Hatari iliyojificha
Dar es Salaam

Mabonde yote ya mito na vijito yamevamiwa na wakulima na wachimba mchanga

Dar es Salaam. Wengi ambao hupita barabara ya Banana-Msongola jijini Dar es Salaam huziona ‘bustani’ ndogondogo ndani ya mabonde ya vijito na mito inayokatisha eneo hilo.

Hata hivyo, kitu ambacho huenda wengi hawafahamu ni kuwa kuna mashamba makubwa zaidi ya hayo yaliyojificha yanayoonekana vyema iwapo wangepata fursa ya kupaa angani kwa angalau urefu wa mita 100 kama inavyoonekana hapo juu.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi ndani ya mabonde mbalimbali jijini hapa na kwa kutumia ndege isiyokuwa na rubani (drone), umebaini kuwa watu wamegawana sehemu kubwa ya maeneo oevu hususan mito na vijito katika vitalu vidogovidogo na baadhi hukodishiana kwa malipo ya mwezi.

Licha ya kifungu cha 57 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 kuzuia shughuli za kudumu za kiuchumi kwenye maeneo oevu ikiwemo mito hiyo, sehemu kubwa ya wakulima hao maisha yao huanzia hapo asubuhi na kumalizikia hapo jioni.

Baadhi ya wachuuzi wa mbogamboga wameshajua maeneo inakopatikana mboga hiyo kwa wingi kiasi cha kuwa soko la uhakika.

Sehemu ya vitalu vya bustani zinazolimwa ndani ya bonde la Mto Kivule. Picha na Bryan Mbuya/UhuruLabs/africanDRONE.

Sehemu ya vitalu vya bustani zinazolimwa ndani ya bonde la Mto Kivule. Picha na Bryan Mbuya/UhuruLabs/africanDRONE.

Kilimo haramu chafanywa wazi

Mkulima wa Msongola Yangeyange, Agnes Daniel anayelima mbogamboga katika bonde la Kivule anasema alinunua eneo analolima bondeni baada ya kuuziwa pamoja na kiwanja cha nyumba mwaka 2002. Wakati huo, eneo hilo kulikuwa na wakulima wachache tofauti na sasa.

“Nina matuta yangu hapa na mengine nakodisha kwa tuta moja Sh2, 000 kwa mwezi na mkulima anaweza kulipa hadi kwa miezi mitatu,” anasema Agnes.

Katika eneo anapolima Agnes na wenzake, vitalu vya bustani vimekatwa hadi sehemu yanapotakiwa kupita maji. Mikondo ya asili ya maji imechepushwa na kupitishwa katika vitalu hivyo ili kuhakikisha kuna maji wakati wote.

Ndani ya mita 20 za mto huo wa mwisho kukatisha barabara ya kuelekea Msongola kuna wakulima zaidi ya watano  na kutokana na uhaba wa eneo, baadhi wanalima hadi kwenye kingo za mito na kukutana na makazi yaliyojengwa karibu na mabonde.

“Kwa sasa ni ngumu kupata matuta ya kulima kwa sababu kila mtu anataka kwa kuwa inalipa sana kulima mabondeni kutokana na soko la uhakika…watu wanakodi hadi tuta kwa Sh3,000 kwa mwezi,” anasema Emmanuel Ezekiel anayelima mchicha, matembele, na mnafu katika bonde hilo.

Ezekiel anasema tuta moja alilohudumia kwa wiki mbili linaweza kuzalisha Sh58, 000 kwa mzunguko wa kwanza wa mavuno na anaweza kuvuna mara mbili na tayari ana soko la uhakika katika masoko ya Buguruni na Ilala.

Alipoulizwa iwapo anajua athari za kulima mabondeni licha ya faida anazodai kuzipata, Ezekiel anasema; “Hajui na Serikali haijawahi wasumbua na viongozi huwa wanawaona wanalima.

Wingi wa watu wanaolima katika mabonde hayo, umefanya pia maji yanayopita kwenye mabonde yaliyokuwa na asili ya chemchemi yakauke kabisa wakati wa kiangazi.

“Zamani kulikuwa na chemchemi na maji yalikuwa mengi. Lakini sasa maji yamepungua naona yanaogopa watu,” anasema Agnes.

Kilomita tatu kutoka Msongola Yangeyange, Aziz Ali (59) analima chini ya daraja lililopo Kivule Nyan’gau na amekuwa akifanya hivyo kwa miaka 17 sasa.

Ali anayeishi Kitunda na kufanya shughuli za kilimo Kivule anajua kuwa hairuhusiwi kulima ndani ya mita 60 kutoka kwenye mto lakini anadai “njaa imewashika” na kuwafanya wakiuke taratibu.

“Tuliwahi kukaa kikao wakatueleza tusilime ndani ya mita 60 lakini kwa kuwa hakuna ajira ndiyo maana nalima mpunga na bamia ili nipate chakula na fedha za matumizi,” anasema Ali.

Ni tatizo la mkoa mzima

Kilimo kinachofanywa Msongola na Kivule ni taswira ya kilimo haramu kilichovamia sehemu kubwa ya mabonde ya vijito na mito yote ya Dar es Salaam ambayo kwa bahati mbaya imeminywa na makazi.

Mbali na makazi, baadhi hutumika kutiririsha maji machafu ya viwandani na kutupa takataka jambo linalochochea kiwango kikubwa cha mafuriko na magonjwa.

Kuanzia mabonde ya mito inayopita katika maeneo ya Msongola, Kivule, Kitunda, Segerea, Tabata, Kigogo, Mabibo, Kawe, Mbezi hali ni hiyo hiyo. Kama wakulima hawalimi bustani pembezoni au ndani ya mito na vijito basi wanafanya uchimbaji haramu wa mchanga.

Kama ilivyo kwa wanaolima mabondeni, wanaochimba mchanga huchimba katika maeneo ya wazi yanayoweza kuonwa na wananchi wote na viongozi.

Baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa zaidi na uchimbaji mchanga ni Kinyerezi darajani, Kigogo, Jangwani, Mbezi, Tegeta na Kawe.

Jinamizi la uchimbaji mchanga Dar

Mchanga nao huchimbwa kwa uwazi bila kuogopa mamlaka

Ni shughuli haramu iliyosambaa kwa kasi zaidi Dar es Salaam

Wachimbaji hao haramu wa mchanga huchimba katikati ya mikondo ya mito na vijito na wengine baada ya kufika kwenye miamba migumu huchimba pembezoni mwa mito na kumomonyoa kingo jambo linaloruhusu maji kuyafikia makazi wakati wa mvua kubwa.

“Sisi tunachimba mchanga kwenye mkondo tu na huwa tunachimba wakati wa maji yamejaa pekee kwa sababu yakikauka mchanga hauji,” anasema Ali Njozi, mchimbaji wa mchanga Mbezi Mtoni.

Njozi, ambaye amekuwa akifanya shughuli hiyo kwa miaka miwili sasa, anasema eneo hilo ni kijiwe cha vijana wengi ambao huchimba mchanga licha ya kuwa ni kinyume na sheria kutokana na kukosa ajira huku akidai kuwa kwa siku mtu anaweza kupata angalau Sh10,000.

Pamoja na wataalamu kuonya kuwa uchimbaji mchanga kwenye mito unaathiri mazingira na kuwa pia kuwa kichocheo cha mafuriko, Njozi anasema haamini kama shughuli yao inasababisha madhara makubwa kiasi hicho na kwamba ikitokea wamechimba kingo za mito “wananchi huwa wanaandamana.”

Katika eneo la Mbezi Mtoni pekee kuna wakati vijana  hadi 200 hujumuika kuchimba mchanga huo ambao hununuliwa na watu mbalimbali wanaofanya shughuli za ujenzi, anasema Andrew Mwenda, mchimbaji wa mchanga anayeishi Kawe.

Katika maeneo hayo ya Mbezi, Kawe na Kigogo, ndani ya mto kuna malundo ya mchanga unaochimbwa na vijana hao na baadaye malori huingia wakati mwingine kwa siri kuubeba.

Wachimbaji wa mchanga wakiendelea na shughuli yao katika eneo la Kigogo jijini Dar es Salaam. Picha na Ericky Boniphace/Mwananchi.

Wachimbaji wa mchanga wakiendelea na shughuli yao katika eneo la Kigogo jijini Dar es Salaam. Picha na Ericky Boniphace/Mwananchi.

Kama ilivyo kwa wakulima, wachimba mchanga nao wanajua kuwa wanachofanya ni kinyume na sheria na hatari kwa mazingira lakini wanasingizia kuwa wanaolima ndiyo hutifua ardhi na kuifanya iathirike zaidi wakati wa mafuriko.

Picha za drone zinaonyesha kuwa sehemu kubwa ya mito ya jiji hili iliyovamiwa zaidi na kilimo inalimwa hadi kwenye kingo kiasi cha kuzifanya ziwe dhaifu na kuvunjwa pale mafuriko yanapotokea na kupeleka maji mitaani.

Watalaamu wa mazingira wanaeleza kuwa uchimbaji mchanga na kilimo katika maeneo ya mabondeni vinasababisha mito na vijito kupoteza asili yake jambo linalofanya baadhi ya mito ihame mara kwa mara kunapokuwa na maji mengi.

“Uchimbaji mchanga unamomonyoa kingo za mito na kuharibu muundo asilia wa mito na kuifanya iwe na kona kona nyingi zisizosababishwa na tabia asilia,” anasema Profesa Pius Yanda, Mkurugenzi wa Kituo cha Masomo ya Mabadiliko ya Tabianchi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (CCCS-UDSM).

“Hii inasababisha mito kuhama wakati mwingine kuja hadi kwenye makazi ya watu au kingo kushindwa kuhimili mafuriko,” anaongeza.

Profesa Yanda, ambaye kwa sasa anafanya utafiti wa kilimo cha mijini, anasema pia uharibifu wa maeneo oevu na vichaka vya asili unaathiri baioanuai na unaongeza athari za mafuriko kwa kuwa maeneo hayo husaidia kupunguza kasi ya maji yanapokuwa mengi na kupunguza madhara kwa wakazi wa maeneo husika.

Hali halisi katika takwimu

Shughuli hizo haramu zinafanyika katika maeneo oevu ambayo ni sehemu ndogo ya ardhi iliyopo Dar es Salaam.

Takwimu za matumizi ya ardhi ya zilizotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam mapema Mei, 2017 zinaonyesha kuwa maeneo oevu yanayojumuisha mabonde, vijito na mitoni ni hekta milioni 4.59 sawa na asilimia 2.8 tu ya ardhi yote.

Takwimu hizo zinazorejea mpango wa matumizi ya ardhi ya mwaka 2012 zinaonyesha jiji hili lina hekta 319,416 pekee zilizotengwa kwa ajili ya kilimo mjini na hekta 516,273 kwa ajili ya machimbo kati ya eneo lote la Dar es Salaam ambalo ni hekta milioni 161.8.

Kuna kila dalili kuwa iwapo mamlaka hazitachukua hatua mapema, mabonde ya mito ya Dar es Salaam yataharibiwa kwa kuwa mahitaji ya mbogamboga na mchanga yanazidi kuongezeka kutokana na kuongezeka kwa watu na kukua kwa sekta ya ujenzi.

Hadi Desemba mwaka jana, Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) inakadiria Dar es Salaam ilikuwa na watu milioni 5.3 kutoka watu milioni 4.3 mwaka 2012, ikiwa ni asilimia 11 ya watu wote nchini.

Pia, jiji hili ndiyo kitovu kikuu cha biashara na kuvutia shughuli za ujenzi kwa ajili ya biashara na makazi ili kuhudumia ongezeko la watu na wawekezaji.

Wakazi waogopa ushirikina

Wakazi wa maeneo ya jirani wanalaumu Serikali kutochukua hatua dhidi ya makundi hayo mawili yanayoendelea na shughuli zao licha ya kuathiri mazingira.

Mkazi wa Kigogo Mbuyuni, Victor Mbega anasema wakulima ndiyo wanao wasababishia zaidi mafuriko kwa kuwa hulima na kupanda mazao hadi kwenye kingo za mito hivyo Serikali iwaondoe haraka.  

“Tunaoishi mabondeni tunawaogopa sana wanaolima kuliko wanaochimba mchanga ndani ya mto kwa sababu wanalainisha mto na maji yakija yanamomonyoa kingo na kuja kwetu na imetokea mara nyingi,” anasema Mbega ambaye eneo lake limeathiriwa zaidi na uchimbaji mchanga na kilimo haramu.

“Wakazi wa mtaa huu wanajuana nani analima na nani anachimba mchanga lakini kuzuiana ni ngumu kwa sababu baadhi ya wanaofanya vitendo hivyo ni washirikina,” anaongeza.

Viongozi wa mitaa wanaonekana kuzidiwa nguvu na makundi haya mawili baada ya kuwazuia bila mafanikio huku baadhi wakitishiwa maisha yao.

Mjumbe wa mtaa wa Mbezi Mtoni, Ashura Mbaruku anasema wamejitahidi kuwazuia lakini vijana wanaochimba mchanga ni wakorofi na sehemu kubwa hawakai mtaani kwao.

“Kuna siku mwenyekiti wa mtaa alienda kuwazuia lakini walitaka kuligonga gari lake na lori la kusombea mchanga na sijui kiburi hiki wamekitoa wapi.

“Hata sisi walishawahitaka kutudhuru na walitupiga marufuku wanawake kwenda kuwafuatilia,” anasema Ashura.

Hata hivyo, kuna baadhi ya viongozi hawajawahi chukua hatua yeyote.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kigogo Mbuyuni, Pili Songa anasema hawajawahi kuwaita kuwapa elimu wala kuwakataza watu wasilime katika bonde la Mto Msimbazi lililopo kwenye utawala wao licha ya kuwa shughuli hizo zina athari.

“Tulichofanikiwa hadi sasa ni kuzuia ni watu wasitupe takataka kwenye mto lakini wachimba mchanga wanaendelea licha ya kuwakataza mara kwa mara.

"Hii ni kwa sababu wachimba mchanga walikuwa na soko la uhakika na tulipobaini tulipiga marufuku malori ya kusomba mchanga yasiende wanapochimba tangu Aprili mwaka huu,” anasema Songa.

Kabla ya sheria kuchukua mkondo wake, Profesa Yanda anasema ni vyema Serikali ikabaini kuwa wengi wanaolima kwenye maeneo yaliyozuiwa na wanaochimba mchanga hufanya hivyo kutokana na kukosa ajira hivyo ni vyema kuchochea ukuaji wa ajira ili kuzuia shughuli hizo.

“Kwa hali ilivyo ujenzi bado utaendelea kwa kasi na mchanga unatumika sana hivyo ni vyema mamlaka zitenge maeneo zaidi ya machimbo yatakayosimamiwa kikamilifu ili kuwapatia fursa za ajira wanaochimba mchanga mtoni,” anasema.

Anasema pamoja na wakulima na wachimba mchanga mtoni kuchangia mafuriko bado janga hilo husababishwa zaidi na utupaji taka ngumu, ujenzi holela unaoziba njia asili za maji na kwa sasa kuongezeka kwa mvua Dar es Salaam kuzidi wastani wa miaka ya nyuma.

Mafuriko yamekuwa yakiikumba Dar es Salaam mara kwa mara na kusababisha vifo, uharibifu wa mali na magonjwa. Mwaka 2015 watu 12 walipoteza maisha jijini hapa kwa sababu ya mafuriko.

Serikali yajipanga kumaliza tatizo

Baraza la Usimamizi wa Mazingira la Taifa (Nemc) linasema kuwa linafahamu uwepo wa tatizo hilo na kwamba wamekuwa wakishirikiana na halmashauri za jiji la Dar es Salaam kuzitokomeza.

Mratibu wa Kanda ya Mashariki wa Nemc, Jafar Chemgege anasema sheria inakataza shughuli za kiuchumi ndani ya mita 60 ya mabonde ya mito na maofisa wa mazingira wa ngazi zote nchini wanajua wajibu wao wa kuisimamia na kutoa elimu kwa wananchi kukabiliana na uharibifu huo.

Chemgege anasema licha ya kuwa usimamizi katika maeneo unatakiwa ufanywe kwa kiasi kikubwa na halmashauri, Nemc bado huwa inafanya operesheni za kukamata wanaojihusisha na uchimbaji mchanga haramu na kukamata malori yote yanayotumika kuubeba.

“Kwa bahati mbaya baadhi ya shughuli za usafirishaji mchanga huo zinafanywa usiku lakini tukiwakamata tunawatoza faini.

“Sheria ya mazingira haiitaji watumishi wa baraza pekee kuna kamati za mazingira kila ngazi…hawa wangefanya kazi vizuri hakuna mtu angechimba mchanga wala kulima lakini tutalitatua kwa kuwa halmashauri zimeshaagizwa kutenga maeneo ya machimbo,” anasema.