Mfumo mpya wa uuzaji korosho ulivyoleta pesa tele katikati ya malalamiko

Nuzulack Dausen
March 16, 2017

Reginald Miruko, Mwananchi

[email protected]

Mtwara. Msimu wa korosho ulioshia Februari mwaka huu katika mikoa ya Lindi na Mtwara huenda ukawa ni msimu bora kuliko yote kwa wakulima baada ya mauzo yao kupaa kwa zaidi ya mara mbili.

Tofauti na misimu iliyopita, katika msimu huo ulioanza Septemba mwaka jana, Serikali ilianzisha mfumo mpya wa mauzo ya korosho kwa kuendesha minada kila wilaya badala ya utaratibu wa zamani wa kuuza zao hilo katika mnada mmoja huku kiwango kikubwa kikiuzwa kwa utaratibu usioratibiwa.

Pia katika msimu huo Serikali ilipunguza baadhi ya makato yaliyokuwa yanakwenda kwa vyama vya ushirika, huku ikiweka udhibiti unaoshirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kuzuia korosho kuuzwa kiholela maarufu kama ‘kangomba’.

Katika utaratibu huo wa stakabadhi ghalani, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego alisema wakulima wa korosho wanatakiwa kupeleka mazao yao kwenye vyama vya msingi vya ushirika, kisha vyama hivyo kupeleka kwenye maghala makuu kwa ajili ya mnada na umesaidia wakulima kupata malipo mazuri.

Kutokana na udhibiti huo, korosho yote imeuzwa kwa pamoja kwa matakwa ya wakulima ambao wanashirikishwa kuteua mzabuni mwenye bei nzuri kwenye mnada, tofauti na awali walipokuwa wanalipwa kwa mafungu.

Utaratibu huo mpya kwa mujibu wa takwimu za Bodi ya Korosho Tanzania umechangia kuongeza mauzo ya zao hilo kutoka tani 158,000 msimu uliopita hadi tani 255,000 kufikia mwishoni mwa Januari kwa sababu yote yameuzwa katika utaratibu unaoratibiwa.

Ongezeko hilo ni zaidi ya mara moja na nusu ya kiwango cha msimu uliopita. Takwimu hizo ni kabla ya msimu haujamalizika mwezi Februari.

Hali hiyo ndiyo inaelezwa kuwa chanzo cha taarifa zilizotikisa kwenye masikio ya wengi kuwa “Korosho imetema pesa hadi mbuzi wanapewa soda”.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Hassan Jarufu alisema pamoja na utaratibu huo, ubora wa korosho iliyopatikana katika msimu huu ulichangia kwa sehemu kubwa katika mabadiliko ya bei.

Ongezeko la kihistoria

Alisema bei ya zao hilo ilipanda hadi kati ya Sh3,700 na Sh4,000 kwa kilo, wakati bei elekezi ya msimu iliyokuwa imepitishwa na kikao cha wadau waliokutana Bagamoyo ilikuwa Sh1,300.

Uchambuzi wa takwimu uliofanywa na Mwananchi katika minada 10 ya awali iliyokuwa chini ya chama kikuu cha ushirika cha Mtwara na Masasi (Mamcu), unaonyesha kuwa bei ya chini ilikuwa ni Sh2,610 kwa kilo ambayo bado ni kubwa mara mbili ya elekezi.

Miaka ya nyuma wakulima wamekuwa wakiuza korosho zao kwa wastani wa wa Sh1,200 kwa kilo.

Mbali na utaratibu mpya wa mauzo na udhibiti wa kangomba, Jarufu alisema wakulima waliandaa mashamba yao vizuri, kupiga dawa kwa wakati na hivyo kupata korosho bora kuliko zilizopatikana katika nchi nyingine kama Msumbiji na nyingine za Afrika Magharibi.

“Wanunuzi wengi walikuja Tanzania kwa sababu tulikuwa na korosho bora, mfumo mpya umechangia kwa sababu kila mfanyabiashara alikuwa anashindana kutoa bei nzuri,” anasema Jarufu.

Kwa mujibu wa Jarufu wakulima wameongeza uelewa jinsi ya kutunza mashamba ili kupata mazao bora kutokana na elimu inayotolewa na anatarajia mwakani watapata mazao bora zaidi.

Hata hivyo, mfumo huo mpya umeanzishwa wakati pia kukiwa na mabadiliko mbalimbali ya kiuzalishaji na kisoko ndani na nje ya nchi hususan kuporomoka kwa uzalishaji katika nchi maarufu kwa zao hilo kama Vietnam.

Kwa mujibu wa Shirika la habari la za biashara duniani Bloomberg, uzalishaji wa korosho nchini Vietnam inayoongoza kwa kilimo hicho ulipungua kwa asilimia 11 mwaka jana huku mahitaji yake yakiongezeka kwa asilimia 53 tangu 2010.

Bloomberg inaeleza kuwa ukame mkubwa katika nchi hiyo ambayo inabeba soko kwa asilimia 58, ndilo sababu ya kupungua kwa uzalishaji huo.

Hali hiyo inaelezwa na wachumi kuwa pengine ndiyo neema kwa nchi nyingine zinazozalisha korosho ikiwamo Tanzania.

Kaimu Meneja wa Mamcu, Potens Rwiza hakubaliani kuwa malipo makubwa waliyopata  wakulima wa korosho msimu huu yalitokana na mfumo mpya kama inavyoelezwa bali kuanguka kwa uzalishaji wa zao hilo katika nchi zinazoongoza kama Vietnam.

Alisema katika kanuni za biashara, kwa kuongezeka kiwango cha korosho nchini kama ilivyokuwa mwaka huu bei yake ingeshuka, lakini hapa bei imeongezeka kwa sababu mahitaji ya zao hilo kwenye soko la dunia ni makubwa.

“Mauzo yameongezeka na pesa iliyopatikana mwaka huu ni kubwa, ukweli sahihi utaonekana mwakani,” anasema Rwiza ambaye ni mhasibu kitaaluma.

Rwiza anauangwa mkono na mfanyabiashara anayenunua korosho kwa wakulima na kuuza nje ya nchi, Abdul Hamad anayesisitiza kuwa bei nzuri ya msimu huu inatokana na hali ya mauzo duniani.

 Furaha, kilio cha wakulima

Mabadiliko ya mfumo wa uuzaji wa korosho ni pesa tele katikati ya malalamiko kibao.

“Pamoja na kuwa sijapata pesa zangu zote, lakini malipo niliyopata mwanzoni yalikuwa mazuri na yameniwezesha kufanya mambo mengi. Nimenunua usafiri wangu wa pikipiki,  sina shida tena,” alisema Mohammed Makwetu, mkulima wa zao hilo katika Kijiji cha Chikwaya, Nanyamba.

Lakini Hamis Chimela wa kijiji hicho, alisema pamoja na mfumo huo kuwa mzuri ila ni mgumu kwa sababu hawajauzoea.

“Kwa kupata pesa kwa pamoja, tumeweza kutenda mambo tuliyokusudia. Awali tulikuwa tunalipwa robo, baada ya muda unapewa nyongeza, na kisha unalipwa pesa nyingine kidogo, utaratibu haukuwa unaeleweka, lakini sasa ukiuza unapewa pesa yako mnamalizana,” alisema.

Licha ya wakulima hao kunufaika na mfumo huo mpya, bado baadhi wameendelea kusubiri malipo yao huku wakiwa na stakabadhi zisizo rasmi.

Mtendaji wa kijiji hicho, Hassan Mdidi alisema pamoja na wakulima kupata fedha kwa mkupuo na kujenga nyumba na wengine kuchimba visima lakini fedha nyingi zimechelewa kwa wiki tatu hadi mwezi mmoja na hawapewi stakabadhi halisi bali vipande vya karatasi.

Mkazi wa Kijiji cha Chikwaya, Halmashauri ya Nanyamba, Mtwara, Mohammed Makwetu akionyesha vipende vya karatasi wanavyopewa wakulima badala ya risiti za mauzo ya korosho baada ya kukosekana. Picha na Reginald Miruko

Akijibu malalamiko ya ucheleweshaji, Katibu wa Chama cha Msingi cha ushirika (Amcos) kijijini hapo, Mawazo Mawazo, alisema tatizo linatokana na kutotengwa fedha za uendeshaji, kama kusafirisha korosho kutoka ghalani hadi ghala kuu la Mamcu.

Kuhusu kutopewa risiti, alisema hilo limekuwa tatizo kwa kuwa Mamcu iliwapatia kitabu kimoja cha risiti chenye kurasa 200, lakini wakulima wako zaidi ya 500 na kila mmoja hauzi korosho mara moja, hivyo wanalazimika kuwaandikia stakabadhi kwenye vipande vya karatasi za daftari.

Mwenyekiti wa Amcos ya Mnyawi, Mohamed Bomba alisema ucheleweshaji huo umewaweka katika wakati mgumu na wakulima wanadhani viongozi wa ushirika ndio wanawakwamisha.

Bosi wa bodi ya korosho, Jarufu licha ya kukiri kuwepo malalamiko hayo, alisema ya sasa ni madogo kuliko ambavyo yangekuwa katika mfumo wa awali.

Alisema safari hii mkulima anaona kwa uwazi mambo yanayofanyika na hii imejenga imani kubwa.

Alisema kwenye vyama vya msingi vijijini, mtu anapewa uhasibu kutokana uaminifu wake kwa wananchi, lakini si kwa elimu aliyonayo katika kuandaa na kutunza vitabu vya fedha.

“Pia, fedha zenyewe zimekuwa ni nyingi mno, mtu kama huyo (mhasibu) kushughulikia hadi Sh3 bilioni si kazi ndogo, ingekuwa milioni moja au mbili ingekuwa rahisi,” anasema Jarufu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nanyamba, Mtwara, Oscar Ng’itu anakiri kuwapo malalamiko kadhaa ya wakulima, akisema mengi yanatokana na kukosa uelewa.

Ng’itu alisema udhibiti wa kangomba ndiyo sababu ya kuongezeka kwa mauzo katika msimu huu kwa kuwa hakuna korosho inayovushwa kutoka wilaya moja kwenda nyingine.

Mfumo mpya haujaharakisha tu malipo bali umeongeza usalama wa fedha.

                 Habari zaidi juu ya korosho tazama video

Mfanyabiashara Hamad alisema mfumo mpya ni rafiki zaidi kwa wafanyabiashara ambao awali walikuwa wanalazimika kusafirisha mabulungutu ya noti kwenda kununua korosho vijijini. Lakini kwa sasa wanalipa moja kwa moja kwenye akaunti za vyama vya ushirika jambo linalopunguza gharama za uendeshaji.

Hata hivyo, alisema minada inayofanyika wilayani ina harufu ya rushwa, akitoa mfano kuwa unaweza kuomba zabuni ukakuta mshindani amekushinda kwa shilingi moja tu, ishara inayoonyesha huenda zabuni zinafunguliwa mapema.

“Zabuni unapeleka leo inafunguliwa kesho asubuhi, inatakiwa mwisho wa kupokea zabuni uwe leo na papo hapo zifunguliwe,” anasema.

Mbali na hilo, mfanyabiashara huyo alisema katika ununuzi wafanyabiashara wanaathiriwa kimapato na  kiwango cha unyaufu ambacho kinatofautiana kati ya mamlaka na nyingine kutoka asilimia 0.5 hadi asilimia 0.9.

“Yaani korosho hata ukiingiza leo kwenye ghala na kuitoa kwa wanakata shrinkage (unyaufu), hii inanyauka na kupungua uzito saa ngapi? alihoji Hamad.

Hamad pia anazungumzia urasimu katika utoaji vibali vya kusafirisha korosho, akitolea mfano gari likiharibika, kuwa lazima mfanyabiashara arudi alipoanzia au amchukue ofisa wa Bodi ya Korosho hadi kwenye eneo la ajali ili kupewa kibali kingine na kuhamishia kwenye gari jingine.

Uchafu wa korosho tatizo

Pia alilalamikia uchafu katika korosho kwa kuwa wanaponunua kwenye mnada hawafungui mzigo kumbe baadhi ya wakulima au watendaji wa vyama vya msingi wasio waaminifu hufunga pamoja na mawe ili kuongeza uzito.

Alisema hawana kimbilio kwa kuwa wanunuzi wamejengewa dhana kuwa hawaaminiki.

Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prosper Ngowi alisema licha ya kutofanya utafiti, katika nadharia za uchumi huenda ongezeko hilo la bei likasababishwa na mambo matatu likiwemo kiwango cha korosho zilizozalishwa.

Mambo mengine ni nguvu ya wanunuzi katika soko na, au nguvu ya wakulima katika kudhibiti soko hilo kwa kuzuia unyonyaji.

Alisema inawezekana korosho ilikuwa imepungua mahali fulani, au nguvu ya wanunuzi ilipungua katika kudhibiti soko na kupanga bei au ile ya wakulima kudhibiti bei ya mazao yao ilikuwa kubwa.

“Nadhani hayo ndiyo yanawezekana kutokana na nadharia za kiuchumi, lakini ningependa kwenda kwenye eneo la tukio na kuchunguza zaidi ili kuja na sababu za kisayansi za ongezeko hilo,” alisema.

Mkuu wa mkoa Dendego alisema utaratibu huu una changamoto ndogo kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma, akitolea mfano wa malipo kuchelewa kuwa mnunuzi anatakiwa kulipa ndani ya siku sita, lakini  fedha ni nyingi hivyo inakuwa si rahisi kulipa kwa siku moja.

Alisema wakulima wengi hawana akaunti inabidi wachelewe kuandaliwa utaratibu ambao ni salama kwa fedha zao.

“Hata utaratibu wa kusindikiza fedha  kwenda kwenye vyama vya msingi 310 katika vijiji 792 nao ni sehemu ya kuchelewesha, lakini kwa ujumla changamoto ni ndogo kuliko zilizokuwapo awali,” anasema Dendego.

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania