Sababu za CAG kuiagiza Serikali iwadhibiti wafanyakazi wenye mikopo lukuki

Nuzulack Dausen
September 28, 2017

  • CAG abaini watumishi wa umma 789 wa halmashauri mbalimbali nchini wanaokatwa sehemu kubwa ya mishahara yao kiasi cha kupunguza ufanisi kazini.
  • Azitaka halmashauri kutoidhinisha mikopo inayozidi theluthi mbili ya mishahara yao.
  • Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke asema atakayemkopesha mtumishi bila kuwasiliana na halmashauri ajue ameliwa.

[email protected]

Dar es Salaam. Licha ya sheria na miongozo ya Serikali kutaka watumishi wa umma wenye madeni wasikatwe zaidi ya theluthi mbili ya mishahara yao, kuna halmashauri 16 nchini ziliacha wafanyakazi 789 wakadizisha makato zaidi ya kiwango hicho.

Idadi hiyo ya watumishi imekuja baada ya halmashauri hizo kutodhibiti ukopaji miongoni mwa wafanyakazi wake ambao hukopa katika taasisi za fedha kiasi cha mikopo hiyo kutafuna sehemu kubwa ya mishahara yao na kuwafanya watumie muda mwingi kusaka fedha za kumudu maisha badala ya kuhudumia wananchi.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad ya mamlaka za serikali za mitaa ya mwaka 2015/16 inabainisha kuwa halmashari tatu zilizoongoza kwa kuwa na watumishi wengi waliokatwa zaidi ya theluthi mbili za mishahara yao ni Kwimba, Nsimbo (Katavi) na Manispaa ya Temeke ya Dar es Salaam.

Idadi ya wafanyakazi wanaokatwa makato zaidi ya asilimia 66 ya mishahara yao inafanana kabisa na iliopo kwenye ripoti ya ukaguzi ya CAG kwa mamlaka hizo katika mwaka wa fedha wa 2014/15.

Uchambuzi wa takwimu zilizopo kwenye ripoti ya mwaka ulioishia Juni, 2016 unaonyesha kuwa halmashauri ya Kwimba iliyopo mkoani Mwanza iliongoza nchini kwa kuwa na watumishi 282 waliokuwa wamekatwa zaidi ya asilimia 66 ya mishahara yao ikiwa ni sawa na zaidi ya theluthi ya wafanyakazi wote aliowabaini CAG.

Halmashauri za Nsimbo yenyewe ilikuwa na watumishi 121 waliokuwa wamekatwa kiwango hicho cha mshahara wakati Temeke ikiwa ya tatu baada ya kuwa na wafanyakazi 115.

Temeke ndiyo manispaa pekee nchini yenye kiwango kikubwa cha watumishi waliobainika kukatwa zaidi ya theluthi mbili ya mishahara yao kwa kuwa na zaidi ya wafanyakazi 100.

“Ukaguzi wa mishahara uligundua kuwa kuna baadhi ya wafanyakazi wanaopokea chini ya moja ya tatu ya mishahara na wengine hawapati kabisa mshahara kwa miezi mingi,” anasema Profesa Assad.

CAG anaeleza katika ripoti hiyo kuwa kitendo kilichofanywa na halmashauri hizo ni kinyume na Kifungu namba 3 cha sheria namba 7 ya Kudai Madeni ya mwaka 1970 na kuelezewa zaidi katika waraka wenye Kumb. Na.CE.26/46/01/1/66 wa tarehe 28, Novemba 2012.

Waraka huo unawataka wafanyakazi walipwe mshahara wa mwezi usiopungua theluthi mbili ya stahili zao za mshahara.

“Wafanyakazi wanaweza wasijishughulishe na kazi ipasavyo kwa kutafuta kipato cha ziada ili wakidhi mahitaji yao ya kujikimu,” anasema Profesa Assad katika ripoti hiyo ambayo iliwasilishwa bungeni miezi ya hivi karibuni.

Profesa Assad anazishauri halmashauri hizo kutoidhinisha mikopo ya mishahara ambayo makato yake yanazidi kiwango kilichowekwa na endapo mfanyakazi atakopa bila ya idhini ya mwajiri wake, halmashauri isishughulike na makato ya watumishi kwa niaba ya taasisi hizo za fedha.

Hata hivyo, halmashauri zimeeleza kuwa kwa sasa wanatumia mfumo madhubuti wa mishahara ambao hauruhusu tena uwezekano wa mfanyakazi kukopa zaidi ya theluthi mbili ya stahiki zake kazini.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Nassib Mmbaga aliimbia MwananchiData hivi karibuni kuwa matokeo hayo ya ukaguzi ni ya miaka iliyopita na kwasasa hakuna tena mfanyakazi mwenye madeni makubwa yanayomlazimu kukatwa zaidi ya kiwango kinachotakiwa.

“Hayo ni mambo ya zamani sana kipindi ambacho watumishi hasa walimu walipokuwa wanamalizana kimyakimya na wakopeshaji halafu baadaye wanaleta madai halmashauri. Siku hizi kuna system (mfumo) ambao unasaidia kujua kiwango cha madeni husika na ofisi ni lazima isaini kuidhinisha mkopo husika,” anasema.

Anasema baadhi wanaonekana bado wanakatwa kiwango hicho cha mishahara kwa sababu wanadaiwa na wadeni wao hivyo ni lazima walipe fedha zote walizochukua kwa kuwa hakuna namna ya kukwepa madeni yao.

Ili kuwapunguzia mzigo wafanyakazi hao, Mmbaga anasema wameshawajulisha wafanyakazi juu ya taratibu na ukomo wa ukopaji kuwa usizidi theluthi mbili na wakopeshaji nao wanajua jambo hilo ikiwemo utaratibu wa halmashauri kusaini kabla ya kukopeshana.

“Wakopeshaji wote ni lazima wawe wamesajiliwa na Wizara ya Fedha na Mipango na ni lazima pia waje kwetu tuwajue. Siku hizi ukimkopesha mfanyakazi bila halmashauri kujua hautalipwa. Hao wakopeshaji wakikopesha tu bila utaratibu watakuwa wamezitoa fedha hizo bure,” anasema Mmbaga.

 

 

 

 

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania