Nuzulack Dausen May 12, 2017
Sharon Sauwa, Mwananchi; [email protected]
Dodoma. Kilio cha kutaka maji safi kilichosikika nchi nzima wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, kilijiwa kwa ahadi kemkem na jana kilipazwa na wabunge baada ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuomba Sh672.2 bilioni ambao zimeonekana kuwa ni ndogo.
Mjadala mkali uliibuka jana baada ya Waziri wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge kusoma hotuba ya bajeti kwa mwaka 2017/18 inayoonyesha Sh623.6 bilioni zimeelekezwa katika miradi ya maendeleo.
Miongoni mwa watu waliozungumza kwa hisia kali kupinga bajeti hiyo ni waliowahi kuwa mawaziri katika Serikali ya John Magufuli, Charles Kitwanga (Mambo ya Ndani) na Nape Nnauye (Habari, Michezo, Utamaduni na Sanaa).
Fedha hizo ni chini ya kiwango cha mwaka wa fedha unaoisha ambao wizara hiyo iliidhinishiwa na Bunge Sh939.6 bilioni na kati ya hizo Sh915.1 bilioni zilitengwa kwa ajili ya maendeleo.
Hata hivyo, hadi kufikia Machi mwaka huu ni Sh184.1 bilioni sawa na asilimia 19.8 tu ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge ndizo zilipelekwa wizarani.
“Rais John Magufuli alikuja bungeni na kuahidi kuwatua ndoo vichwani wakinamama, jambo ambalo ni tatizo kubwa,” alisema mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe.
“Na tumeona Makamu wa Rais Samia Suluhu akizunguka nchi nzima kufanya kazi hiyo. Hata bajeti ya mwaka jana picha iliyotumika ni ya Makamu wa Rais akimtua mama ndoo kichwani. Lakini kwa masikitiko makubwa sana bajeti ambayo inawahusu Watanzania moja kwa moja imeshuka kutoka Sh915 bilioni za maendeleo mpaka Sh623 bilioni.
“Unatafsiri vipi uwekezaji wa uwekaji raslimali fedha namna hii kwenye ajenda ya kuwaondolea kinamama ndoo kichwani. Nilikuwa nawaomba kwa siku tatu hizi za bajeti hii- najua tuna matatizo katika majimbo yetu na mikoa yetu tutaanza kuisema- iwapo hatutaungana kwa pamoja na kutaka bajeti ya wizara hii iongezwe angalau kwa kiwango cha mwaka jana, hayo malalamiko mtakayoyatoa ya majimbo yenu hayatakuwa na maana.”
Mbunge wa Misungwi (CCM), Charles Kitwanga alikwenda mbali zaidi na kutuhumu kuwa Serikali haipeleki maji kwenye vijiji vyake kwa sababu inamuandaa mtu aliyemtaja kwa jina la Bashite kugombea ubunge kwenye uchaguzi ujao.
Habari inayohusiana: Nape, Kitwanga wageuziwa kibao
Kitwanga alikuwa akifikisha kilio cha maji katika Kijiji cha Kolomijee wilayani Misungwi mkoani Mwanza ambako Bashite alizaliwa.
Kitwanga alisema kijiji cha Ihelele ambapo ndicho chanzo cha maji kimesahulika katika miradi ya maji iliyopangiwa bajeti.
“Sasa safari hii patachimbika. Na mimi sitatoa shilingi, nitakachofanya nitakwenda kumobilize (kuhamasisha) wananchi wa Misungwi kama 10,000 tukazime ule mtambo,” alisema.
Alisema hiyo ni kwa sababu tangu mwaka 2008 wanaendelea kusubiri na kwamba katika hotuba ya bajeti ya wizara hiyo wamethubutu kuandika katika Kijiji cha Nyangomango wamepata maji wakati hakina.
“Siwezi kukubali lazima ibadilike, kwa sababu hii nchi ni yetu wote. Ukiangalia huku pesa zimepelekwa sehemu ambazo siwezi kuzitaja na maji labda yapo. Ni vyema tukatendeana haki. Lakini inanipa shida zaidi hata mahali ambapo Rais aliahidi maji pale Usagala hakuna senti iliyowekwa humu,” alisema.
Video inayohusiana: Nape: CCM ikicheza na suala la maji haitarudi madarakani
Alisema huwezi kuwa na mradi wa maji ambao unakwenda Tabora unatumia Sh600 bilioni, halafu unashindwa kuwapa watu pale maji hata ya Sh10 bilioni.
“Very unfair (sio haki) nazungumza kutoka moyoni kwangu,” alisema.
Naye waziri wa zamani, Nape Nauye, ambaye ni mbunge wa Mtama (CCM), alisema mabadiliko yanayofanywa na Rais Magufuli hayatakuwa na manufaa kama huduma za jamii hazitaboreshwa na kushauri bajeti ya maji iongezwe.
Mbunge wa Same Mashariki (Chadema), Naghenjwa Kaboyoka alisema magonjwa mengi yakiwemo kuhara, kutapika na UTI yanatokana na ukosefu wa maji.
“Sasa tunataka bajeti ya afya iongezwe lakini magonjwa mengi yamekuwa yakitokana na ukosefu wa maji. Serikali iongeze bajeti hii,” alisema.
Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), Jasson Rweikiza alisema kupunguzwa kwa bajeti ya maji katika mwaka huu wa fedha hakukubaliki na kutaka iongezwe na kufikishwa kama ilivyokuwa bajeti iliyopita.
“Hata kama kuna shida ya fedha katika kuongeza bajeti hii, haikubaliki. Fedha hizo ziongezwe kwa ajili ya kuwezesha wananchi kupata maji. Ninashauri irudi palepale kama ilivyokuwa mwaka uliopita,” alisema.
Hoja ya kuongeza kiwango cha fedha katika bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji iliungwa mkono na wabunge wote waliopata nafasi ya kuchangia, akiwemo Mussa Mbarouk ( Tanga Mjini, CUF), Suleiman Bungara (Kilwa Kusini, CUF), Tunza Malapo (CUF) na Dk Mary Nagu (Hanang’-CCM).
Hoja zao hazikupishana sana na maoni ya Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji.
Akisoma maoni hayo, mjumbe wa kamati hiyo, Oliver Semuguruka alisema tathimini waliyoifanya imebaini kuwa fedha zinazoombwa hazikidhi mahitji makubwa ya maji.
Alisema mahitaji hayo kama ilivyoelezwa katika Mpango ya Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano umebainisha maji kama kipaumbele kimojawapo katika kukuza uchumi, hasa kwa kuchangia uzalishaji wa umeme, kilimo cha umwagiliaji, ufugaji, viwanda, usafirishaji na uchukuzi na kupunguza umasikini.
Habari inayohusiana: Serikali yaja na mkakati wa kukabiliana na changamoto ya uhaba wa maji
“Kamati imebaini pia kwamba imekuwa kawaida kwa Serikali kutenga kiasi kikubwa cha fedha za miradi ya maendeleo na kushindwa kuzitoa kama zilivyoidhinishwa,” alisema.
Oliver alisema kamati imebaini udhaifu mkubwa katika kutoa fedha za maendeleo zinazokuwa zimetengwa na Serikali na kuidhinishwa na Bunge kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za maji na umwagiliaji.
Kwa upande wake, msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Hamidu Bobali alisema takwimu za bajeti zinaonyesha kuongezeka kwa fedha, lakini haina maana kwamba fedha hizo zitatolewa kwa uwiano wa bajeti.
“Hivyo basi kambi rasmi ya upinzani bungeni inaitaka Serikali kuacha kupanga bajeti inayotoa matumaini lakini haina uhalisia katika utekelezaji wa miradi,” alisema Bobali.
Akisoma hotuba ya bajeti ya wizara yake bungeni jana, Waziri Lwenge alisema kutokana na hali ya upatikanaji mdogo wa fedha za bajeti, miradi mingi ya maendeleo imeshindwa kukamilika kwa wakati.
Alisema wao wabunge wanayo mamlaka ya kuitaka Serikali ikapange upya bajeti hiyo na kuongeza.
“Kama mbunge anaguswa na kero ya maji kwenye mkoa wake ama jimbo lake au kijiji chake ana njia moja tu ya kufanya, nayo ni kumsaidia waziri bajeti hiyo iandikwe upya,” alisema.
“Tuchague tupige kelele humu ndani tulalamike halafu tuonekane tumesemea watu wetu, ama tuchukue hatua bajeti ya maji irudishwe, iongezwe hata kiwango cha mwaka jana. Huko ndio mjadala wetu uende tuweze kuwatua wakinamama ndoo kichwani. alisema”
Nuzulack Dausen
Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.