Madereva waluwalu wanavyowamaliza Watanzania barabarani

Nuzulack Dausen
October 10, 2017

  • Makosa ya kibinadamu yanasababisha zaidi ya robo tatu ya ajali zote nchini hususan uzembe wa madereva wa magari na bodaboda.
  • Wadau wataka Serikali iboreshe sheria za usalama barabarani ili kutoa adhabu kali kwa madereva.

[email protected]

Dar es Salaam. Licha ya ajali za barabarani kupungua, bado kiwango cha ajali zinazobabishwa na uzembe wa madereva wa magari na pikipiki nchini kinaongezeka hali inayoendelea kugharimu maisha ya Watanzania.

Katika robo ya kwanza ya mwaka huu, takwimu za  Jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani zinabainisha kuwa kiwango cha ajali kilishuka kwa asilimia 41 hadi 2,443 kutoka ajali 1,447 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Hata hivyo, uchambuzi wa takwimu hizo uliofanywa na MwananchiData unabainisha kuwa bado madereva waluwalu wameendelea kuwa chanzo kikuu cha ajali hizo baada ya kusababisha asilimia 72.5 ya ajali zote ikilinganishwa na asilimia 64.5 ya ajali zilizotokea kati ya Januari hadi Machi mwaka jana.

Soma zaidi: Waliokufa Ziwa Victoria wafikia 12

Soma zaidi: Walionusurika kifo Ziwa Victoria wamlaumu dereva

Kwa takwimu hizo, ina maana kuwa kwa kila ajali nne zilizotokea katika robo ya kwanza mwaka huu takriban tatu zilisababishwa na uzembe na tabia ya madereva kutotii sheria na taratibu za babarabarani zikijumuisha mwendokasi na kupishana bila kujali taratibu.

Visababishi vingine vikubwa vya ajali vilivyoorodheshwa na kikosi hicho ni watembea kwa miguu kutotii sheria za barabarani waliyosababisha ajali kwa asilimia 7.5 na ubovu wa magari kwa asilimia saba.

Hata hivyo, visababishi kama ubovu wa magari na ubovu wa miundombinu ambavyo baadhi ya madereva husingizia wakipata ajali vimezidi kupungua katika kusababisha ajali ikilinganishwa na robo ya kwanza ya mwaka jana.

Kwa miaka miwili ya hivi karibuni ajali za barabarani zimekuwa zikipungua mwaka hadi mwaka.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alilieleza Bunge wakati akisoma hotuba ya bajeti ya mwaka 2017/18 kuwa katika kipindi cha Julai 2016 hadi Machi mwaka huu ajali za barabarani zilipungua kwa asilimia 7 nyingi zikisababishwa na uzembe wa madereva.

Mwigulu alieleza kuwa katika kipindi hicho zilitokea ajali 1,552 zilizosababisha vifo vya watu 2,372 na majeruhi 6,074.  Idadi  hiyo ni ahueni ikilinganishwa na ajali 7,006 zilizosababisha vifo 2,589 na majeruhi 7,536 katika kipindi cha Julai 2015 hadi Machi, 2016.

“Wizara imeendelea kusimamia sheria ya usalama barabarani ambapo katika kipindi cha Julai 2016 hadi Machi 2017 madereva 6,500 wa magari mbalimbali na na pikipiki 5,865 walikamatwa na kupelekwa mahakamani kwa kukiuka sheria za usalama barabarani,” alisema Nchemba.

Ili kukabiliana na ajali za barabarani, Waziri huyo aliyeteuliwa tena na Rais John Magufuli kuendelea kuongoza wizara hiyo katika mabadiliko ya baraza la mawaziri yaliyofanywa mwishoni mwa wiki, alisema kwa sasa wamechukua hatua za kuzuia na kudhibiti vyanzo vya ongezeko la ajali za barabarani.

Nchemba alieleza kuwa hatua hizo ikiwemo kuelimisha watumiaji wa barabara inafanywa na Jeshi la Polisi kwa ushirikiano na Wakala wa barabara nchini (Tanroads), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra) na vyuo vya udereva vilivyosajiliwa.

Tazama zaidi kuhusu ajali Ziwa Victoria

“Hatua zilizochukuliwa ni kuongeza askari wa usalama barabarani, kuendeleza zuio la magari ya abiria kusafiri baada ya Saa 4 usiku, kudhibiti mwendokasi kwa kuweka vituo vya ukaguzi, wa ratiba za magari ya abiria, kufuta leseni za madereva wanaosababisha ajali kubwa, kuzuia leseni kwa muda kwa madereva wanaosababisha ajali ndogo na kutoa elimu ya usalama barabarani kwa njia ya redio na luninga,” anasema Nchemba.

Takwimu za kikosi cha usalama barabarani za mwaka 2015 zilizochapishwa katika tovuti ya takwimu huru ya Hurumap zinabainisha mwaka huo watu wanane kwa kila 100,000 walikuwa wakipoteza maisha kutokana na ajali za barabarani.

Bofya alama kwenye ramani kujua zaidi eneo ilipotokea ajali ya daladala Mwanza

Mwenyekiti wa mtandao wa mabalozi wa usalama barabarani nchini(RSA), John Seka ameiambia MwananchiData kuwa sehemu kubwa duniani ajali nyingi  asilimia 75 husababishwa na tabia za binadamu hususan kutofuata sheria na taratibu za barabarani.

“Sehemu kubwa ya visababishi vya ajali hizi vinaweza kuzuilika kama ulevi, mwendokasi, kutofunga mkanda, kutumia vitu vinavyopunguza umakini katika uendeshaji. Lakini ajali hizi haziwezi kupungua hata kama tunaelimisha watu kila siku bila kubadili mfumo wa sheria za usalama barabarani,” anasema Seka.

Soma zaidi: Usalama Barabarani wachanganue vyanzo vya ajali

Seka anasema kwa sasa hakuna faini kali zitakazofanya madereva kutii sheria ipasavyo kwa kuwa faini ni Sh30, 000 na baadhi hutoa rushwa ndogo tu kwa askari wa usalama barabarani na huachiwa.

“Lazima kuwe na sheria kali itakayomfanya dereva aogope kuvunja sheria,” anasema.

Kwa sasa anasema hakuna mifumo mingi ya kudhibiti ajali za barabarani ikiwemo kuwadhibiti wale wanaotumia simu wakati wakiendesha magari.

Seka anaeleza kuwa angalau Serikali imesikia kilio chao na Oktoba 13 imeitisha mkutano wa wadau jijini Dar es Salaam utakaojadili namna ya kuboresha sheria zinazosimamia usalama barabarani.

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania