jana.
Kitendo cha wanafunzi wengi wa ngazi za chini katika elimu ya msingi kukaririshwa madarasa kutokana na uelewa mdogo si jambo la ajabu.
Soma zaidi: Ndalichako awatega walimu
Matokeo ya tathmini ya utafiti wa Uwezo wa mwaka 2017 uliofanywa na asasi ya kiraia ya Twaweza yanabainisha uwepo wa tatizo kubwa la KKK miongoni mwa wanafunzi huku sehemu kubwa ya watoto wenye miaka kati ya tisa na 13 walishindwa kufanya majaribio ya darasa la pili huku utofauti ukiwa mkubwa kati ya wilaya na wilaya.
“Mwanafunzi mmoja kati ya 10 wa darasa la tatu alikuwa ana uwezo wa kusoma hadithi ya darasa la tatu huku watano kwa kilo 10 wa darasa la saba waliweza kufanya hivyo,” inasomeka sehemu ya Ripoti ya tathmini ya kujifunza ya mwaka 2017 iliyotolewa na Twaweza Aprili mwaka huu.
Hata hivyo, takwimu za utafiti mwingine wa Uwezo wa mwaka 2015 uliochapishwa kwenye tovuti ya Hurumap Tanzania zinaonyesha tatizo hili ni la muda mrefu kwa kuwa watoto takriban wanane kati ya 10 wenye miaka sita hadi 16 walifeli jaribio la Kiingereza wakati watano kati ya 10 walishindwa jaribio la Kiswahili.
Meneja wa Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa asasi ya kiraia ya Hakielimu, Godfrey Boniventure anasema sababu kubwa ya wanafunzi wa shule za msingi kushindwa KKK inatokana na kukosa misingi imara tangu wanapoanza elimu ya awali.
Anasema baadhi ya walimu hawana ujuzi mahususi unaotakiwa kuwafundisha watoto wadogo wakaelewa vyema na mazingira ya kujifunzia nayo siyo mazuri.
Tazama zaidi: Mambo yanayosababisha kushuka kwa elimu Handeni, Tanga
Kwa kawaida, anasema mtoto anavyoingia darasa la kwanza anatakiwa ameshapitia elimu ya awali na kupewa msingi mzuri wa KKK.
“Watoto wanatakiwa wakae katika madarasa mazuri, ikifika saa 4 asubuhi wapewe uji na kufundishwa na walimu wazuri. Sasa unakuta watoto hawapewi chakula, wale wadogo njaa ikianza kuwauma wanalia lakini wale wakubwa kidogo wanajua namna ya kujiuzuia ila hawaelewi wakifundishwa darasani,” anasema.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, Boniventure anashauri kuboreshwa kwa mazingira ya kujifunzia ikiwemo kuwa na uwiano mzuri wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 25 kwa elimu ya awali na mwalimu mmoja kwa wanafunzi 40 kwa shule za msingi na sekondari.
“Jambo jingine muhimu ni kuhakikisha watoto wanapata chakula wakiwa shule hii itaongeza uelewa na kupunguza idadi ya wanaofeli na kukariri madarasa,” anaeleza.
Serikali inasema kuwa inaendelea na juhudi kuhakikisha watoto wanaojiunga na elimu ya msingi pamoja na wale walio nje ya mfumo rasmi wanamudu vema stadi ya kusoma, kuandika na kuhesabu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako aliliambia Bunge wakati akisoma bajeti ya mwaka 2017/18 kuwa wizara hiyo inatekeleza programu ya kukuza KKK yenye lengo la kuhakikisha watoto wanaojiunga darasa I-IV na wale walio nje ya mfumo usio rasmi wanajua kuandika, kusoma na kuhesabu.
Nuzulack Dausen
Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.