Umbumbumbu wa Hesabu, Kiingereza unavyotishia mustakabali wa elimu Tanzania

Nuzulack Dausen
August 14, 2017

  • Wadau waishauri Serikali kuwekeza zaidi kwenye masomo hayo kusaidia uchumi wa viwanda

[email protected]
Msingi dhaifu wa masomo ya Hisabati na Kiingereza unazidi kudhoofisha elimu ya msingi nchini, jambo linalotishia mustakabali wa kuzalisha wataalamu bora watakaochochea maendeleo.

Uchambuzi wa kina wa takwimu mbalimbali za elimu ya msingi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kuwa masomo hayo yamekuwa na mwenendo usioridhisha, kuanzia ngazi ya elimu ya msingi kiasi cha kufanya wanafunzi wahitimu wakiwa hawana uelewa wa kutosha.

Hisabati na Kiingereza ni masomo yaliyofanya vibaya katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka jana, huku ufaulu wake ukishuka zaidi ikilinganishwa na mwaka 2015.

Kwa mujibu wa takwimu za Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), ufaulu wa Hisabati mwaka 2016 ulishuka kwa asilimia tatu ikilinganishwa na mwaka 2015 na kwa upande wa Kiingereza ulishuka kwa asilimia 12.

 

Hata hivyo, kiwango hicho cha ufaulu siyo bahati mbaya. Ripoti ya utafiti wa Uwezo wa mwaka 2015 uliochapishwa katika tovuti ya takwimu huru ya Hurumap, inabainisha kuwa uelewa wa masomo hayo miongoni mwa wanafunzi wa umri wa kati ya miaka sita hadi 16 bado ni mdogo.

Utafiti huo uliofanywa na asasi ya kiraia ya Twaweza unaeleza zaidi kuwa ni wanafunzi wanne pekee kati ya 10 waliofanyiwa tathmini nchini ndiyo waliokuwa na uelewa mkubwa wa somo la Hisabati.

Hata mijini ambako wengi huamini kuwa kuna kiwango kikubwa cha ufundishaji kwa kuwa walimu wengi hukimbilia huko, kiwango cha uwezo watoto kuelewa masomo hayo kinatofautiana.

Watoto wenye umri wa miaka kati ya sita na 16 Mbeya mjini, kwa mujibu wa ripoti ya Uwezo, wamewazidi kidogo uelewa wa somo la Kiingereza wenzao kutoka Temeke jijini Dar es Salaam.

Asilimia 50 ya watoto wa Mbeya mjini wanaelewa vyema Kiingereza ikilinganishwa na asilimia 45 ya watoto wa Temeke. Ni tofauti katika somo la Kiswahili ambalo takriban robo tatu (asilimia 72) ya wanafunzi katika wilaya hizo wanaelielewa vyema.


Wataalamu wa masuala ya elimu wanasema kuwa uelewa mdogo wa masomo ya Hisabati na Kiingereza kwa wanafunzi wa shule ya msingi nchini, unafanya watoto wengi washindwe kufanya vizuri wanapoingia sekondari.
Wanasema hali hii inasababishwa na kushuka kwa ari ya kufundisha miongoni mwa walimu na kubadilikabadilika kwa mbinu za utahini.

“Walimu wengi kwa sasa uwezo wao wa kuongea Kiingereza ni mdogo na hawafuati sarufi. Kiingereza hicho ndiyo wanatumia kufundishia watoto wetu ndiyo maana hawaelewi vyema,” anasema Dk Luka Mkonongwa, Mhadhiri wa elimu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).

Anasema mbali na uwezo wa walimu, watumishi hao wanafanyiwa vitendo vinavyowakatisha tamaa kama kucheleweshewa maslahi yao na kudhalilishwa ikiwamo kuchapwa viboko na viongozi wa Serikali mbele ya umma.

Dk Mkonongwa anasema ili kuongeza ufaulu wa masomo ya Kiingereza na Hisabati nchini, ni vyema Serikali ikakaa na walimu ili wafikie mwafaka wa njia za kuboresha ufundishaji na kuwapa maslahi yatakayoongeza ari.

Soma zaidi: Wadau walia na kuporomoka ufaulu wa somo la Hisabati nchini

Soma zaidi:  Nusu ya wanafunzi darasa la saba hawawezi Kiingereza cha darasa la pili

“Hatuwezi kuwa na uchumi wa viwanda kama walimu hawatathaminiwa. Pia, Serikali ilirudishe utaratibu wa maswali ya hesabu ya kukotoa ya ‘kazi, swali na jibu’ badala ya maswali ya sasa ya kuchagua,” anasema.

Serikali inasema kuwa inaendelea kuboresha sekta ya elimu ikiwemo kuajiri walimu wa shule za msingi hususan sayansi, ili kuwaandaa wataalamu wataosaidia kufanikisha mkakati wa nchi ya viwanda.

“Wanafunzi nao hawatakiwi kukimbilia tu masomo rahisi ya sanaa na inabidi wajitume na kutumia muda wao mwingi kusoma masomo ya sayansi ili wafanikiwe zaidi baada ya kuhitimu masomo,” anasema Mussa Iyombe, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-Tamisemi na kuongeza;
“Serikali itaendelea kuajiri walimu na wataalamu wa sayansi ili kupunguza uhaba wa wataalamu uliosababishwa miaka ya nyuma.”

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania