Watumiaji wa simu benki waongezeka Tanzania

Nuzulack Dausen
February 28, 2017

[email protected]

Dar es Salaam. Idadi ya watumiaji wa huduma za kifedha kwa kutumia simu za mkononi imepaa kwa akaunti zaidi ya 400,000 ndani ya mwaka mmoja  jambo linaloonyesha mwenendo chanya wa sekta hiyo.

Mbali na kuongezeka kwa watumiaji hao, ushindani umeendelea kupaa baina ya kampuni kubwa za huduma za simu za mkononi huku Vodacom ikipoteza asilimia tatu ya wateja wake.

Ripoti  mpya ya mawasiliano iliyotolewa hivi karibuni na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imebainisha kuwa akaunti hizo ziliongezeka hadi milioni 18 mwaka jana kutoka milioni 17.6 ilivyokuwa Desemba, 2015.

https://datawrapper.dwcdn.net/jZSET/4/

Ongezeko hilo linakuja baada ya idadi ya watumiaji hao kuporomoka kwa kasi katika robo ya mwisho ya mwaka juzi kiasi cha kutia wasiwasi juu ya mustakabali wa huduma hiyo inayokua kwa kasi nchini kutokana na mabadiliko ya teknolojia.

Uchambuzi wa kitakwimu uliofanywa na MwananchiData unaonyesha kuwa Oktoba, 2015 Tanzania ilikuwa na akaunti za simu benki milioni 19.98 lakini  iliporomoka kwa watumiaji zaidi ya milioni 2.34 mwezi uliofutia.

Kampuni ya Vodacom inaongoza kuwa na akaunti nyingi za simu benki kupitia M-pesa baada ya kuweka kibindoni watumiaji takriban milioni 7.5 ikifuatiwa na Tigo-pesa yenye watumiaji milioni 6.1. Kampuni hizo mbili kwa pamoja zina robo tatu ya watumiaji wa huduma hizo za kifedha nchini.

Hadi Desemba, 2016 kulikuwa na kampuni za simu za mkononi tano zilizokuwa zikitoa huduma za kifedha ambazo ni Tigo Pesa, M-Pesa, Airtel Money na Halo Pesa iliyoingia sokoni mwaka jana. Hata hivyo, TCRA haikuijumuisha Halo Pesa katika ripoti yake hiyo.

Pamoja na kwamba inaongoza kwa watumiaji wengi wa M-Pesa, Vodacom ilipoteza asilimia tatu ya wateja wake kutoka akaunti milioni 7.96 mwaka 2015 hadi milioni 7.48 mwaka jana.

Tofauti na mshindani wake mkuu, Tigo yenyewe iliongeza kibindoni wateja takiban milioni moja ndani ya mwaka mmoja na kuifanya iwe na asilimia 34 ya watumiaji wote wa huduma hizo.

https://datawrapper.dwcdn.net/jZSET/2/

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania