Hii ndiyo siri ya utofauti wa kipato kati ya wanaume na wanawake Tanzania

Nuzulack Dausen
September 10, 2017

 

*Wanaume wanapata kipato kikubwa, asilimia 11 zaidi ya kile wanachopata wanawake nchini

[email protected]

Dar es Salaam. Licha ya kipato cha mfanyakazi kwa mwezi kuongezeka nchini bado kuna mwanya mkubwa wa kimapato kijinsia baada ya wanaume kuingiza fedha nyingi zaidi kuliko wanawake.

Utafiti wa Ajira na Kipato wa mwaka 2014/15 uliotolewa mwaka huu unabainisha wastani wa kipato cha mfanyakazi kwa wanawake na wanaume ulipanda kidogo mwaka 2014 ikilinganishwa na mwaka 2013.

Hata hivyo, wastani wa kipato cha mwezi kwa wanaume mwaka 2014 kilikuwa Sh427,000 ikilinganishwa na wanawake waliokuwa wanapata Sh386,000 kwa mwezi. Wastani wa kipato kwa mwezi kwa wanawake ulipanda kwa Sh27,000 kwa mwezi wakati ule wa wanaume ulipanda kwa Sh17,000 kwa mwezi.

“Takwimu hizi zinabainisha utofauti mkubwa wa wastani wa kipato cha mwezi baina ya wanaume na wanawake katika sekta zote za umma na binafsi,” inasomeka sehemu ya kitabu kipya cha Takwimu muhimu za wanaume na wanawake Tanzania mwaka 2017.

Kitabu hicho kilichochapishwa hivi karibuni na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kinaeleza kuwa utofauti wa kipato unatokana na matokeo ya tofauti iliyopo katika kujihusisha na kazi za kiuchumi baina ya wanawake na wanaume.

Mbali na utofauti wa kimapato, kitabu hicho kinabainisha kuwa bado kuna kundi kubwa la wanawake ambao hawana ajira wakihaha kupata mkate wao wa kila siku.

Kwa kutumia takwimu za ripoti ya utafiti wa nguvu kazi wa mwaka 2014 (Integrated Labor Force Survey, 2014), kitabu hicho kinaeleza kuwa kundi la vijana wenye miaka 15 hadi 24 ndiyo waathirika wakubwa wa ukosefu wa ajira kuliko kundi la wenye umri mkubwa kidogo huku kiwango kikubwa kikiwa kwa wanawake kuliko kwa wanaume.

“Takwimu zinaonyesha kuwa ukosefu wa ajira ni mkubwa kwa wanawake wa makundi yote ya umri kuliko wanaume” kinaeleza kitabu hicho kilichoandikwa na Mariam Kitembe na Philbert Mrema wa NBS, Chisker Masaki (EASTC), Judith Luande wa Tume ya Kupambana na Ukimwi (Tacaids) na Joyce Mkina wa Asasi ya kiraia ya Haki Elimu.

Soma zaidi: Mjue mwanamke aliyepania kuwakomboa wanawake Tanzania

Ni sekta tatu tu za kilimo, uvuvi na misitu; ukarimu na malazi; na uzaaji wa bidhaa za rejareja, utengenezaji wa pikipiki na magari ambako wanawake wanafanya vyema.

Utafiti wa nguvukazi wa mwaka 2014 unaonyesha wanawake saba kati ya 10 wameajiriwa katika sekta za kilimo, misitu na uvuvi ikilinganishwa na wanaume sita. Lakini katika ajira za sekta ya ujenzi wanaume ni asilimia 4 wakati wanawake ni asilimia 0.1.

Takwimu za Sensa ya mwaka 2012 zilichambuliwa na kuchapishwa katika tovuti ya Hurumap Tanzania zinabainisha kuwa asilimia 51 ya watu wote nchini walikuwa ni wanawake huku kati ya hao asilimia 36 wakiishi vijijini.

Hata kwa wanaoishi mijini, takwimu hizo zinaonyesha wanawake bado ni wengi kuliko wanaume wakiwazidi kwa asilimia moja.

Mtafiti wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Patience Mlowe anasema kuwa mara nyingi utofauti wa kipato na kiajira kati ya wanaume na wanawake unahusiana na upatikanaji wa elimu rasmi na mtizamo hasi dhidi ya wanawake.

Anasema kwa miaka mingi wanawake walikuwa nyuma katika elimu rasmi jambo lililowafanya wawe nyuma pia katika kupata ajira rasmi katika kampuni binafsi na umma.

“Katika utafiti wetu wa hivi karibuni karibu asilimia 70 ya kampuni tulizozifanyia utafiti hususan viwanda zinaeleza kuwa zinapenda kuajiri wanaume kuliko wanawake.

“Huu mtazamo hasi unafanya wanawake moja kwa moja waachwe nyuma kwa sababu hata katika kazi za kilimo wanazofanya kila siku wanufaikaji wakubwa bado ni wanaume,” anasema.

Ili kuondoa utofauti huo, Mlowe anasema lazima itolewe elimu ya kutosha kwa umma kuwa wanawake nao wanaweza kufanya kazi kama wanaume zikiwemo za viwandani, udereva na maofisini.

“Pamoja na kwamba usawa wa kijinsia ni zaidi ya namba bado miongozo na sheria zinazotaka usawa wa kijinsia ni lazima zitekelezwe ili kufanya jinsia zote zinufaike na kuondokana na umaskini kwa kuwa kazi nyingi wanazofanya wanawake kama za kulea na za nyumbani hazina malipo,” anasema.

Soma zaidi: “Ujasiriamali unahitaji moyo wa kujituma na kujitoa”

Utofauti huo unatokea licha ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 kusisitiza usawa wa kijinsia na ushiriki sawa wa wanawake na wanaume katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Lengo namba tano la malengo ya maendeleo endeleo ya Umoja wa Mataifa yalipitishwa mwaka juzi linataka kufikia usawa wa kijinsia ifikapo mwaka 2030 na kuwawezesha akina mama na wasichana kuwa na uwezo sawa na wanaume.

Serikali imesema itaendelea kuwainua wanawake kiuchumi ili waweze kujikwamua na umaskini kwa kuwawekeza mazingira mazuri ya ufanyaji biashara ikiwemo kutumia taasisi mbalimbali za kifedha.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Hassan Suluhu. Picha ya Maktaba.

Hivi karibuni wakati akizindua tamasha la 14 la kijinsia la Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alisema Serikali itatumia mifuko ya uwezeshaji, Saccos na vikundi vidogo vidogo vya kuweka na kukopa maarufu kama Vikoba kuhakikisha wanawake wanajikwamua na umaskini.

Ili kuongeza kasi ya kufikia malengo hayo, Suluhu anasema kuwa wataiimarisha Benki ya Wanawake (TWB)–inayolegalega kwa sasa–iweze kutekeleza malengo yake ya kuwaweza wanawake na kwamba hadi wanaume watanufaika nayo.

 

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania