Nuzulack Dausen January 30, 2017
Saumu Mwalimu na Nuzulack Dausen
Wakati shule za msingi zikimaliza mwezi wa kwanza katika muhula mpya wa masomo wa 2017, walimu kutoka nusu ya shule za umma nchini watalazimika kufundisha idadi ya wanafunzi juu ya wastani unaotakiwa kutokana na uhaba wa watumishi hao.
Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inabainisha uwiano sahihi wa mwalimu kwa wanafunzi (PTR) katika shule za msingi kuwa ni mwalimu mmoja kwa watoto 40 (1:40).
Serikali imekuwa ikijitahidi kuajiri walimu lakini hadi Disemba mwaka jana, takwimu za Tamisemi zinaonyesha bado kulikuwa na uhaba wa walimu 47,151 wa shule za msingi, idadi inayozidi kidogo jumla ya walioajiriwa katika shule za msingi za umma na binafsi kwa miaka 10 iliyopita ambao ni 45,528.
Zisemavyo takwimu
Uchambuzi wa takwimu za uwiano wa mwalimu na wanafunzi kwa shule za msingi za umma mwaka 2016 uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa pamoja na jitihada za Serikali kuongeza watumishi wa umma, bado asilimia 58 ya shule za msingi zina uwiano wa juu ya kiwango kinachotakiwa.
Takwimu hizo zilizotolewa kutoka kituo huru cha takwimu zinabainisha kuwa hadi Machi mwaka jana, shule za umma 9,358 kati ya 16,083 zilikuwa na uwiano wa zaidi ya mwalimu mmoja kwa wanafunzi 40.
Takwimu za hivi karibuni kutoka Tamisemi zinaonyesha kuwa shule za msingi za umma ziliongezeka na kufikia 16,088 Disemba mwaka jana.
Uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi hupatikana baada ya idadi ya wanafunzi kugawanywa na waliopo katika shule husika na hutumika pia kupima utajiri wa rasilimali wa shule husika.
Katika uchambuzi wa takwimu hizo, kati ya shule hizo zenye walimu pungufu, zipo 345 ambazo mwalimu mmoja anafundisha wastani zaidi ya wanafunzi 100, jambo linalotishia mustakabali wa elimu nchini.
Hali siyo nzuri katika shule 15 ambazo mwalimu mmoja anafundisha zaidi ya wanafunzi 200. Mwananchi linaziweka shule hizi katika kundi la zenye uhaba mkubwa wa walimu nchini.
Kwa mujibu wa takwimu hizo zinazosimamiwa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), mikoa mitano yenye uwiano usioridhisha wa mwalimu kwa wanafunzi ni Kigoma ambao mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 59. Katavi (1:58), Mara (1:55), Mwanza na Singida zenye uwiano wa 1:54.
Mkoa wa Kilimanjaro unaongoza kwa kuwa na uwiano mzuri kwa mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi 33 ukifuatiwa na Arusha (1:37), Dar es Salaam (1:38), Iringa (1:39) na Njombe wenye uwiano wa 1:41.
https://datawrapper.dwcdn.net/amFVa/4/
Kati ya shule 10 zenye uhaba mkubwa wa walimu kwa mujibu wa takwimu hizo, sita zinatoka Kigoma ambazo ni Rukoma (Uvinza), Muhunga (Kasulu Mji), Muhamani, Sokoine, Makombe na Gombe.
Hata hivyo, gazeti hili linaitoa Sokoine kwenye orodha baada ya kujiridhisha kuwa ina walimu 22 tofauti na mmoja aliyebainishwa kwenye takwimu.
https://datawrapper.dwcdn.net/CtSKq/1/
Wakati baadhi ya shule zikiwa na uhaba mkubwa wa walimu, zipo baadhi ya shule zenye hali nzuri kama Sangasanga na Matambwe zilizopo halmashauri ya Morogoro vijijini na Irente liyopo Lushoto mkoani Tanga ambazo mwalimu mmoja hafundishi zaidi ya watoto sita.
Uwiano wa mwalimu na wanafunzi umekuwa ukiimarika mwaka hadi mwaka kitaifa baada ya kushuka kutoka mwalimu mmoja kwa wanafunzi 54 mwaka 2008 hadi 42 mwaka 2015.
Hali ilibadilika mwaka jana baada ya mwamko mkubwa wa kuandikisha watoto wa darasa la kwanza kutokana na sera mpya ya elimu bure iliyoanza kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano.
Mwamko huo ulifanya uwiano kupaa tena hadi mwalimu mmoja kwa wanafunzi 48 mwishoni mwa Julai mwaka jana huku idadi ya walimu ikiwa ileile.
Shule za msingi zisizo za umma zimekuwa na uwiano mzuri wa mwalimu kwa wanafunzi wa 1:25 hadi kufikia Disemba 2015 ukilinganisha na shule za umma zilizokuwa na uwiano 1:42.
Licha ya mafanikio katika uandikishaji wa wanafunzi katika elimu ya msingi na kushusha kidogo uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi, hali halisi inaonyesha kuwa kuna shule zenye hali mbaya ya uhaba wa walimu nchini ambazo mwalimu mmoja anafundisha wastani wa zaidi ya wanafunzi 100.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika mikoa ya Kigoma, Tabora na Morogoro umebaini kuwa Serikali ikiwekeza kwa walimu kiwango cha elimu kitaimarika baada ya shule zenye uwiano usioridhisha kufanya vibaya katika mtihani wa Taifa wa darasa la saba wakati zile zenye uwiano mzuri zikifanya vizuri.
Shule ya msingi Chohero ambayo ni miongoni mwa shule 15 zenye uhaba mkubwa wa walimu, ina walimu wawili waliokuwa wanafundisha wanafunzi 510 mwishoni mwa mwaka jana.
Ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu pamoja na ugumu huo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bernard Pius anasema wamegawana madarasa ya kufundisha, huku yeye akifundisha kutoka madarasa ya awali hadi darasa la tatu na mwenzake Henry Matanji akifundisha kuanzia darasa la nne hadi la saba.
“Mazingira ya kazi ni magumu,” anasema Pius. Walimu wengi tunaovumilia kufanya kazi hapa ni wenyeji wa Morogoro pekee, wengine kutoka mikoa mingine hawadumu kwa kuwa hakuna barabara na huduma nzuri za kijamii.”
Katika mtihani wa darasa la saba mwaka jana, Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) liliweka Chohero katika orodha ya shule 10 za mwisho baada ya kufaulisha wanafunzi sita kati ya 49 waliofanya mtihani huo.
Hali hiyo ni sawa na shule za msingi Sokoine, Bondo and Muhamani zilizopo halmashauri ya Kigoma vijijini.
Walimu Wakuu wa shule hizo wanaeleza kuwa uhaba huo wa walimu unatofautiana na aina ya masomo, huku Hisabati na Kiingereza yakiwa na ‘ukame’ mkubwa kiasi cha kuwalazimu kutumia walimu wasio na ujuzi nayo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi, Sokoine, Mohamed Athuman anasema hadi Disemba mwaka jana alikuwa na walimu 22 wakiwamo wanne waliopo masomoni wanaofundisha wanafunzi 902, hivyo anahitaji walimu zaidi ya sita ili apate uwiano unaopendekezwa wa 1:40.
Athuman anasema mwalimu wa darasa la kwanza alikuwa anafundisha wanafunzi 167 wakati wa la pili alikuwa na watoto 145.
Pia, pamoja na Rais John Magufuli kuagiza uongezaji wa madawati mwaka jana, shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa madawati 312, mara mbili ya yaliyopo sasa 154 na kufanya wanafunzi wa darasa la awali, la kwanza na la pili kukaa chini.
Shule hiyo ilikuwa ya 25 kati ya 30 katika halmashauri hiyo baada ya kufaulisha wanafunzi 38 kwa wastani wa alama B na C kati ya 68 waliofanya mtihani wa darasa saba mwaka jana.
Mwalimu Mkuu wa shule ya Igombe iliyopo Kaliua mkoani Tabora, Kasseka Iddy anasema wanashindwa kuwamudu wanafunzi, huku wakiwa na mzigo wa kusahihisha kazi jambo linalopunguza muda wa kuandaa masomo na kumwelesha mtoto kwa ukaribu.
Iddy alisema hali hiyo inaathiri na kiwango cha ubora wa elimu inayotolewa na kuiomba Serikali kutoa mahitaji yanayohitajika katika shule mbalimbali nchini ili kuongeza ufaulu.
Shule za kupigiwa mifano
Wakati Chohero na Sokoine zikikatisha tamaa, Sangasanga na Matambwe zilizopo Morogoro zina hali nzuri ya walimu na zinafanya vizuri katika mitihani.
Sangasanga iliyokuwa na wanafunzi 69 mwaka jana wakiwamo darasa la waliomaliza, ina walimu 11 hivyo kufanya uwiano wa mwalimu mmoja kufundisha wastani wa watoto sita jambo linalotoa fursa ya kuwaelewesha zaidi masomo wanafunzi.
Shule hiyo iliyopo ndani ya kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kambi ya Sangasanga 21KJ, imekuwa ya pili kwa miaka miwili mfululizo katika wilaya hiyo. Mwaka jana ilikuwa ya pili kati ya shule 78 zenye wanafunzi chini ya 40 na ya 33 kati ya shule 384 kimkoa. Wanafunzi wote walifaulu kwa wastani wa B.
“Ukiwa na wanafunzi wachache inakusaidia kuwaelewesha vizuri hata wanaochelewa kuelewa,” anaeleza Kaimu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Ruthbeth Mshana.
“Kwa mfano, kama unafundisha madarasa manne, maana yake una wastani wa madaftari 40 ya kusahihisha. Mwalimu anasahihisha kwa uhakika na inakupa muda wa kuandaa vizuri masomo,” anasema.
https://datawrapper.dwcdn.net/CtSKq/1/
Uwepo wa walimu kutosha umeonyesha mafanikio pia katika shule ya msingi Matambwe iliyopo katika hifadhi ya Selous ambayo hadi Disemba ilikuwa na walimu sita na wanafunzi 26.
“Kwa mwaka wa tatu mfululizo, tumekuwa tukiongoza kiwilaya katika mtihani wa darasa la saba,” anasema Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Hassan Kilindi na kuongeza:.
“Baadhi ya watu wanadhani hii ni shule ya mtu binafsi kumbe siyo na wengi waliopo nje ya hifadhi wanapenda kuleta watoto hao hapa, lakini haiwezakani kwa sababu hatuna hosteli.”
Kauli ya Serikali
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Elimu kutoka Tamisemi, Juma Kaponda anasema Serikali mwaka huu ipo mbioni kuajiri walimu 40,000 wa shule za msingi na 10,169 wa sayansi na hesabu ili kuondoa uhaba uliopo.
“Tayari tumeshatoa maelekezo kwa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanawapeleka walimu katika maeneo yote yasiyo na walimu hususan vijijini, ili kuhakikisha watoto wanapata elimu bora,” anasema.
Nuzulack Dausen
Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.