Siri ya wanawake kuchemka riadha

Nuzulack Dausen
April 23, 2017

*Ni wanawake 23 tu walioshiriki mashindano ya kimataifa kwa miaka 20 kati ya wanariadha 130

Imani Makongoro, Mwananchi

[email protected]

Singida. Wakati  Kamati ya Olimpiki Afrika (ANOCA) ikijizatiti kuhakikisha ifikapo 2030 ushiriki wa wanawake katika michezo unakuwa sawa na wanaume kwa asilimia 100, kwenye riadha katika kipindi cha miaka 20 ushiriki wa wanawake umekuwa kuwa mdogo kuliko wanaume.

Mwenendo huo, iwapo utaendelea bila kupatiwa ufumbuzi wa haraka huenda ukawatupa wanawake katika ushiriki wa mchezo huo nchini jambo litakalokatisha ndoto za wasichana wengi wanamichezo.

Takwimu za Shirikisho la riadha la Ulimwengu (IAAF) tangu 1997 zinaonyesha wanariadha 130 waliiwakilisha nchi kimataifa kwenye mbio za dunia, michezo ya Afrika, Jumuiya ya Madola, Olimpiki, Mbio za Nyika za Dunia na mbio za dunia za nusu marathoni.

Hata hivyo, kati ya wanariadha hao, wanariadha wanawake ni 23 pekee sawa na asilimia 18 ya washiriki wote huku Restituta Joseph akishiriki mbio nyingi zaidi kwa wanawake ndani ya miaka 20 iliyopita akiwa kwenye timu ya Taifa.

Restituta ameiwakilisha nchi mara nne ndani ya miaka saba kwenye mbio za nyika za dunia kuanzia mwaka 1998 hadi 2001, michezo ya Olimpiki mara mbili ya 2000 na 2004, mbio za dunia mwaka 1999, Hispania na mbio za nusu marathoni za London za 2001. Pia ni mshindi wa medali ya fedha wa mbio za Afrika  za majeshi  za 2002.

Tausi Juma ni ‘binti’ anayekamata nafasi ya pili kwa kuiwakilisha nchi katika mbio nyingi ndani ya miaka 20 akiwa amebeba bendera ya Taifa kwenye mbio za nyika za dunia mara tatu tangu 2001 mpaka 2003 na kushiriki mbio za dunia za nusu marathoni za mwaka 2001.

Wanadada wengine wanaopamba orodha ya wanawake 20 wa riadha ni Zakia Mrisho na Banuelia Katesigwa ambao kila mmoja ameiwakilisha nchi mara tatu akiwa na kikosi cha taifa katika kipindi cha miaka 20.

Zakia ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kupitia Olimpiani amekimbia mbio za Olimpiki za 2012 nchini England, mbio za dunia za 2011 nchini Korea Kusini na mbio za Jumuiya ya Madola za 2010 nchini India akiwa mkimbiaji wa mita 3000 na 5,000.

Wakati Banuelia  ambaye ndiye mwanariadha pekee wa kike anayetokea Kagera kuitwa kwenye kikosi cha Taifa tangu 1997, yeye ameiwakilisha nchi kwenye mbio za nyika ya dunia mwaka kuanzia 2001 hadi 2003.

Wanariadha wengine waliolibeba taifa katika kipindi cha miaka 20 na aina ya mbio walizokimbia kwenye mabano ni Sarah Ramadhan (Olimpiki 2016 Brazil na mbio za nyika za dunia 2017), Catheline Lange (madola 2014, Scotland) na Hawa Hussein (mbio za nyika za dunia za 1998 na 2001).

Wengine ni Jackline Sakilu aliyeshiriki madola 2014 na mbio za nyika za dunia 2017 zilizomalizika wiki iliyopita Kampala nchini Uganda, Magreth Iro (mbio za nyika za dunia 2001 na 2002), Monica Samila (Mbio za nyika za dunia 2001), Mery Naali (Madola 2010, India),  Neema Tuluway (mbio za nyika za dunia 1997) na Rukia Mkanda aliyekimbia mbio za nyika za dunia mwaka 2003.

Magdalena Shauri, Angelina Tsere, Failuna Abdi, Siata Kalinga, Cecilia Ginoka, Maicelina Issa, Asha Salum, Noela Remy, Elizabeth Boniface na Amina Mgoo  ambao wameiwakilisha nchi kwenye mbio za nyika za dunia mwaka huu huku wengine wakishiriki kwa mara ya kwanza.

Kati ya wanawake hao, ni wawili pekee walioweza kurudi na medali.

 

Walipowanariadha hao hivi sasa

 Takriban nusu ya wanawake hao mashujaa wa riadha nchini wameshatundika daruga.

Restituta ni mwajiriwa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) alistaafu kukimbia tangu mwaka 2006, anaishi Arusha na mumewe, Restitua vilevile ni kocha wa riadha nchini.

Tausi na Magreth ni waajiriwa wa JWTZ pia wamestaafu riadha pamoja na Banuelia, Zakia, Hawa, Monica Samila, Neema Tuluway na Rukia Mkanda.

Catheline Lange yuko Arusha, bado anakimbia lakini pia ni mwajiriwa wa jeshi la Magereza ambaye anaeleza kikwazo kikubwa cha wanawake kushiriki kwa asilimia chache katika riadha kuwa ni ubinafsi na kutopewa nafasi.

Catherine anasema riadha ilichukuliwa kama mchezo wa wanaume, hata kwenye mashindano ya kutafuta viwango, kina dada walitumia juhudi zao binafsi tofauti na wanaume waliokuwa wakipewa fursa.

“Lakini pia tulikatishwa tamaa katika uteuzi wa timu kwa sababu wanaume walipewa kipaumbele zaidi.

“Mfano, kwenye mbio za nyika za 2016 tuliambiwa wanawake sita tuliofanya vizuri tutakwenda kushiriki mbio za dunia, tulijiandaa lakini mwishoni walikwenda wanaume peke yao sisi tukaachwa, bora mwaka huu kidogo uwiano umekuwepo,” anasema Lange.

Kwanini wanawake hawakupewa nafasi?

Uchambuzi wa data uliofanywa na Mwananchi umebaini kuwa katika kipindi chote cha miaka 20, hakukuwa na uwiano mzuri baina ya wanaume na wanawake katika uwakilishi katika timu za Taifa zilizoshiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Licha ya kuwepo kwa ajenda 50 kwa 50 inayotaka uwakilishi wa wanawake uwe sawa kwenye masuala tofauti ya siasa, michezo, elimu, afya na mingineyo, katika riadha wanariadha wakike ni asilimia 18 pekee waliobeba bendera ya Taifa kuiwakilisha nchi katika riadha.

Idadi hiyo imekuwa ikiwaumiza vichwa viongozi mbalimbali wa michezo.

Mjumbe wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Irene Mwasanga anataja mila na desturi za Kiafrika kuwa zimechangia kuwanyima fursa wanawake kushiriki katika michezo ikiwamo riadha.

“Mila na Desturi zilitutenga wanawake na michezo, familia nyingi ziliamini mtoto wa kike kushiriki michezo anakwenda kufanya mambo yasiyofaa, hakukuwa na makocha wa kike katika nchi nyingi za Afrika,” anasema Mwasanga ambaye pia ni ni Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake ya TOC na ile ya Afrika (ANOCA).

“Mwaka 2014, tuliandaa kongamano la wanawake michezoni, lengo lilikuwa kujadili ni namna gani tutaweka uwiano sawa baina ya wanawake na wanaume michezoni.

Katika kongamano hilo lililohusisha viongozi wanawake wa kamati za Olimpiki walishiriki kutoka katika nchi 11, Mwasanga anasema waliangalia fursa ya mtoto wa kike michezoni kwa kuweka maadhimio kuwa kufikia 2030, kuwepo na uwiano sawa na wanaume katika ushiriki wa michezo kuanzia ngazi ya uchezaji hadi uongozi.

“Mfano kwenye riadha,  hakuna kocha wa mchezo huo wa kike mwenye sifa za kuambatana na timu kwenye mashindano ya kimataifa, tumejijengea imani kwamba makocha ni wanaume, mzazi pia anaweka ugumu  kumruhusu binti yake kuambatana na kocha wa kiume, lakini pia kuna makocha kumpa nafasi mtoto wa kike ni nadra, wanaoangaliwa zaidi ni wanaume pekee,” anasema.

Ukiacha na mfumo dume, baadhi ya wanawake wamekuwa wakishindwa kutumia fursa zilizopo kutoka na hofu.

Mkurugenzi wa  ufundi wa Shirikisho la riadha Tanzania (RT), Dk Hamad Ndee anasema , vijana wa kike kwa kipindi kirefu walikuwa waoga kutumia fursa huku mazingira waliyokulia yakiwatenga na ushiriki wa michezo.

“Angalau kwa sasa mwamko upo, lakini hakuna kizazi kipya ambao watakuwa mbadala ya wanariadha ambao sasa ndiyo wanaelekea ukingoni. Wanariadha kama Sarah Ramadhan, Magreth Iro, Mery Naali, Zakia Mrisho na Jackline Sakilu ndiyo wanaelekea ukingoni, swali ni je nani atakuwa mbadala wao baada ya kizazi hiki kupita,” Mkurugenzi wa  ufundi wa Shirikisho la riadha Tanzania (RT), Dk Hamad Ndee.

Kuna wasiwasi kuwa wanariadha wanaokimbia huenda kikawa kizazi cha mwisho kwa wanawake katika riadha ya Tanzania kutokana na mwamko uliopo wa ushirikishwaji wa wanawake kwenye michezo ikiwamo riadha.

Bingwa wa zamani wa Taifa wa mbio fupi upande wa wanawake, Mwinga Mwanjala pamoja na kuwa na wasiwasi huo, anaomba iwepo kampeni ya asilimia 50 kwa 50 ifikapo 2030 inayopaswa kupewa msukumo wa hali ya juu.

“Hata mimi wakati nakimbia (miaka ya 1980) nilipitia changamoto ikiwamo wazazi kunikatilia hivyo sishangai kuona wanariadha 23 pekee wa kike kuiwakilisha nchi katika kipindi cha miaka 20,” anasema.

Hata wakati baadhi ya wasichana wakiendelea kujificha na kutotumia vyema fursa zilizopo kwenye mchezo huo, Singida na Manyara kwa kiasi flani wameanza kuelewa maana ya riadha hasa kupitia mafanikio waliyowahi kupata aidha baba zao miaka ya nyuma.

Wazazi wamekuwa pia chachu ya kufanikisha mabinti zao kuingia kwenye riadha katika mikoa hiyo.

Maria Seliwari ambaye ni mama wa mwanariadha kinda, Elizabeth anasema nafasi ya mtoto wa kike miaka ya 1980 mpaka miaka ya 2000 ilikuwa finyu lakini mafanikio ya baadhi ya wanariadha hao na wengine kupata ajira za kudumu yamefungua fursa kwa wengine.

“Kwa sasa wanariadha wa kike wapo na yote hiyo ni kutokana na mafanikio ya waliotangulia ambao wengi wao wamepata ajira katika Taasisi za majeshi, naamini mtoto wangu atafikia huko,” anasema.

Pamoja na RT kuongozwa na viongozi mbalimbali bado ushiriki wa wanawake katika riadha umekuwa finyu.

Hata hivyo, uongozi uliopo unaeleza kuwa utatua tatizo hilo.

Rais wa riadha, Anthony Mtaka anasisitiza katika utawala wake wa miaka minne atahakikisha kunakuwa na uwiano sawa baina ya mwanariadha wa kike na wa kiume katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

“Mkakati huo utaenda sambamba na kupewa fursa sawa ya kushiriki mashindano ya viwango ili kufuzu Olimpiki, Jumuiya ya madola na kushiriki mbio za dunia,” anasema Mtaka.

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania