Ukosefu wa huduma bora za afya unavyokwamisha maendeleo Nkasi

Maria Mtili
September 25, 2017

Pamoja na jitihada mbalimbali za Serikali kukabiliana na uhaba wa huduma za afya nchini, bado maeneo mengine yanakabiliwa na tatizo hilo kwa zaidi ya asilimia 50.

Elias Msuya, Mwananchi

Licha ya mwongozo wa utumishi wa mwaka 2014 kuagiza kuwa kila zahanati iwe na wahudumu 20, hali ni tofauti wilayani Nkasi, mkoani Rukwa yenye uhaba wa wahudumu mara nne ya wanaohitajika na kusababisha kuzorota kwa utoaji wa huduma za afya.

Taarifa zilizotolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Julius Kaondo zinaonyesha kuwa ina wahudumu 353 pekee kati ya mahitaji ya wahudumu 1,345.

Mbali na upungufu huo, wilaya hiyo ina upungufu wa zahanati kwa zaidi ya asilimia 50, huku hali mbaya zaidi ikiwa katika visiwa vya Kijiji cha Mandakerenge vilivyomo katika Ziwa Tanganyika.

Kijiji cha Mandakerenge chenye vitongoji 13 na watu zaidi 4,600 kina zahanati moja tu ambayo baadhi ya wananchi wanaoishi katika vitongoji vilivyopo visiwani hulazimika kutembea takriban kilomita saba kupata huduma za afya wengi wao wakitumia mitumbwi.

Muuguzi katika zahanati ya Kisiwa cha Mandakerenge wilayani Nkasi, Erica Mkama akimuhudumia mgonjwa. Picha na Elias Msuya
Muuguzi katika zahanati ya Kisiwa cha Mandakerenge wilayani Nkasi, Erica Mkama akimuhudumia mgonjwa. Picha na Elias Msuya

Vitongoji vyote vya kijiji hicho vikiwemo Ntanga, Mageuzi, Azimio, Uhuru, Umoja, Jembe ni mali, Mvuna (kisiwa), Mwendapole, Mbereketwa, Juhudi, Majaona Kamsokaya na Mwila havifikiki kwa magari wala pikipiki zaidi ya kutembea kwa miguu na mitumbwi kwa walio visiwani.

Wananchi wamelieleza gazeti hili kuwa wamekuwa wakiahidiwa na viongozi wa siasa wakati wa kampeni za uchaguzi, lakini wakichaguliwa hawatekelezi.

Juma Kakozi mkazi wa Kisiwa cha Mvuna anasema watoto wake wanne wamefariki dunia baada ya kukosa usafiri wa kuwawahisha hospitali kupata matibabu.

“Mimi nilishapoteza watoto wa kiume wanne; wa kwanza nilisafiri naye kwenda kisiwani Mandakerenge, wakasema hakuna vifaa vya kumtibu na alikuwa na hali mbaya, akafariki.

“Wa pili alikuwa na miezi miwili na wa tatu alikuwa na mwezi mmoja. Kila tukifika Kisiwa cha Mandakerenge tunaambiwa hakuna vifaa na usafiri wa kwenda Kirando hatuna uwezo wa kulipia, ndio maana walifariki,” anasema Kakozi baba wa watoto wanane.

Mke wa Kakozi, Regina anasema walipoteza watoto kwa sababu ya kukosa fedha za kununua petroli kwa ajili ya mtumbwi wa kuwapeleka watoto wao kupata matibabu Kijiji cha Kirando kilichopo umbali wa kilomita nane.

“Kila unapofika uchaguzi, wanasiasa wanakuja hapa kutuomba kura na kuahidi kujenga zahanati, lakini uchaguzi ukiisha wanatutelekeza na kututaka tuhame huku,” anasema.

Baadhi ya wakazi wameona kuhamisha sehemu ya familia zao kwenda kwenye maeneo yenye huduma bora za kijamii ndiyo suluhu.

Elizabeth Yamsebo na mumewe, Ephraim Pondamali wameamua kuwahamisha watoto wao tisa kwenda Kijiji cha Kalungu kwa ajili ya kupata huduma za afya na elimu na huwarudisha watoto hao wakati wa likizo tu au wakipata dharura.

“Hapa tunaishi kwa sababu ya shughuli za uvuvi. Tatizo kubwa hatuna huduma za afya; tukiwa na mgonjwa inabidi tuchangishane fedha kati ya Sh30, 000 hadi Sh80,000 kumpeleka hospitali,” anasema Yamsebo.

Mwenyekiti wa CCM kisiwani humo, King Mwalimwa anasema chama hicho kimeshindwa kutekeleza ilani yake katika visiwa hivyo kwa kushindwa kutoa huduma za jamii.

“Mwaka 2016 alikuja hapa Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Rukwa, Zenosi Mwanakulya tukamweleza changamoto za kupeleka wagonjwa na wajawazito hospitali katika kisiwa kingine inavyohatarisha maisha, lakini hawajatekeleza chochote mpaka sasa,” anasema Mwalilwa.

Mwenyekiti wa kisiwa hicho, Elias Mlea (Chadema) anasema kutokuwepo kwa huduma za jamii hususan afya kunatokana na sababu za kisiasa ambapo alisema baadhi ya viongozi wa CCM wamekuwa wakiwataka wahame kisiwani humo wakati kinatambulika kiutawala.

“Hiki kisiwa kipo kisheria na ndiyo maana tunafanya chaguzi zinazotambulika kisheria. Serikali ilijenga jengo la zahanati ya muda, lakini hutumika wakati wa dharura tu. Kwa hiyo wananchi hulazimika kuchangishana fedha kwa ajili ya kupeleka wagonjwa wao Mandakerenge,” anasema Mlea.

Hali hiyo inafanana katika visiwa vingine vya eneo hilo kikiwemo cha Mandauhuru.

Mandauhuru nako ni maumivu

Kisiwa cha Mandauhuru hali pia ni mbaya kwani licha ya kutambuliwa kama kijiji kwa mujibu wa Sheria Na. 7 ya Serikali za Mitaa (Serikali za vijiji) ya mwaka 1982, hakina huduma yoyote ya jamii zikiwamo huduma za afya.

Kutokana na hali hiyo wananchi wa kisiwa hicho chenye wakazi zaidi ya 400, wanalazimika kutumia mitumbwi hafifu kuvuka Ziwa Tanganyika kwenda Kijiji cha Mkinga ili kupata huduma za afya.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Venance Kapunda anasema wamekuwa wakivuka Ziwa Tanganyika ili kupata huduma za jamii ikiwemo afya katika Kijiji cha Mkinga kilichopo umbali wa kilometa mbili kwa kutumia mitumbwi ya kienyeji.

“Kutokuwa na zahanati ni kero kubwa kwa sababu tunalazimika kuvuka maji kwenda Mkinga. Kwa sasa hakuna mpango wa kujenga zahanati,” anasema.

Kata ya Mkinga yenye vijiji vitano vya Kalungu, Mkinga, Mandauhuru, Majengomapya na Ntanganyika ina zahanati moja iliyoko katika Kijiji cha Mkinga na kuhudumia wakazi zaidi ya 11,000.

Mganga mfawidhi wa zahanati hiyo, Anthony Lyachemi anasema uhaba wa wahudumu unaleta changamoto ya kuhudumia wakazi hao.

“Tuko wahudumu wanne tu na mmoja wetu yuko masomoni, ni mzigo mzito kuwahudumia watu wote hao. Hata hivyo tunapambana hivyo hivyo,” anasema Lyachemi.

Upatikanaji wa dawa

Kuhusu upatikanaji wa dawa, Lyachemi anasema awali lilikuwa tatizo kubwa, lakini kwa mwaka 2017/18 zimeletwa za kutosha.

Uhaba wa wahudumu unaikabili zahanati ya Kisiwa cha Mandakerenge ambayo Mganga mfawidhi wa zahanati hiyo, Erica Mkama anasema kwa sasa watu watatu wanalazimika kufanya kazi za watu 20 kutokana na upungufu wa watumishi.

“Pamoja na uchache wetu tunalazimika kuwahudumia wananchi wengi siyo hapa kijijini tu, bali tunalazimika kusafiri kwa miguu au kwa mitumbwi kwenda kwenye vitongoji vya mbali kutoa huduma”, anasema Erica.

Erica anasema hali huwa mbaya zaidi wakati wa msimu wa uvuvi ambapo kunakuwa na mlipuko ya ugonjwa wa kipindupindu kwa sababu ya msongamano wa watu na miundombinu iliyopo haiwezei kubeba idadi kubwa ya wagonjwa.

Anasema licha ya utaratibu wa kazi kutoruhusu wahudumu wenye watoto wadogo kutoa huduma kwa wagonjwa wenye magonjwa ya kuambukiza kama kipindupindu, wao hulazimika kutoa huduma hizo jambo linalohatarisha afya zao.

Mbali na mzigo wa majukumu, Erica anasema hata nyumba waliyopatiwa na kijiji waishi na mhudumu mwenzie wa kike haina hadhi, kwa kuwa haina madirisha wala milango ya vyumba vya ndani, hivyo kukosa faragha kati ya familia na familia.

Wananchi wa visiwa vya Mandakerenge na Mvuna wakijiandaa kupanda mtumbwi katika bandari ya Kirando, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa. Picha na Elias Msuya
Wananchi wa visiwa vya Mandakerenge na Mvuna wakijiandaa kupanda mtumbwi katika bandari ya Kirando, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa. Picha na Elias Msuya

Upungufu huo wa zanahati na wahudumu wa afya unakwenda kinyume na Sera ya Afya ya mwaka 2007 inayoelekeza kila kijiji kiwe na zahanati moja ndani ya mzunguko wa kilomita tano na kila kata kuwa na kituo cha afya.

Diwani wa Kata ya Mkinga, Reuben Kisi anasema hakuna uwezekano wa sasa wa kujenga zahanati katika Kisiwa cha Mandauhuru kwa sababu ya uhaba wa fedha.

Hata hivyo, diwani wa Kata ya Kipili anayeishi Kisiwa cha Mandakerenge, Wilbrod Chakukila anasema Kisiwa cha Mvuna kimekosa huduma za jamii kwa sababu si makazi rasmi bali kinatumika kwa ajili ya makazi ya wavuvi tu.

“Kile ni kisiwa cha wavuvi wanaotoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Burundi,” anasema Chakukila.

Anakiri kwenda kufanya kampeni za uchaguzi katika kisiwa hicho akisema “hayo ni mambo ya kisiasa tu.”

Kuhusu changamoto za afya za Kijiji cha Mandakerenge, Chakukila anasema jitihada zimefanyika za kupata mtumbwi utakaosaidia kusafirisha wagonjwa waliozidiwa kwenda katika kituo cha afya kilichopo Tarafa ya Kirando na wananchi wanapaswa kuchangia gharama za mafuta.

Kauli ya mbunge

Mbunge wa jimbo hilo, Ally Keissy amekiri kufahamu kero za huduma za afya katika visiwa hivyo na amechukua hatua ikiwemo kutoa mtumbwi wenye injini ili utumike kusafirishia wagonjwa wakati wa dharura Mandauhuru.

Anasema katika Kisiwa cha Mandakerenge kuna zahanati na tumeweka mtumbwi wa kusafirishia wagonjwa wakati wa dharura.

“Kuna visiwa kama Mvuna hatutajenga zahanati kwa sababu siyo makazi ya watu, ni makambi ya wavuvi. Kumejaa raia wa Congo na Burundi, tumeshawaambia wahame lakini hawasikii,” anasema.

Keissy anasema katika Tarafa ya Kirando kuna hospitali ya kisasa yenye chumba cha upasuaji inayotoa huduma kwa visiwa hivyo.

Uhaba wa zahanati na wahudumu wa afya unaikabili wilaya nzima ya Nkasi na taarifa za halmashauri hiyo zinaonyesha kuna upungufu wa zahanati 44 sawa na asilimia 52 kati ya mahitaji ya zahanati 90.

Mpaka sasa wilaya hiyo haina hospitali yake badala yake inatumia kwa ubia hospitali inayomilikiwa na shirika la dini na ndiyo hospitali teule ya wilaya.

Ally Keissy, Mbunge wa Nkasi

 

 

Kwa upande wa watumishi wa afya, taarifa hizo zinaonyesha kuna upungufu wa asilimia 74 ya mahitaji ambapo watumishi waliopo ni 353 wakati mahitaji halisi ni watumishi 1,345.

Wakati Mwongozo wa Utumishi (staff establishment 2014) ukielekeza zahanati moja kuhudumiwa na wahudumu 20 wastani zahanati moja wilayani humo ina wahudumu watatu na wakati mwongozo ukitaka kituo cha afya kiwe na wahudumu 35, vituo vya wilaya hiyo vina wastani wa watumishi 35.

Mkurugenzi halmashauri azungumza

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nkasi Namanyere, Julius Kaondo amekiri kuwepo kwa changamoto hizo akisema kwa muda mrefu Mkoa wa Rukwa ulikuwa nyuma kimaendeleo.

“Tunajua wananchi wanaokaa visiwani kuwa wana changamoto nyingi ikiwemo afya na elimu na nyinginezo, lakini kama halmashauri tumejipanga kuzitatua hatua kwa hatua.

“Hapa hatuna hata hospitali ya wilaya, tuna hospitali ya ‘mission’ tumefanya nao ubia, lakini tuna kituo chetu cha afya ambacho sasa tunataka kiwe kinafanya operesheni mbalimbali. Tunajenga wodi kubwa ili kuboresha,” anasema Kaondo.

Akizungumzia kuhusu upungufu wa zahanati na wahudumu wa afya, Kaondo anasema wameshawaelekeza viongozi wa vijiji na kata kutenga maeneo ya kujenga vituo vya afya vya kata na kila kijiji kiwe na zahanati.

“Maeneo uliyoyataja, Mvuna, Mandauhuru, Mandaulwile na mengineo ni maeneo ya uvuvi na sisi huwa tunapeleka asilimia 20 ya mapato ya uvuvi kwenye mfuko wa vijiji hivyo. Ukifuatilia kwenye vijiji utakuta kwenye akaunti wana Sh10 milioni ya uvuvi. Zitumike katika shughuli za maendeleo.”

Akizungumzia huduma ya afya ya mama na mtoto, Kaondo anasema idadi ya wanawake wanaojifungulia katika vituo vya afya imeongezeka kutoka asilimia 48.5 mwaka 2010 hadi asilimia 84 mwaka 2015.

Waziri wa Afya

Alipoulizwa kuhusu kadhia hiyo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu amekiri kuwepo kwa upungufu wa watumishi wa Sekta ya afya, akisema Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa mikoa tisa yenye upungufu mkubwa zaidi.

“Tumechukua hatua kadhaa ikiwemo kuajiri madaktari 258 katika mwaka wa fedha 2016/17 na kuwatawanya mikoa na halmashauri ambazo zina upungufu ikiwemo Nkasi,” anaongeza.

Kuhusu juhudi hizo za kuongeza watumishi, anasema wameshatangaza nafasi za ajira za afya takribani 3,200 ambapo mchakato wake unatarajiwa kukamilika kabla ya Septemba 30, 2017.

“Sambamba na ajira mpya tumezielekeza mamlaka za mikoa (RAS)/halmashauru kuwatanya watumishi wa afya ndani ya maeneo yao ili kuweka uwiano mzuri,” anasema.

Waziri Ummy anasema mwaka huu sekta ya afya itapata mgao mkubwa wa watumishi kati ya ajira 52,000 zinazotegemewa kutolewa na Serikali mwaka wa fedha 2017/18.

Maria Mtili

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania