Manyara yaongoza kwa ukeketaji Tanzania

Nuzulack Dausen
February 9, 2017

Herieth Makwetta, Mwananchi

[email protected]

Dar es Salaam. Wakati ulimwengu ukiadhimisha wiki ya kutokomeza ukeketaji ulimwenguni, utafiti mpya umebaini idadi ya wanawake waliokeketwa inaendelea kupungua nchini kutoka asilimia 16 mwaka 1996 hadi asilimia 10 mwaka jana, huku sehemu kubwa ya waliofanyiwa vitendo hivyo wakiondolewa kabisa nyama ukeni.

Utafiti huo (ukurasa wa 16) wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria Tanzania wa mwaka 2015/2016 uliotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Takwimu ya Taifa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, umeeleza kuwa aina maarufu ya ukeketaji ni ile ya kukata nyama na kuiondoa kabisa inayofanyika kwa asilimia 81%.

Aina hiyo ya ukeketaji inatajwa na wataalamu kuwa ni hatari zaidi kwa afya za wanawake hao kwa kuwa umekuwa ukisababisha ongezeko la vifo vitokanavyo na uzazi.

Daktari wa Magonjwa ya Binadamu na Lishe kutoka Hospitali ya Bugando, George Kaanan anasema mwanamke akikeketwa na kuondolewa nyama yote anabaki na kovu kubwa ambalo humletea madhara wakati wa kujifungua.

“Anapojifungua lile kovu lazima lichanike, mwishowe anatokwa na damu nyingi na mara nyingi anapata tatizo na ukiangalia katika vifo vya mama na mtoto kinachowaua zaidi ni hicho kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua,” anasema Dk Kaanan.

Mara nyingi, mtaalamu huyo anasema waliokeketwa hukwepa hospitali, hivyo asilimia 48 kati yao hujifungulia majumbani na kwa waganga wa kienyeji kwani wenye mila hizo wengi hawataki kujihusisha na hospitali.

https://datawrapper.dwcdn.net/tKLrD/2/

Dk Kaanan alisema ukeketaji wa aina hiyo pia humletea athari mwanamke wakati wa tendo la ndoa, “kinachotolewa pale ni kitu kinachomgusa mwanamke kupenda tendo, hivyo humchukua muda mrefu ikilinganishwa na kama hakuondolewa nyama yote au kutokeketwa kabisa.”

Pamoja na jitihada za kutokomeza vitendo hivyo, bado kuna mikoa mitano inayoongoza kwa ukeketaji nchini ikiongozwa na Manyara wenye asilimia 58 ukifuatiwa na Dodoma(47), Arusha(41), Mara(32)na Singida yenye asilimia 31.

Hii ina maana kuwa kila wanawake 10 waliopo mkoani Manyara, sita wamekeketwa jambo linalorudisha nyuma mapambano ya kuzuia vifo vya akina mama na watoto.

Hata hivyo, utafiti huo uliofanywa na NBS na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto unaonyeha kuna mikoa yenye idadi ndogo ya wanawake waliokeketwa ikiwemo ya Ruvuma, Kagera, Rukwa na yote iliyopo Zanzibar ambayo ina kiwango cha chini ya asilimia moja.

https://datawrapper.dwcdn.net/3vlJ6/4/

Meneja Takwimu za Jamii kutoka NBS, Sylivia Meku anasema kiwango cha ukeketaji kinaongezeka kulingana na umri, ambapo asilimia 19 ya wanawake wenye miaka 45-49 wamekeketwa ikilinganishwa na asilimia 5 kwa wanawake wenye miaka 15 mpaka 19.

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema matokeo ya utafiti huo, yanaisaidia serikali ya awamu ya tano na wadau wa masuala ya afya kujipanga na kuangalia namna ya kupambana na vifo vitokanavyo na uzazi.


Anasema ukeketaji ni moja ya vitu ambavyo serikali inapiga marufuku kwa kuwa unarudisha nyuma juhudi za kupambana na vifo vitokanavyo na uzazi.

“Tayari tumeandaa Mpango Mkakati Mmoja wa Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto na Vijana wa mwaka 2016 –  2020 ambapo tumedhamiri kupunguzu vifo vitokanavyo na uzazi kutoka 432 hadi 292 katika kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2020, tutafikia na kuvuka lengo ikiwa ukeketaji utakoma,” alisema Mwalimu.

 

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania