Namna Serikali inavyoweza kuongeza viwanda vya bidhaa za mifugo

Nuzulack Dausen
May 9, 2017

Tabora. Kasi ya kuongezeka kwa idadi ya mifugo nchini huenda isilete tija katika ukuzaji wa viwanda vya bidhaa za rasilimali hiyo iwapo uwekezaji kwenye miundombinu na utoaji elimu kwa wafugaji havitafanyika siku za karibuni.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inakadiria kuwa hadi Oktoba 2015 kulikuwa na ng’ombe 25.8 milioni, mbuzi 19 milioni, kondoo 5.5 milioni na nguruwe wapatao 1.7 milioni.

Pamoja na kiwango hicho cha mifugo, uchambuzi wa takwimu nyingine za viwanda kutoka NBS za mwaka 2015 unaonyesha bado kuna idadi ndogo ya viwanda vya ngozi, maziwa na nyama ambavyo vingesaidia kuongeza thamani ya rasilimali hizo.

Hata mikoa inayoongoza kwa idadi ya ng’ombe kama Tabora, Manyara, Mwanza, Mara na Shinyanga haina viwanda vikubwa ikilinganishwa na Arusha uliopo nje ya orodha ya mikoa mitano bora.

Mikoa inayoongoza kwa idadi ya ng’ombe ni Tabora, Manyara, Mwanza, Mara na Shinyanga.

Kitendo cha mifugo kutosaidia zaidi ukuaji wa uchumi kinaelezwa na wataalamu kuwa kinasababishwa na uwekezaji mdogo unaofanywa na Serikali na wafugaji.

Mhadhiri wa Ufugaji katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), Dk Daniel Mushi anasema tatizo ni sera na utekelezaji wake jambo linalosababisha kukosekana kwa viwanda vikubwa vya mazao ya mifugo nchini.

“Lazima Serikali iwekeze kwenye kuongeza uzalishaji sio kwenye wingi tu, bali pia ubora. Uwekezaji kwenye sekta ya mifugo bado ni mdogo mno. Awali kulikuwa na ruzuku nyingi ya mifugo kwa ajili ya majosho na dawa ili ng’ombe wasiwe na magonjwa, lakini sasa zimeondolewa. Inabidi zirudishwe,” anasema Dk Mushi.

Anatoa mfano wa Ethiopia yenye sera zinazokataza uingizwaji wa bidhaa za mazao ya mifugo kama maziwa, nyama na za ngozi.

“Hapa kwetu japo sera zinazuia, lakini hakuna usimamizi kiasi kwamba viwanda vyetu vinakufa,” anasema Dk Mushi.

Anasema kitaalamu mnyama anatakiwa kuchinjwa akiwa na miaka miwili hadi miwili na nusu, lakini kwa Tanzania huchinjwa akiwa na miaka minne hadi saba.

“Hali hii tunapaswa kuiboresha kwa kuwa huwezi kuwekeza kiwanda kama huna uhakika na upatikanaji wa malighafi,” anasema mtalaamu huyo.

Mbali na kulegalega kwa utekelezaji wa sera ya Taifa ya ufugaji, wafugaji wameshindwa kutumia mbinu za kisasa kufuga ili kuongeza ubora wa wanyama ambao wangesaidia kuzalisha malighafi za kutosha kwa viwanda.

Tabora inafanyaje?

Mkoa wa Tabora pamoja na kuongoza kwa mifugo mingi nchini, sehemu kubwa inafugwa kienyeji.

Ripoti ya Kilimo ya mwaka 2014/15 iliyotolewa na NBS inaonyesha mkoa huo hadi Oktoba 2015 ulikadiriwa kuwa na ng’ombe 2.74 milioni. Hata hivyo, uongozi wa mkoa unakadiria kwa sasa kuwapo kwa ng’ombe 2.4 milioni kiasi ambacho ni pungufu kidogo na kile cha NBS.

Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Tabora, Philip Mtiba anasema ufugaji wa kienyeji badala ya kibiashara unarudisha nyuma jitihada za kuanzisha kiwanda cha nyama, maziwa na ngozi. “Aina ya ng’ombe tulionao ni Zebu na Ankole ambao ni wafupi na maumbile madogo,” anasema. “Kwa hiyo kama ni kutoa nyama, inakadiriwa ng’ombe mmoja ana uzito wa kilo 250, lakini anaweza kutoa nyama (edible meat) kilo 138 kiasi ambacho ni kidogo kuwezesha kujenga kiwanda cha kusindika nyama.”

Kuhusu maziwa, anasema theluthi mbili ya ng’ombe waliopo ni majike ambayo kati ya asilimia 35 hadi 40 hukamuliwa na hukadiriwa kutoa lita 1.8 milioni za maziwa kwa siku tena wakati wa masika. “Wakati wa kiangazi utoaji wa maziwa hushuka hadi lita 400,000 kwa siku, kumbuka hii ni jumla ya wilaya zote saba za Mkoa wa Tabora. Uzalishaji huu hauvutii wawekezaji wa viwanda kufanya biashara,” anasema Mtiba.

Mbali na kukosa kiwanda kikubwa cha mazao ya mifugo, Mtiba anasema mkoa una machinjio moja yenye uwezo wa kuchinja ng’ombe 50 kwa siku.

Habari inayohusiana: Faida za unenepeshaji wa ng’ombe wa nyama

Matatizo, uvamizi wa mifugo

Ili kukabiliana na changamoto hiyo, uongozi wa mkoa kupitia Mradi wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) ulipeleka madume ya mbegu aina ya Borani kutoka Kituo cha Utafiti wa Mifugo cha Mabuki Mwanza. Pia, walipeleka mbegu za kupandikiza kwa njia ya chupa kutoka Kituo cha Mifugo Usa River kilichopo mjini Arusha.

“Hata hivyo, madume yale hayakutunzwa vizuri, mengi yalikufa kwa ugonjwa wa Ndigana kali. Dume moja lina uzito wa kilo 900 na linapaswa kulishwa chakula cha kutosha, zikiwamo pumba na mashudu. Kwa hiyo hata ulishaji haukuwa mzuri, hivyo matokeo hayakuwa mazuri,” anasema Mtiba.

Mbaya zaidi, anasema mbegu kutoka Arusha zilikosa kemikali ya Nitrogen ya kutosha kuhifadhia hivyo zikafa na mpango wa kuboresha mbegu za ng’ombe ukashindikana na kuwarudisha palepale.

Mbali na uzalishaji huo mdogo, anasema asilimia 54 ya ng’ombe hao ni wavamizi kwenye maeneo ya misitu ya hifadhi na wameingizwa na wahamiaji kutoka mikoa jirani ya Mwanza, Simiyu, Mwanza na Geita.

“Uwezo wa mkoa kufuga ni ng’ombe 1.1 milioni tu, kwa sababu asilimia 74 ya eneo lote ni misitu ya hifadhi. Ardhi iliyobaki ni kwa ajili ya kilimo, mifugo na makazi,” anasema.

Habari inayohusiana:

Wafugaji waua na kujeruhi Morogoro

Mapigano ya wakulima, wafugaji yajeruhi wanne Bagamoyo

Wawekezaji wanasemaje?

Uwapo wa mifugo mingi ungetarajiwa kuzalisha ngozi nyingi za kutosha viwandani, lakini uhalisia ni tofauti. Wawekezaji wanasema ubora hafifu wa ngozi unafanya zinazozalishwa zisitosheleze mahitaji.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha Ngozi cha SAK International cha Arusha, Tauseef Mahmood anasema kuna uhaba mkubwa wa ngozi kiasi cha kuwafanya kuzunguka mikoa mbalimbali kuzisaka ili angalau kutimiza mahitaji. “Hatutegemei mkoa mmoja kupata ngozi kwa ajili ya kiwanda, tunanunua Tabora, Dodoma, Singida na mikoa mingine, ilimradi tupate za kutosha. Lakini soko siyo zuri mbaya zaidi Serikali imeweka kodi,” anasema Mahmood.

Hata hivyo, kwa kutumia fursa zilizopo, anasema wana mpango wa kuanzisha kiwanda cha viatu vya shule maana soko hilo lipo.

Ukilinganishwa na mikoa mingine, Arusha hadi Desemba 2015 ulikuwa na viwanda vinne vya nyama kati ya vitano vilivyokuwapo nchini na kuna ari ya wawekezaji kupanua biashara zao.

Meneja wa machinjio ya kisasa Arusha Meat, Fabian Kisinga anasema mpango uliopo ni kujenga kiwanda kikubwa cha kusindika nyama mkoani humo.

Mbali na mpango wa ujenzi wa kiwanda hicho kitakachogharamiwa na fedha za mkopo wa Sh3.5 bilioni, anasema kwa sasa wana mashine za kutengenezea soseji, kusaga nyama na kuikata kwa vipimo maalumu kwa mafunzo kabla ya kuiuza.

Mkoa wa Arusha kwa mujibu wa NBS unashika nafasi ya 10 kwa idadi ya ng’ombe nchini na kabla ya kutenganishwa na Manyara ulikuwa ukishika nafasi ya pili kwa wingi wa wanyama hao.

Awali mkoa huo ulikuwa na kiwanda cha nyama cha Tanganyika Packers kilichopo Moshono wilayani Arusha, lakini kilifungwa baada ya kampuni hiyo kufungwa mwaka 1993.

Hata hivyo, ubora wa nyama inayopatikana Arusha siyo bahati mbaya. Kuna mfumo imara wa kukagua ng’ombe kabla ya kumchinja jambo linalowafanya baadhi ya wafugaji kuzingatia taratibu za ufugaji ili kuzuia hasara.

“Sisi hatuna ng’ombe, ila wafugaji huleta tunawachinjia na kulipa ada ya Sh14,100. Ng’ombe huletwa na kuwekwa kwenye zizi na hukaa kwa saa 24 bila kula majani bali maji,” anasema Kisinga ambaye machinjio yake huchinja wastani wa ng’ombe 130 kwa siku. “Hapo hukaguliwa magonjwa na wataalamu na anayebainika kuathirika hutengwa na kama ni ugonjwa wa hatari kama kimeta, huchomwa moto na eneo alilokuwapo kupigwa dawa.”

Ng’ombe walio salama, anasema huingizwa mmoja baada ya mwingine kwenye machinjio na kabla hawajachinjwa hupigwa ganzi kwa bunduki maalumu jambo linalozuia damu kusambaa kwenye nyama hivyo kuifanya kuwa bora zaidi.

Mkoa wa Mwanza ulishaona ufugaji wa kienyeji hauwezi kusaidia kuongeza ufanisi katika sekta hiyo.

Ili kutoka kwenye hali ya sasa, mkoa huo umefanya jitihada za kuzalisha ng’ombe wenye sifa ya kutoa maziwa mengi na nyama ya kutosha.

Ofisa Mifugo wa Shamba la Mabuki, Issa Ali ameliambia gazeti hili kuwa kwa sasa wanazalisha mitamba chotara iliyochanganywa kati ya Borani na Friesian ili kupata mbegu inayotoa maziwa mengi na inayohimili magonjwa na ukame.

“Tunauza mitamba hii kwa wanavijiji na wateja wengine kwa Sh900,000 kila mmoja. Ngombe huyo ana uwezo wa kutoa lita nane hadi 10 kwa siku,” anasema Ali.

Mbali na mitamba hiyo, Ali anasema wanauza madume bora ya mbegu kwa Sh600,000 na mbuzi wa maziwa kwa Sh120,000.

“Tunazalisha pia mbegu za majani kwa Sh15,000 kwa kilo moja. Hawa ng’ombe wanahitaji kuwa na chakula cha kutosha hivyo ni lazima mfugaji awe na shamba la majani,” anasema.

Kauli ya Serikali

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo, Dk Mary Mashingo anakiri wafugaji kutofuga kibiashara jambo linalosababisha utendaji hafifu katika masoko na viwandani.

“Tumeona ufugaji wa kienyeji hauna tija. Tunatoa elimu kwa wafugaji na kwa sasa wameanza kufuga kibiashara kwa kunenepesha mifugo yao na kuuza kila mara,” anasema Dk Mashingo.

Anasema kuwa wanajipanga kuwashirikisha wadau ambao ni sekta binafsi wakiwamo wafugaji na mashirika ya hifadhi za jamii ili wajenge viwanda kwa kuwa malighafi ipo. “Mpaka sasa tuna viwanda 84 vya maziwa, 24 vya nyama na tisa vya ngozi,” anasema.

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania