Nuzulack Dausen May 24, 2017
- MSIMAMO WA SERIKALI: Serikali imesema ipo tayari kuwapa wawekezaji wengine upendeleo katika nishati iwapo wanahitaji.
Elias Msuya, Mwananchi; [email protected]
Je, Serikali ilimpendelea au haikumpendelea bilionea Aliko Dangote kumpa mgodi wa makaa ya mawe?
Hayo ni miongoni mwa maswali yaliyoibuka baada Rais John Magufuli kukipatia Kiwanda cha Dangote, kinachomilikiwa na bilionea huyo, mgodi wa makaa ya mawe mkoani Ruvuma ili kipate nishati ya uhakika ya kuzalisha saruji.
Machi 7, mwaka huu Rais Magufuli akiwa mkoani Mtwara wakati wa uzinduzi wa malori 580 ya kiwanda hicho, aliagiza Wizara ya Nishati na Madini kumpa tajiri huyo namba moja Afrika, mgodi wa makaa ya mawe kwa ajili ya kiwanda hicho.
Agizo hilo la Rais alilotaka litekelezwe ndani ya siku saba, lilikuja baada ya kiwanda hicho kusitisha uzalishaji kwa muda mwaka jana kwa madai ya kutopata nishati ya makaa na gesi za kutosha kuendeshea mitambo yake kiasi cha kuwafanya waagize kutoka Afrika Kusini ili kuziba pengo.
Habari inayohusiana: Magufuli, Dangote wapeana ahadi nane
Uamuzi huo umeleta hisia tofauti miongoni mwa wawekezaji wanaotumia nishati hiyo katika uzalishaji huku baadhi wakieleza uwepo wa dalili za upendeleo baada ya kukosekana usawa katika utoaji wa vivutio vya uwekezaji.
Baadhi wamekuwa wakiunga mkono uamuzi huo kwa maelezo kuwa kiwanda hicho kinatumia kiwango kikubwa cha makaa ya mawe kuzalisha nishati huku wengine wakipinga kuwa vipo vingine vyenye uhitaji unaofanana.
Dangote na makaa ya mawe
Pamoja na ukweli kuwa mgodi wa Tancoal uliopo Ngaka mkoani Ruvuma ulikuwa na matatizo ya ufanisi katika uzalishaji, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa hadi Rais anampatia Dangote mgodi huo alikuwa hajawahi kununua mzigo mkubwa wa makaa ya mawe kiasi cha kushindwa kuhudumiwa ndani ya nchi.
Uchambuzi wa takwimu za mauzo kutoka katika mgodi huo umebaini kuwa kampuni hiyo huomba oda kubwa ya kupatiwa makaa ya mawe zaidi ya wastani wa tani 17,000 kwa mwezi lakini katika utekelezaji huishia kuchukua wastani wa tani 6,000 pekee.
Kiwango hicho ni kidogo ikilinganishwa na kinachonunuliwa na kampuni za Tanga Cement na Lake Cement.
Takwimu za mgodi wa Tancoal Mines za mwaka 2016 zinaonyesha kuwa tangu Januari 2016 hadi Januari 2017, kiwanda cha Dangote kimenunua jumla ya tani 17,006 za makaa ya mawe ukilinganisha na kiwanda cha Lake Cement kilichoongoza kwa kununua tani 94,252 kwa kipindi hicho.
Tanga Cement ni cha pili kwa kuagiza tani 59,131 za makaa ya mawe katika mgodi huo huku kiwanda cha Cimerwa cha Rwanda kikiwa cha tatu kwa kuagiza tani 36,427. Dangote hakikuwamo kwenye tano bora.
Kitendo cha Dangote kupewa mgodi licha ya kutokuwapo kwenye orodha ya watumiaji wakubwa watano wa makaa ya mawe katika miezi ya hivi karibuni, kumewafanya wadau kuomba Serikali kuzingatia usawa katika utoaji wa vivutio vya uwekezaji.
Nadharia ya kwanza ilikuwa uamuzi huo ulikuwa sahihi kwa kuwa Dangote ana matumizi makubwa ya makaa ya mawe kuliko viwanda vingine.
Novemba 2014, kiwanda cha Dangote kiliomba leseni kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kujenga mtambo wa kuzalisha umeme wa MW75 kwa kutumia makaa ya mawe kwa ajili ya kuendeshea mitambo yake.
Mtambo huo utakaogharimu kiasi cha Sh1.1 trilioni na unatarajiwa kuzalisha tani 62 milioni kwa miezi 12 kuanzia mwaka huu.
Baadhi ya wawekezaji wa saruji wanahofu kuwa fursa hiyo aliyopewa Dangote huenda ikatengeneza ukiritimba katika soko la bidhaa hiyo muhimu katika sekta ya ujenzi nchini.
Menejimenti ya kiwanda cha Saruji Tanga (Tanga Cement) imeeleza kusikitishwa na upendeleo katika upatikanaji wa makaa ya mawe na gesi kwa wazalishaji wa saruji nchini.
“Kuna upendeleo unaofanywa kwa wazalishaji, kwa mfano kuwezeshwa kupata leseni ya kuchimba makaa ya mawe na gesi kwa ajili ya kuendeshea mitambo. Makubaliano tuliyowekeana kisheria na Serikali hayajapitishwa mpaka sasa,” alisema Meneja Mawasiliano wa kiwanda hicho, Mtanga Noor.
Alisema hata baadhi ya makubaliano waliyowekeana na Serikali ili kuongeza uboresha mazingira ya biashara hiyo hayajatekelezwa mbali ya tatizo la miundombinu linalokwaza upatikanaji wa makaa hayo ili kuhakikisha uzalishaji wa uhakika wa saruji.
Video inayohusiana:
“Tanga Cement inahitaji wastani wa tani 12,000 za makaa ya mawe kwa mwezi. Umeme na makaa kwa pamoja vinagharimu asilimia 70 ya uzalishaji,” alisema Noor.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Masoko wa Kiwanda cha Rhino Cement kilichopo Mkuranga Mkoa wa Pwani, Indra Pathak alisema wao hupata kiasi cha makaa wanachotaka.
“Kiwanda chetu kinatumia wastani wa tani nane hadi 10 za makaa ya mawe kwa mwezi, kinatosha kwa uzalishaji wetu.
“Tunao mtambo wa kuzalisha umeme MW10 kwa kutumia makaa hayo unaotosha kwa uzalishaji,” alisema Pathak ambaye kiwanda chake kiliongoza kununua makaa ya mawe nchini mwaka jana.
Meneja wa Mgodi wa Ngaka, David Kamenya alikiri kuwa awali walishindwa kutimiza mahitaji kwa wateja wote lakini pamoja na upungufu huo hawajawahi kushindwa kumhudumia Dangote.
“Ni kweli Dangote huwa anaweka ‘order’ kubwa ya tani 17,000 hadi 20,000 lakini akija kununua hajawahi kuzidisha tani 6,000. Kwa mfano, wiki hii (Mei 2-9, 2017), hakuna foleni mgodini, lakini bado hatuoni akichukua mzigo mkubwa kama anavyoomba,” alisema Kamenya.
Kamenya alisema ni kweli uzalishaji wao ulikuwa chini ya mahitaji kwa kuwa walikuwa wakizalisha tani 30,000 kwa mwezi na sasa wamefikia 40,000.
“Sasa hivi ndiyo tuko mwishoni ili kuweza kuzalisha tani 60,000 kwa mwezi na tutaongeza zaidi kwa kuwa lengo letu ni kuzalisha kati ya tani 80,000 hadi tani 100, 000,” alisema.
Alisema kwa sasa kinachofanywa ni kuongeza vifaa vya kuchimbia ili kuendana na kasi ya mahitaji.
“Mpaka sasa tumeshajipanga na tumeagiza baadhi ya vifaa. Lengo letu ni kuangalia mahitaji ya wateja wetu si wale wa Tanzania tu, bali hata wa Kenya na nchi nyinginezo,” alisema.
Udhaifu katika uzalishaji wa makaa ya mawe ndiyo uliofanya Serikali kuamua kumpatia Dangote mgodi ili aweze kuzalisha mwenyewe nishati hiyo.
Kwa sasa Tancoal inaeleza kuwa kampuni ya Effco Solution Tanzania Ltd yenye mitambo ya kuchimbia makaa ya mawe imeongeza kasi ya uchimbaji.
Ili kuongeza ufanisi, Tancoal wameipa zabuni kampuni ya Caspian ya kuongeza mitambo ya kuchimbia.
“Kwa mashine ambazo tumeagiza tungeweza kukidhi mahitaji yote ya Dangote. Ila Rais wetu ameangalia kwa mapana ili saruji izalishwe kwa wingi kwa sababu bado kuna nyumba nyingi za udongo huko vijijini zinazoweza kujengwa iwapo bidhaa hiyo itakuwa bei rahisi.
“Ni kweli Dangote akishaanza kuchimba atapungua kwenye wateja wetu, lakini kwa kuwa agizo limeshatoka hatuwezi kupinga,” alisema Kamenya.
Juhudi za kuutafuta uongozi wa Dangote Cement kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa. Licha ya kutumiwa maswali kwa barua pepe, hayakujibiwa hata baada ya kufuatilia kwa zaidi ya mwezi na msemaji wa kampuni hiyo kuthibitisha kuyapokea.
Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya biashara na uwekezaji wanasema uamuzi wa Serikali kumpa Dangote mgodi ni wa kisheria, kisera na unategemea nguvu ya mwekezaji katika kushawishi kupewa upendeleo wa kiuwekezaji.
“Mtu kupewa upendeleo katika uwekezaji si kitu kibaya. Kila mtu anapokwenda kujadiliana na Serikali anatumia ushawishi. Ni ufundi wa kuongea tu.
“Mtu anapata upendeleo kutokana na mkataba wake na Serikali na nafikiri Dangote alikuwa na wataalamu wazuri wa kushawishi Serikali wakati wa kujadili mkataba,” alisema Hussein Kamote, aliyekuwa Mkurugenzi wa Sera na Ushawishi wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI).
Mbali na uwezo wa kushawishi, Kamote ambaye ni mchumi kitaaluma, alisema Dangote pia amesaidia eneo la kijiografia la Mtwara na Lindi ambako kulionekana kuwa nyuma kimaendeleo kuliko mikoa mingine.
“Dangote alikuwa anaagiza makaa ya mawe kutoka Afrika Kusini wakati hapa Tanzania yapo, kwa hiyo ili kumwezesha kupata kwa wingi ndiyo wanampa upendeleo. Hao wengine wasilalamike tu kwa sababu walikuwapo, warudi kujadiliana na Serikali,” alisema Profesa wa Uchumi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Humphrey Moshi.
Kuhusu iwapo uamuzi wa Dangote kupewa mgodi utaleta ukiritimba, Profesa Moshi alisema kampuni hizo zinapaswa kushindana kwa kuzalisha saruji bora itakayouzika sokoni na kwa bei nafuu.
“Kabla ya Dangote, bei ya saruji ilikuwa juu lakini sasa imeshushwa kwa sababu wazalishaji wameongezeka. Inawezekana kampuni hizo zilikuwa zinapata faida kwa asilimia 100, lakini sasa faida yao imepungua ila kwa sababu ya umuhimu wa saruji katika uchumi inabidi bei ishuke,” alisema Profesa Moshi.
Mbali na makaa ya mawe, Kiwanda cha Dangote kimepewa pia upendeleo wa bei ya gesi kulingana na Sheria ya Fedha ya mwaka 2014.
Taarifa ya bei elekezi ya gesi asilia ya Mamlaka ya Udhibiti Maji na Nishati, (Ewura) ya Desemba 20, 2016 kwa uwekezaji wa mkakati, inaitaja Dangote kuwa moja ya viwanda vinavyopata upendeleo wa nishati kwani ni miongoni mwa wawekezaji wa kimkakati.
Ewura inaeleza kuwa uchumi wa Tanzania unatarajiwa kukua kwa asilimia saba kwa miaka mitano ijayo, ukiungwa mkono na sekta za uzalishaji, madini na utalii hivyo kusababisha mahitaji makubwa ya saruji.
“Uzalishaji bora unalengwa kwa Dangote Cement Tanzania ambayo inalenga kuongeza maradufu uzalishaji kufikia tani milioni sita ifikapo mwaka 2019 katika kuimarisha sekta ya ujenzi,” inasema.
Taarifa ya Ewura pia inataja viwanda vya mbolea vinavyotarajiwa kujengwa katika mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa miongoni mwa miradi ya uwekezaji wa mkakati.
Sheria inasemaje?
Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997, kifungu cha 2(2) inasema, biashara itakayopata upendeleo na ulinzi wa kisheria ni pamoja ile inayomilikiwa na mwekezaji wa nje au kwa ubia, mtaji wa chini usiwe chini ya Sh au karibu sawa na Dola 500,000, au inayomilikiwa na wazawa na mtaji wa chini usiwe chini ya Dola 100,000.
Kwa mujibu wa jarida la Forbes uwekezaji wa kiwanda hicho ni zaidi ya Dola 500 milioni (zaidi ya Sh1 trilioni) na hutumia wastani wa Dola 4 milioni sawa na Sh8.7 bilioni kwa mwezi kwa ajili ya mafuta ya dizeli.
Barabara bado tatizo Ngaka
Licha ya Tancoal kuongeza uzalishaji wa kutosheleza wateja wakubwa kama Dangote, bado mgodi huo unakabiliwa na changamoto ya ubovu wa barabara inayotoka eneo la Kitai hadi Ngaka umbali wa zaidi ya kilometa 70.
Barabara hiyo ni nyembamba na sehemu kubwa ina mashimo kiasi cha kutokuwa rafiki wa malori makubwa yanayoingia katika mgodi huo ulioanzishwa mwaka 2008.
Kutokana na ubovu wa barabara hiyo, madereva wanalazimika kupunguza mwendo jambo linalopunguza ufanisi wa muda katika usafirishaji wa nishati hiyo.
Ili kupunguza maumivu kwa wanunuzi wa nishati hiyo, kabla ya kufika Ngaka, Tancoal imeweka kituo cha mauzo ya makaa ya mawe cha Makolo kilichopo kilomita 20 kutoka barabara kuu ya Songea.
Wanunuzi kwa sasa hawalazimiki tena kufika hadi mgodini, badala yake makaa hayo husafirishwa na malori yaliyokodiwa na Tancoal umbali wa kilomita 54 kutoka mgodini hadi Makolo.
Barabara kutoka Makolo hadi mgodini ni mbovu hasa wakati huu wa mvua hali inayosababisha ucheleweshwaji wa makaa kwa wateja.
Nuzulack Dausen
Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.