Wivu wa mapenzi wawamaliza Dodoma idadi ya visa vya mauaji ikipungua

Nuzulack Dausen
November 10, 2017

• Ripoti ya uhalifu na makosa ya barabarani ya mwaka 2016 inaonyesha sehemu kubwa ya mauaji yaliyotokea mwaka jana mkoani Dodoma yalisababishwa na wivu.
• Sehemu kubwa ya wakazi wa Tabora waliuawa mwaka jana kwa sababu ya kishirikina.

[email protected]
Dar es Salaam. Wakati visa vya mauaji vikizidi kupungua nchini, ripoti mpya ya uhalifu inaonyesha sehemu kubwa ya visa vinavyotokea mkoani Dodoma husababishwa na wivu wa mapenzi.

Ripoti ya Uhalifu na Makosa ya Barabarani ya mwaka 2016 iliyotolewa na Jeshi la Polisi inaonyesha kuwa matukio ya mauaji yaliyoripotiwa yalipungua kwa asilimia 6.8 kutoka 3, 560 mwaka 2015 had 3,318 mwaka jana. Hata hivyo, watu waliouawa mwaka jana walikuwa 3,439.

Uchambuzi zaidi uliofanywa na MwananchiData unaonyesha kuwa licha ya idadi ya matukio ya mauji kushuka bado uhalifu ni kinara katika makosa ya jinai, ukishika nafasi ya pili baada ya ubakaji uliokuwa na visa 7,645.

Maofisa watatu wa Serikali wateketezwa Dodoma

Sehemu kubwa ya visa vya mauaji, kwa mujibu wa ripoti hiyo, vilisababishwa na wizi wa mifugo, ujambazi, imani za kishirikina, wivu wa kimapenzi, visasi, ulevi, migogoro ya kifamilia, bahati mbaya, uchizi na ujambazi wa pikipiki na magari.

Mkoa wa Tabora umeonekana kuwa kinara cha visa vya mauaji vilivyofikia ikifuatiwa na mikoa ya Kagera, Geita, Dodoma, Mbeya na Mwanza huku mikoa ya visiwani Zanzibar ikiwa na kiwango kidogo zaidi ya matukio hayo.

Licha ya kuwa sehemu kubwa ya matukio ya mauaji kusababishwa na wizi, mkoani Dodoma hali ni tofauti. Uchambuzi wa takwimu hizo wa miaka miwili iliyopita unaonyesha kuwa watu wengi huuawa kwa wivu wa kimapenzi.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa mwaka jana wivu uliongoza kwa kusababisha watu wengi zaidi kuuawa baada ya watu 29 kati ya 178 kufariki kwa sababu hiyo ukifuatiwa na matukio ya nyumbani na wizi. Hata hivyo, kiwango hicho ni nafuu kuliko cha mwaka 2015.
Theluthi ya watu (asilimia 32) ya walioauawa mwaka 2016 katika makao hayo makuu ya nchi waliuawa kwa sababu nyingine ndogo ndogo.

Uchambuzi wa takwimu za uhalifu za mwaka 2015 uliofanywa pia na tovuti inayochambua na kuchapishwa takwimu huru ya Hurumap ilibainika kuwa takriban ya asilimia 38 ya vifo vilitokea kutokana na kupigana hadharani vilisababishwa na wivu.

Mwaka huo, watu 34 kati ya 211 waliauawa kutokana na wivu sawa na watu 16 kwa kila 100 waliouawa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Mroto anasema baada ya kupitia takwimu hizo ataweza kuelezea hali hiyo kwa kuwa sasa ni mgeni.

“Ukija ofisini tutaweza kueleza vyema,” anasema Kamanda Mroto.

Kamanda Mroto alianza katika mkoa huo mapema Agosti mwaka huu.
Hata wakati sehemu kubwa ya mauaji yakisababishwa na wivu Dodoma, watu wengi mwaka jana walioawa wengi mkoani Tabora walikuwa ni wazee polisi ikihusisha na imani za kishirikina.

Takwimu hizo za polisi zinaonyesha watu 48 kati ya 247 waliouawa mwaka 2016 walikuwa ni wazee ikiwa ni asilimia 19 ya wote waliopoteza maisha kutokana na uhalifu huo.

Kwa ujumla vifo vya zaidi ya robo (asilimia 27.5) ya waliouawa mkoani humo vilitokana na imani za ushirikina.

Katika ripoti ya takwimu za uhalifu ya mwaka 2016, jeshi la polisi linawasihi Watanzania kushiriki katika ulinzi na usalama wa mali zao na majirani zao na watoe ushirikiano pale unapobainika uhalifu ili kuhakikisha Taifa lipo salama.

“Kila mwanajamii anatakiwa kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote anafanya uhalifu katika eneo lake la kazi na ikitokea uhalifu umefanyika basi ahakikishe wahusika wamefikishwa mahakamani kwa ajili ya hatua za kisheria,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo iliyosainiwa na Mkuu wa Polisi wa zamani, Ernest Mangu Januari mwaka huu.

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania