Nuzulack Dausen December 1, 2017
• Utafiti huo unaonyesha matumaini katika kufikia malengo 90-90-90 ifikapo mwaka 2020.
• Watu wenye VVU waitaka Serikali itunge sheria ya ARVs.
• Wataalamu wa afya wanasema ufubazaji wa VVU unaongeza muda wa kuishi.
[email protected]
Dar es Salaam. Katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, Serikali imetoa matokeo ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi nchini wa mwaka 2016/17 yanayobainisha kuwa zaidi ya nusu (asilimia 52) ya watu wenye umri wa miaka 15 hadi 64 wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini vipimo vinaonyesha kuwa kiasi cha virusi mwilini kimefubazwa.
Matokeo ya utafiti huo uliozinduliwa leo Ijumaa, Desemba Mosi, 2017 na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan yanabainisha kuwa katika kundi la watu hao ambao kiasi cha VVU kimefubazwa asilimia 57.5 ni wanawake na wanaume ni asilimia 41.2.
Makali ya VVU mwilini hufubazwa na dawa za kufubaza virusi hivyo (ARVs) ambazo Serikali imekuwa ikizisambaza nchini kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa masuala ya afya ukiwemo mfuko wa dharura wa rais wa Marekani wa Ukimwi (Pepfar).
Wataalamu wa afya wanaeleza kwa ufubazaji wa VVU hufanya watu wenye virusi hivyo kuishi kwa muda mrefu kuliko wale ambao hawapati matibabu.
Utafiti huo uliofanywa kati ya Oktoba, 2016 hadi Agosti mwaka huu unaeleza kiasi cha VVU mwilini kwa watu wenye maambukizi ya virusi hivyo kimefubazwa kwa kiasi kikubwa kwa watu wazima ambapo takriban theluthi mbili (asilimia 64) ni wanawake wenye umri wa miaka 55 hadi 64 na asilimia 62 ni wanaume wenye umri huo.
“Kuna tofauti kubwa ya kijinsia ya kufubazwa kwa VVU mwilini katika kundi la vijana wenye umri wa miaka 25 hadi 34 ambapo asilimia 51 ya wanawake na asilimia 26 kwa wanaume wa umri huo, kiasi cha VVU mwilini kimefubazwa,” inasomeka sehemu ya ripoti ya utafiti huo wa tano tangu uanze kufanywa.
Hata hivyo, kati ya watu wanaoishi na VVU wenye miaka 15 na zaidi kufubazwa kwa VVU mwilini kunatofautiana kimkoa nchini kutoka theluthi mbili (asilimia 66) mkoani Kagera hadi asilimia 29 mkoani Arusha. Lindi, ripoti hiyo inaonyesha wote wanaoishi na VVU katika mkoa huo wa kusini mwa nchi virusi vyao vimefubazwa.
Takwimu hizo zinaeleza hadi sasa kuna watu milioni 1.4 wenye umri wa miaka 15 hadi 64 wanaoishi na VVU sawa na asilimia tano au watu watano kwa kila 100 wenye umri huo.
Soma zaidi: Ukimwi tishio Njombe
Utafiti huo ulifanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar na ICAP Tanzania kwa kushirikiana na wadau wengine wakiwemo Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), na Zanzibar (ZAC),na Maabara ya Taifa ya Afya za Jamii, Uhakiki, Ubora na Mafunzo (National Health Laboratory – Quality Assurance and Training Center – NHL-QATC).
Taasisi nyingine zilizoshiriki ni Mpango wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI (NACP), na Kitengo Shirikishi cha UKIMWI, Kifua Kikuu na Ukoma, Zanzibar (ZIHTLP).
Serikali imepanga kuwa ifikapo mwaka 2020 iwe imefikia malengo ya 90-90-90 ikiwa na maana kuwa asilimia 90 au watu tisa kwa kila 10 ya watu wanaoishi na VVU wawe wamejua hali zao za maambukizi, asilimia 90 ya waliopima na kugundulika kuwa wana maambukizi ya VVU wapatiwe tiba ya kufubaza makali ya VVU.
Pia, katika malengo hayo, Serikali inataka asilimia 90 ya wanaotumia dawa hizo za VVU katika miili yao viwe vimefubazwa.
Tayari utafiti huo mpya unabainisha kuwa lengo la 90 ya awali imefanikiwa baada ya matokeo kuonesha asilimia 90.9 ya watu wenye miaka 15 hadi 64 wanaojua hali zao kuwa wanaishi na VVU kutoa taarifa kuwa wanatumia dawa za kufubaza virusi hivyo.
“Kati ya watu wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15 hadi 64 ambao wametoa taarifa kuwa wanatumia dawa za kubaza VVU, asilimia 87.7 ya watu hao inaonesha kiasi cha VVU kimefubazwa. Kwa wanawake ni asilimia 89.2 na wanaume asilimia 84,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Pamoja na mafanikio hayo, nusu tu (asilimia 52.2) ya watu wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15 hadi 64 wanajua hali zao za maambukizi ya VVU huku wanawake ikiwa asilimia 55.9 wakati wanaume ni asilimia 45.3.
Hadi mwaka 2014, takwimu rasmi zilizochapishwa katika kituo huru cha takwimu (Opendata) na Hurumap zinaonyesha kulikuwa na vituo 2,672 vinavyotoa huduma na matibabu kwa watu wenye VVU nchi nzima.
Mwenyekiti wa Baraza la Watu wanaoishi na VVU (Nacopha), Justin Mwinuka amesema wamekuwa mstari wa mbele kuhamasisha jamii yote kupima na kuweka wazi hali zao za afya ili kupata huduma zinazotolewa na Serikali.
“Pamoja na jitihada hizi za Serikali, bado kuna changamoto mbalimbali ikiwmo uhaba wa dawa za magonjwa nyemelezi na zinakopatikana zinauzwa,” amesema Mwinuka katika hotuba yake.
“Uwezo wa watu wanaoishi na VVU (Waviu) wengi kununua dawa hizi kila mara ni mdogo mno hivyo tunashindwa kuzipata na kuathiri afya zetu na hata kufa.
Ili kukabiliana na hali hiyo, ameiomba Serikali Waviu wote kuwekwa kwenye mpango wa bima ya afya ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa urahisi.
“Pia, nashauri dawa za ARVs ziundiwe sheria ili kuwabana wale wanaocha na kuzitumia vibaya kwani Serikali inatumia gharama kubwa,” amesema.
Nuzulack Dausen
Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.