Makato ya asilimia 15 yavunja historia ya makusanyo kwenye Bodi ya mikopo

Nuzulack Dausen
May 16, 2017

  • Marejesho yaliyokusanywa ndani ya miezi tisa ni zaidi ya yaliyokusanywa miaka mitatu iliyopita

Nuzulack Dausen na Kalunde Jamal, Mwananchi
[email protected]
Dar es Salaam. Vigogo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) huenda sasa wakapata usingizi baada ya fedha za marejesho ya mikopo kupaa zaidi ya mara mbili ndani ya miezi tisa, shukran kwa ongezeko la makato ya asilimia 15 na ukali wa Rais John Magufuli katika suala hilo.

Ongezeko hilo linakuja wakati wanufaikaji wa mikopo waliohitimu masomo yao miaka iliyopita wakiendelea kukabiliana na maumivu ya upungufu wa kipato baada ya Serikali kuongeza makato ya urejeshaji kutoka asilimia nane za awali hadi 15, Februari mwaka huu.

Novemba mwaka jana Bunge lilipitisha maboresho ya sheria iliyoanzisha HESLB sura namba 178 inayowataka waajiri sasa kuwakata kiwango hicho wafanyakazi wote walionufaika na mkopo huo kutoka kwenye mshahara ghafi.

Uchambuzi wa taarifa ya kifedha za HESLB ambayo Mwananchi imeipata unaonyesha kuwa hadi Machi 31 mwaka huu taasisi hiyo ilishakushanya Sh76.1 bilioni kiwango ambacho ni mara mbili ya Sh30.26 bilioni ilichokusanya katika mwaka wa fedha wa 2015/16. Hii ina maana fedha za marejesho zilizopatikana katika robo tatu za mwaka 2016/17 ni zaidi ya jumla ya zilizokusanywa kwa miaka mitatu mfululizo ya 2012/13 hadi 2014/15.

Licha ya ukweli kuwa marejesho ya mikopo yalikuwa yakipanda mwaka hadi mwaka kutoka mwaka 2012/13, kasi yake imepaa zaidi baada ya Rais John Magufuli kuingia madarakani ambaye amekuwa akisisitiza urejeshwaji wa mikopo hiyo ili isaidie wengine.

Awali urejeshaji mikopo hiyo ulikuwa ukiongezeka kwa wastani wa Sh4 bilioni kwa mwaka lakini uliimarika hadi Sh9 bilioni mwaka 2015/16 baada ya kufikisha marejesho ya Sh30.26 bilioni kutoka Sh21.67 bilioni zilizokusanywa mwaka 2014/15.

Taasisi yalalamikiwa
Kasi isiyoridhisha ya urejeshaji wa mikopo ilifanya taasisi hiyo kukabiliwa na malalamiko lukuki ya kiutendaji yakiwamo malalamiko ya kutoa mikopo kwa wanafunzi hewa na kusababisha vigogo wa juu wanne akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa zamani, George Nyatenga kung’olewa mapema mwaka jana.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Adul-razaq Badru alisema hivi karibuni kuwa fedha za marejesho zimeongezeka kwa kasi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuongeza ufanisi katika utendaji na utashi wa kisiasa uliopo katika Serikali ya Dk Magufuli.

“Ni wazi makato ya asilimia 15 tuliyoanza kukusanya Februari mwaka huu yamesaidia kwa kiasi kikubwa kurejesha fedha zilizokopeshwa kwa wanufaika.

“Pia, tumeongeza ukaguzi kwa waajiri kuhakikisha kila mnufaika anayeajiriwa anakatwa mkopo ili usaidie wengine wanaotaka kupata elimu hiyo,” alisema.

Badru alisema kwa sasa watumishi wa umma waliokopa mkopo huo wanakatwa moja kwa moja na Utumishi lakini wa sekta binafsi na waliojiajiri wanakatwa ipasavyo na wamerahisishiwa mfumo wa ulipaji kwa kutumia benki ili mchakato usiwakatishe tamaa.

HESLB yaweka rekodi sawa
Sanjari na kuimarisha ukusanyaji, HESLB imelazimika kusafisha takwimu zake za wanufaika baada ya kuwepo malalamiko lukuki juu ya baadhi ya watu waliozidishiwa deni ambalo hawakukopa au wengine kupangiwa marejesho kiduchu. “Zamani data hazikuwa safi lakini sasa tunarekebisha anayedaiwa kidogo ataambiwa kiwango sahihi na aliyewekewa kiwango kikubwa kimakosa atawekewa anachostahili. Hayo yamefanyika sanjari na kuwaondoa wakusanya madeni wa nje ambao hawakuwa na ufanisi katika kazi hii,” alieleza.

Pamoja na mabadiliko ya kimenejimenti, Badru alisema kuwa ushirikiano anaoupata kutoka kwa viongozi wa Serikali umewapa nguvu ya kukusanya marejesho na anatumaini kuwa kwa mwenendo huo wataanza kujitegemea kutoa mikopo badala ya kusubiri mgao kutoka serikalini ambao hubadilika kutokana na vipaumbele vya bajeti kila mwaka.

“Baadhi ya waliokopeshwa wanafikiri walipewa zawadi na wanaona uchungu kulipa bila kujali wanawakwamisha wengine waache ‘upuuzi’ walipe hizo fedha. Kuna watu wanakatwa kila mwezi Sh10,000 baada ya mtandao kukosea lakini hawatoi taarifa na wapo tayari wakatwe kiasi hicho kwenye mshahara wa Sh2 milioni.”
Stella Manyanya.

Makato hayo ya asilimia 15 yanayopingwa na baadhi ya wadau nchini, yamefanya bodi ikusanye marejesho ya Sh18.9 bilioni ndani ya mwezi mmoja pekee wa Machi, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi kuliko kilichokusanywa mwaka 2013/14 ambacho ni Sh18.1 bilioni.

Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (Tucta) ni miongoni mwa taasisi za awali zilizopinga uamuzi wa HESLB kuwakata wanufaika waliochukua mikopo hiyo kabla ya maboresho ya sheria hiyo mwaka jana likieleza kuwa hatua hiyo inawaumiza wafanyakazi.

“Kikubwa hapa si kwamba tunagomea kulipa makato ya asilimia 15 la hasha…tunapenda fedha za marejesho zisaidie wengine kama tulivyonufaika lakini kikubwa ni uwingi wa makato yaliyopo na huku mshahara ukiwa ni ule ule,” alisema Adinan Livamba mnufaikaji wa mkopo huo wa HESLB.

Livamba anayefundisha mkoani Tanga, alisema hali hiyo inasababisha watumishi wenye mshahara ghafi wa Sh716, 000 wabakiwe na kiasi kidogo kama walimu huku gharama za maisha zikiwa juu hivyo Serikali irudishe asilimia nane kwa wenye kipato cha chini huku wale wenye cha juu waendelee kukatwa asilimia 15.

“Wakipanda madaraja wanaweza kuwekwa katika kundi la kukatwa asilimia 15. Serikali ijaribu kuwa na masikio na huruma kwa vile kwa sasa inaonekana imekuja kuwakomoa baadhi ya watumishi kama walimu, kada ambayo haina posho wala marupurupu yoyote.

Tayari jambo hilo limepelekwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam. Mmoja wa walalamikaji wanaopinga makato hayo, Shukuru Mlwafu kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) amefungua kesi kuomba tafsiri ya kifungu cha 20 (1B) cha sheria ya HESLB kwa maelezo kuwa kinakiuka misingi ya katiba na kanuni.

Mawakili 20 waomba tafsiri ya sheria
Mwakilishi wa jopo la mawakili 20 wanaosimamia kesi hiyo, Dickson Matata aliwaambia wanahabari kuwa lengo si kupinga makato hayo bali wanaomba tafsiri ya sheria sababu baadhi wakati wanakopa sheria hiyo ilikuwa haijaanza kutumika hivyo walistahili kukatwa asilimia nane ya awali.

Uamuzi wa kufungua kesi hiyo ulikuja baada ya Rais Magufuli kusisitiza wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi kutetea kiwango hicho akieleza kuwa wote waliopata mikopo hiyo lazima walipe kwa kuwa hadi sasa ni Sh181.4 bilioni pekee zilizolipwa kati ya Sh424 bilioni zinazotakiwa kurejeshwa HESLB. Hata hivyo, si wanufaika wote wanapinga kiwango hicho cha makato.

Henry Rodrick mnufaika wa mkopo huo akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema, “watu walipe mikopo yao hata kwa asilimia 45 ya mishahara yao kama inawezekana ili tusaidie watoto wetu wasome kwa sababu awali makato hayo yalikuwa chini sana”.

Wataalamu wa masuala ya ugharamiaji elimu ya juu nchini walieleza kuwa ufanisi katika urejeshaji mikopo kama unaoendelea sasa ni njia pekee itakayoifanya HESLB iwahudumie watu wengi zaidi kuliko hapo awali.

Mhadhiri wa Shule ya Elimu ya UDSM, Dk Johnson Ishengoma alisema kwa sasa HESLB inaitegemea Serikali kwa takriban asilimia 90 hivyo jitihada zinavyofanywa na bodi kuongeza vyanzo vyake vya mapato ikiwemo kuimarisha urejeshaji mikopo ni hatua nzuri.

“Bado kuna matatizo ya uendeshaji ndani ya bodi ya mikopo ambayo yameanza kufanyiwa kazi. Bila kuondoa utegemezi serikalini bodi hiyo haiwezi kufanya kazi kwa ufanisi,” alisema Dk Ishengomba ambaye amefanya tafiti mbalimbali kuhusu ugharamiaji wa elimu ya juu nchini.

Serikali imesema marejesho hayo ya mikopo yameanza kusaidia kunufaisha baadhi ya wanafunzi ambao kwa bajeti ya kawaida huenda wangekosa mikopo.

“Tangu tumerekebisha sheria ya wanufaika wa mikopo kukatwa asilimia 15 kutoka nane ya awali tumeanza kuwapa wanafunzi wengi mikopo hata waliokosa mwaka jana, ”alisema Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya.

Waliopata mikopo wapungua
Hata hivyo, Mwananchi linafahamu kupitia takwimu za HESLB kuwa idadi ya waliopata mikopo kwa mwaka wa kwanza katika mwaka wa masomo inaendelea kushuka takriban mara mbili kutoka wanafunzi 54,072 mwaka 2015/16 hadi kufikia 28, 354 Machi 31 mwaka huu.

Manyanya alisema baadhi ya waliokopeshwa wanafikiri walipewa zawadi na wanaona uchungu kulipa bila kujali wanawakwamisha wengine hivyo waache ‘upuuzi’ wazilipe fedha hizo.

Alisema kuna watu wanakatwa kila mwezi Sh10,000 baada ya mtandao kukosea lakini hawatoi taarifa na wapo tayari wakatwe kiasi hicho kidogo cha fedha kwenye mshahara wa Sh2 milioni.

“Juzi nimekutana na mzalendo anayelipwa zaidi ya Sh2 milioni na alikuwa akikatwa Sh10,000 ameona ni upuuzi. Amekuja kutoa taarifa na amelipa mkopo wote hivyo kama kutakuwa na mwitikio wa aina hii inawezekana ukafika wakati wanafunzi wote wenye uhitaji wakapata mikopo, ”alisema Manyanya.

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania