Misukosuko ya karafuu yapunguza mabilioni ya mauzo ya nje Zanzibar

Nuzulack Dausen
July 4, 2017

[email protected]

Dar es Salaam. Misukosuko inayoikabili karafuu katika uzalishaji na bei katika soko la Dunia ni miongoni mwa sababu zilizofanya thamani ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi kushuka kwa kasi Zanzibar jambo linalopunguza mapato ya fedha za kigeni na kutishia mustakabali wa wakulima.

Ripoti (Kiingereza) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya mwaka ulioishia Aprili mwaka huu inaonyesha kuwa thamani ya mauzo ya nje ya bidhaa visiwani humo yalishuka kwa asilimia 54.4 kutokana na kushuka kwa uuzaji bidhaa nje ya nchi hususan karafuu. Karafuu ni moja ya mazao makuu ya biashara Zanzibar ikifuatiwa na mwani na nazi.

Ripoti hiyo ya tathmini ya uchumi kwa mwezi iliyotolewa mwezi Mei  inabainisha kuwa mauzo ya karafuu kwa mwaka ulioishia Aprili yalishuka zaidi ya mara mbili ikilinganishwa na mwaka jana yakichagizwa na kushuka kwa kiwango cha uuzaji na kuporomoka kwa bei katika soko la Dunia.

Unaweza kusoma zaidi: Kuna siri kubwa katika biashara ya karafuu

“Thamani ya mauzo ya karafuu nje ya nchi yalikuwa Dola za Marekani 17 milioni (Sh37.4 bilioni) ikilinganishwa na Dola 45.7 milioni (Sh100.54 bilioni) katika kipindi kama hicho mwaka 2016,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo ya BoT.

“Kushuka huko kwa thamani ya mauzo kulitokana na kuporomoka kwa bei ya karafuu kutoka Dola 8,064 (Sh17.74 milioni) kwa tani hadi Dola 7,750 (Sh17 milioni) kwa tani”.

Kuendelea kushuka kwa bei ya karafuu katika soko la dunia ni pigo kwa wakulima wa Zanzibar ambao sehemu kubwa ya kipato chao hutegemea mauzo ya zao hilo ambalo sehemu kubwa hutumika dawa zikiwemo za meno na kurahisisha mmeng’enyo wa chakula.

Mbali na kushuka kwa bei ya karafuu, thamani ya mauzo nje ya nchi visiwani humo kwa ujumla yalishuka hadi Dola 178.4 milioni (Sh392.5 bilioni) kwa mwaka ulioishia Aprili mwaka huu kutoka Dola 197.6 milioni (Sh434.7 bilioni) ndani ya kipindi kama hicho mwaka jana.

Wakati sekta ya bidhaa ikifanya vibaya katika uuzaji wa bidhaa nje, sekta ya utalii yenyewe imezidi kung’aa baada ya kuendelea kuingiza mabilioni ya shilingi zaidi ya yaliyoingizwa mwaka jana.

Kwa mujibu wa Issa Hassan Shoka, mtafiti wa kilimo nchini,  sekta za utalii na biashara zinakua kwa kasi kiasi cha kuizidi karafuu katika uingizaji fedha za kigeni kinyume na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Katika utafiti alioufanya mwaka 2015 kwa ajili ya kuhitimu shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Shoka anasema mwenendo wa kushuka kwa bei ya karafuu ulianza kuonekana tangu mwaka 2011.

Hata wakati Zanzibar ikikabiliwa na changamoto za uzalishaji wa karafuu, kasi ya ukuaji wa sekta ya utalii inasaidia kufukia mwanya huo wa kuongeza mapato ya fedha za kigeni.

 

 

 

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania