Mauzo ya hisa yaporomoka DSE

Nuzulack Dausen
March 13, 2017

[email protected]

Hali haikuwa nzuri sana katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) wiki iliyopita baada ya mauzo ya hisa kushuka takriban mara nne kutoka Sh5 bilioni hadi Sh1.3 bilioni wiki iliyopita kutokana na kushuka kwa idadi ya hisa zilizouzwa sokoni hapo.

Ripoti ya DSE kwa wiki iliyoishia Machi 10 mwaka huu inaonyesha kuwa hisa zilizouzwa na kununuliwa sokoni hapo ziliporomoka kutoka milioni 2.2 hadi 640,000.

“Ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa katika soko umeshuka kwa takriban Sh1.1 trilioni kutoka Sh20.3 wiki iliyopita hadi Sh19.2 trilioni.

“Hii ni kutokana kupungua kwa bei za hisa za kampuni zilizoorodheshwa kutoka kwenye masoko jirani ambazo thamani zake hutokana na mwenendo wa masoko hayo,” inasema ripoti hiyo iliyotolewa na Patrick Mususa, Meneja wa miradi na maendeleo ya biashara wa DSE.

Hata hivyo, mtaji wa kampuni za ndani wa soko hilo lenye wawekezaji zaidi ya 500,000 umeendelea kubaki katika kiwango cha kawaida cha Sh7.4 trilioni wiki hadi wiki.

Pamoja na soko hilo kutetereka kidogo, bado kuna kampuni tatu zilizofanya vizuri sokoni zikiongozwa na Swissport (Swiss) ambayo mauzo yake yalipaa kwa asilimia 51.

Nyingine ni kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambayo mauzo yaliongezeka kwa asilimia 37.3 wakati Benki ya CRDB ikishuhudia mauzo yake yakipanda kidogo kwa asilimia 5.2.

Mbali na mwenendo wa uuzaji hisa, mauzo ya hati fungani nayo yalipungua kwa Sh960 milioni kutoka thamani ya Sh1.08 bilioni wiki iliyopita hadi Sh113 milioni.

“Hii inatokana na mauzo ya hati fungani mbili za Serikali zenye thamani ya Sh127 milioni na hati fungani moja yenye thamani ya Sh2 milioni kwa jumla ya gharama ya Sh113 milioni,” anaeleza Mususa.

 

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania