Uwanja wa Songwe fursa mpya kibiashara

Nuzulack Dausen
April 10, 2017

Godfrey Kahango, Mwananchi [email protected]
Mbeya.
Miaka minne baada ya kuanza kutumika, Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Songwe (SIA) umeongeza wigo wa fursa za kibiashara na kurahisisha huduma za usafiri wa anga kwa wakazi wa Mbeya, huku ukianza kuunganisha kanda hiyo ya Nyanda za Juu Kusini na ulimwengu.

Katika kipindi hicho, kiwango cha mizigo na abiria wanaotumia uwanja huo wakiwamo wa kigeni wamekuwa wakiongezeka mwaka hadi mwaka ikilinganishwa na ilivyokuwa katika uwanja wa zamani uliopo katikati ya Jiji la Mbeya.
Uchambuzi wa takwimu kutoka ofisi ya meneja wa SIA unabainisha kuwa idadi ya abiria wanaosafiri kupitia uwanja huo imeongezeka takriban mara tatu ndani ya miaka mitatu kutoka abiria 46,572 mwaka 2013 hadi 133,796 mwaka 2015.

Hata hivyo, ni mwaka jana pekee ambapo abiria walipungua kidogo hadi kufikia abiria 117,839 jambo ambalo wachambuzi wa masuala ya biashara na uchumi wamelihusisha na kuadimika kwa fedha miongoni mwa wananchi kulikoathiri sekta nyingi nchini, ikiwemo ya usafiri wa anga.

Kiwango hicho kimefanya idadi ya abiria wanaosafiri kupitia uwanja huo kwa sasa kufikia wastani wa watu 12,000 kwa mwezi, ikiwa ni karibu mara 10 ya idadi ya awali iliyokuwa abiria 1,200.

Kwa upande wa usafirishaji wa mizigo, tangu kufunguliwa kwa uwanja huo ambao ni wa kisasa, mizigo inayosafirishwa kupitia uwanja huo imeanza kuongezeka hadi kufikia tani 55,000 kwa mwezi lakini ni midogo inayobebwa na abiria.

Kadri siku zinavyoenda raia wa nchi jirani za Zambia, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Malawi wamekuwa wakitumia uwanja huo.

Wageni hao, ambao huingia nchini kwa ajili ya shughuli za biashara na utalii, wamezidi kuifungua kibiashara Songwe na Mbeya na kuonyesha ishara chanya kuwa uwanja huo unaelekea kuwa kitovu cha biashara kati ya Tanzania na nchi za kusini mwa Afrika.

Takwimu za Idara ya Uhamiaji mkoani Mbeya zinaonyesha kuwa wageni waliongia kupitia uwanja huo wameongezeka takriban mara sita kutoka 21 mwaka 2013 hadi wageni 120 mwaka 2016.
Wakati huohuo, idadi ya wageni wanaotoka imeongezeka kutoka 19 mwaka 2013 hadi 85 mwaka mwaka 2016 ambapo ni sawa na ongezeko la zaidi ya mara nne.

Mrakibu msaidizi wa Uhamiaji mkoani Mbeya, Marco Matiko anasema kwa kipindi hicho, wageni wote wanaotumia uwanja huo ni wale wanaotumia ndege binafsi kwa vile hakuna ndege za abiria kutoka nje ya nchi.
“Ndani ya miaka minne wageni walioingia nchini kupitia Uwanja wa Songwe ni 299 na waliotoka ni 240. Idadi hiyo ya wageni inaongezeka kwa kuwa raia wengi wa kigeni wametambua kwamba uwanja huu ni pointi moja wapo ya kuingia na kutoka na unakubalika kimataifa.

“Hii inaleta picha kuwa endapo kutajitokeza ndege za abiria zinazotoka nje ya nchi moja kwa moja, idadi ya raia wa kigeni wanaotumia uwanja huo itaongezeka mara dufu,” anasema Matiko.

Hadi sasa kuna kampuni mbili za Fastjet na Air Tanzania zinazotoa huduma za usafiri wa abiria kila siku kati ya Dar es Salaam na Mbeya. Ndege nyingine zinazotumia huo ni za kukodi.
Air Tanzania ilianza safari zake hivi karibuni baada ya Serikali kuikodishia kampuni hiyo ndege mbili aina ya Bombardier Q400 zilizonunuliwa mwaka jana ili kuiongezea ufanisi.

Kuongezeka kwa idadi ya abiria wa ndani na nje ya nchi na mizigo inayosafirishwa kupitia uwanja huo, kunafungua fursa nyingi na kubwa za kiuchumi kwa wananchi wa mikoa yote ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini pamoja na nchi jirani kama vile Zambia, Malawi, Afrika ya Kusini na DRC.

Habari inayohusiana: Wafanyabiashara wanavyolilia ndege za mizigo Mkoani Mbeya
Dereva wa taksi anayefanya kazi zake uwanjani hapo, Noel Mwambuga anasema biashara ya kubeba abiria wanaoshuka Songwe imewapa madereva unafuu wa maisha, japo uvumilivu unahitajika kutokana na biashara kuwa na matokeo mseto siku hadi siku.
“Maana kuna siku neema inatushukia. Tunapata abiria wengi, lakini siku nyingine mambo yanakuwa magumu. Huwezi kulala njaa kabisa kama ratiba ya ndege ipo,” anasema Mwambuga.

Anasema kuwa kwa siku madereva wanaondesha magari madogo hawakosi fedha ya mafuta na kula nyumbani pamoja na baadhi ya siku kuwa na ukame kwa kuwa wana uhakika wa kuingiza angalau Sh20, 000 kwa siku.
Kasi ya ukuaji biashara katika uwanja huo imesaidia pia kuongeza mapato kwa Serikali.

Meneja wa uwanja huo, Amiry Hassan anasema mapato ya uwanja huo yamefikia Sh1.6 bilioni kwa mwaka, ongezeko ambalo ni mara tano zaidi ya mapato waliyokuwa wakikusanya uwanjani hapo zamani. Miongoni mwa fursa zinazotokana na uwepo wa uwanja huo mkoani Mbeya ni usafirishaji wa mazao kwa haraka kwenda masoko ya ndani na nje.

Fursa hii inatokana na ukweli kwamba wananchi wa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ni wakulima na wazalishaji wakubwa kwa wadogo wa mazao ya chakula na biashara, kama vile mahindi, kahawa, ndizi, maparachichi, mpunga, na chai.
Aidha wananchi hao pia wanaweza kutumia fursa ya uwepo wa uwanja wa ndege kujenga hoteli za kitalii, nyumba za kulala wageni na hata maghala ya kuhifadhia mazao jirani na uwanja wa ndege wa SIA kwa lengo la kuwarahisishia wafanyabiashara upatikanaji wa huduma kama hizo.


Uwepo wa uwanja wa SIA pia unafungua fursa ya kilimo cha maua, ambayo yana soko kubwa barani Ulaya ambako yanaweza kupelekwa kirahisi na kupata soko zuri na la uhakika, hivyo wakulima wakaweza kujiingizia kipato pamoja na viwanda kupata soko la bidhaa zinazozalishwa kwa kusafirishwa kiurahisi zaidi.

Hata hivyo, licha ya kuwepo kwa fursa lukuki, wananchi na wafanyabiashara wa Mbeya, mikoa mingine ya Nyanda za Juu kusini na hata nchi jirani za Zambia, Malawi, Congo na Afrika Kusini bado hawajaonekana kuutumia ipasavyo uwanja huo.
Uchunguzi wa awali unaonyesha fursa nyingi zitokanazo na uwanja huo hazijatumika kikamilifu kutokana na changamoto kadhaa zilizopo, kama kukosekana kwa ndege zinazofanya safari zake nje ya nchi.

Habari zinazohusiana:
Fastjet yashindwa kutua, Bombardier yashindwa kupaa
Fast Jet yashindwa kutua Songwe

Amiry anasema ingawa idadi ya abiria imekuwa ikiongezeka tangu kufunguliwa kwa uwanja huo, changamoto iliyopo ni uchache wa ndege za abiria.

Amiry anasema uwanja huo sasa unatoa huduma kwa ndege za abiria za ndani na za kukodi huku akibainisha kwamba hata sehemu kubwa ya ongezeko la mizigo inayosafirishwa ni ile midogo ya abiria na si mikubwa ya kibiashara.
“Kiwanja hiki kwa sasa kinahudumia ndege kubwa aina ya Airbus 319(A319) ndege ambayo inafanya safari zake mara mbili kwa siku ikiwa na uwezo wa kubeba jumla ya watu 160, idadi hii ni abiria pamoja na wafanyakazi,” anasema.

Abiria   wengi kuliko ndege.

Pamoja na idadi ya abiria kuongezeka, bado ndege zilizopo hazitoshelezi mahitaji.

Amiry anasema kutokana na ongezeko la abiria kutaka kutumia uwanja huo, mahitaji ya ndege nyingi zaidi zinazofanya safari za ndani na nje ya nchi yanazidi kukua kwa kasi.

Kwa sasa ndege zilizopo zinafanya safari kati ya Mbeya na Dar es salaam pekee. Kukosekana kwa ndege zinazoenda mikoa mingine kunafanya abiria wanaotumia usafiri wa kwenda Mbeya kutua kwanza Dar es Salaam ili kupata ndege ya kwenda sehemu nyingine za nchi.

“Lakini kuna kampuni nyingine za ndege zimeomba kufanya safari kati ya Mbeya na mikoa mingine,e hivyo tunaamini hiyo itachochea zaidi usafiri wa anga kupitia uwanja huu,” anasema Amiry.

Hakuna     ndege   ya mizigo

Pamoja na kiwango cha mizigo inayosafirishwa kupitia uwanja wa Songwe kuongezeka, bado hakuna ndege maalumu za mizigo ambazo zingechochea ukuaji wa biashara katika ukanda huo kwa wafanyabiashara kusafirisha shehena zao.

“Bahati mbaya sana, hakuna kampuni yoyote ya ndege iliyojitokeza kuleta ndege za mizigo hadi sasa. Ila kuna mahitaji makubwa   kwa ndege za mizigo kwa kuwa kuna wafanyabiashara wengi ambao wapo tayari kusafirisha bidhaa zao kupitia uwanja huu lakini shida ni hiyo tu,” anasema.

Anasema bado wanaendeleaa na mazungumzo na kampuni za ndege kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi ili zianzishe safari zao za ndege za mizigo ili wafanyabiashara waweze kusafirisha bidhaa zao.

Habari inayohusiana: Wafanyabiashara wanavyolilia ndege za mizigo Mkoani Mbeya

TCCIA yalia na kutokamilka uwanja

Ofisa mtendaji mkuu wa Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Kilimo, (TCCIA) mkoani Mbeya, Emile Malinza anasema kuna wafanyabiashara wengi ambao wapo tayari kutumia fursa hizo, lakini wanatatizwa na kutokamilika kwa baadhi miundombinu muhimu.

Anasema kuna wanachama wao ambao ni wafanyabiashara wakubwa wanaopenda kusafirisha bidhaa zao kwenda nje ya nchi, lakini wanashindwa kwa kuwa uwanja haujamilika na ndege za mizigo hazitui hapo.

“Kwa mfano, hata jengo la abiria lile kubwa bado halijakamilika, lakini pia hakuna maghala au majengo ambayo wafanyabiashara watayatumia kwa ajili ya kuhifadhia mizigo yao kabla ya kusafirishwa kwa ndege, hakuna kituo cha mafuta, lakini pia hata sasa watu wanashindwa kwa ndege hizi zinazotua kutokana na masharti ya usafiri kuwa si rafiki kwa abiria,” anasema Malinza.

Malinza anasema TCCIA Mkoa wa Mbeya inawahamasisha wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kuwekeza kwenye miundombinu ili uwanja huo ukamilike na fursa zilizopo ziweze kutumika kwa ufanisi.

Habari inayohusiana:  Wawekezaji, FastJet waonja joto la uchumi

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania