Utoro wa walimu wapoteza nusu ya muda wa masomo Tanzania

Nuzulack Dausen
October 5, 2017

  • Ripoti ya Benki ya Dunia yabainisha kuwa robo tatu ya watoto wa darasa la tatu Tanzania, Uganda na Kenya walishindwa kuelewa jina la mbwa baada ya kusomewa na wenzao kwa Kiingereza.
  • Walimu Tanzania wanatumia asilimia 55 tu kufundisha kikamilifu wakiwa darasani na kuacha muda uliosalia watoto wakikosa masomo.

[email protected]

Dar es Salaam. Wanafunzi wa shule za msingi za umma nchini hukosa takriban nusu ya muda wanaotakiwa kujifunza wakiwa darasani kutokana na utoro wa walimu hali inayopunguza ufanisi wa kuelewa vema masomo.

Ripoti ya utafiti mpya wa Benki ya Dunia (PDF kwa Kiingereza) unaongazia mafunzo umebaini kuwa walimu Tanzania hutumia asilimia 55 tu ya muda waliopangiwa kufundisha kikamilifu darasani na kuacha muda uliosalia ukipotea.

Utafiti huo unaoitwa ‘Ripoti ya Maendeleo Ulimwenguni mwaka 2018-Kujifunza ili kutimiza ahadi ya elimu (World Development Report 2018- Learning to realise education’s promise)’ unabainisha kuwa tabia hiyo inachochewa na utoro uliokithiri miongoni mwa walimu.

Hata hivyo, ripoti hiyo inaonyesha ahueni kidogo kwa wanafunzi wa Tanzania kuliko majirani zao wa Kenya, Uganda na Msumbiji. Nchini Kenya walimu hutumia asilimia 45 ya muda wa masomo kufundisha kikamilifu, Uganda asilimia 42 na Msumbiji asilimia 39.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa ziara za kushtukiza katika shule za msingi za umma katika nchi sita walizofanya utafiti (Tanzania ikiwemo), kwa wastani mwalimu mmoja kati ya watano hakuwepo shule kwa siku moja.

“Hata kwa wale waliokuwepo shule, huenda hawafundishi kwa kuwa katika nchi saba za Kusini mwa Jangwa la Sahara wanafunzi wanafundishwa kwa saa mbili na nusu kwa siku chini ya nusu ya muda uliopangwa,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inasema utoro huo wa walimu unaathiri mchakato wa watoto kujifunza matokeo yake baadhi wanahitimu wakiwa mbumbumbu wa mambo waliyotakiwa wayafahamu tangu wakiwa madarasa ya chini.

“Tatizo hili la utoro linapaswa kuangaziwa kwa karibu kwa kuwa sehemu kubwa ya bajeti za elimu inatumika kwa ajili ya kulipa mishahara ya walimu,” inaeleza ripoti hiyo iliyozinduliwa hivi karibuni.

Wanafunzi washindwa jina la mbwa

Katika kiwango cha kujifunza miongoni mwa wanafunzi, ripoti hiyo inaeleza kuwa robo tatu ya wanafunzi wa darasa la tatu wa Tanzania, Uganda na Kenya walishindwa kuelewa maana ya sentensi ya Kiingereza yenye tafsiri ya Kiswahili kuwa ‘jina la mbwa ni Puppy.’

Kwenye jaribio la kusoma, takwimu za watafiti hao wa Benki ya Dunia zinabainisha kuwa zaidi ya robo ya wanafunzi (asilimia 28) walishindwa kusoma angalau neno moja la ujumbe mfupi.

Matokeo kama hayo yaliwahi kutolewa na utafiti wa kutathmini mafunzo nchini ambao hufanywa na asasi ya kiraia ya Twaweza.

Utafiti wa Uwezo wa mwaka 2015, ambao takwimu zake zimechapishwa katika tovuti huru ya takwimu ya Hurumap Tanzania (Kiingereza), unabainisha ni asilimia 18.5 tu ya watoto wenye umri wa miaka sita hadi 16 walikuwa mahiri katika masomo yote.

Hali inaonekana mbaya zaidi katika somo la Kiingereza baada ya robo tatu (asilimia 79) ya watoto hao kushindwa jaribio la kiingereza la darasa la pili.

Hivi karibuni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (Duce) Dk Luka Mkonongwa aliiambia MwananchiData kuwa baadhi ya walimu uwezo wao wa kufundisha ni mdogo hususan somo la Kiingereza.

Mbali na uwezo mdogo wa ufundishaji, anasema walimu wengi hawana molari kutokana na mazingira magumu ya kazi kwa kuwa wengi hucheleweshewa maslahi yao baadhi hudharirishwa na viongozi ukiwamo kuchapwa viboko.

“Ili kuongeza umahiri katika masomo ya Kiingereza na Kiswahili nchini, ni vyema Serikali ikakaa na walimu ili wafikie mwafaka wa njia za kuboresha ufundishaji na kuwapa maslahi yatakayoongeza ari,” anasmea Dk Mkonongwa.

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania