Nuzulack Dausen July 27, 2017
Aurea Simtowe,Mwananchi
Rooney* ni miongoni mwa wanafunzi wachache waliobahatika kusoma shule za msingi za umma maarufu nchini. Kila asubuhi ya siku za wiki huamka na kuanza safari ya kwenda kutimiza ndoto za kielimu katika Shule ya Msingi Bunge jijini Dar es Salaam.
Wazazi wanaamini mtoto wao anasoma shule yenye mazingira mazuri ikizingatiwa ipo mita 200 tu kutoka Ikulu. Watoto wenzie anaokaa nao Tabata Kisukuru wanamuonea wivu kusoma katika shule hiyo ya ghorofa iliyopo katikati ya jiji.
Kitu ambacho wengi hawajui ni kwamba Rooney, anayesoma darasa la sita shuleni hapo, huitaji kupanga foleni kwa zaidi ya dakika tatu kwenda msalani kujisaidia kutokana na uhaba wa matundu ya vyoo.
“Najivunia tu kusoma Bunge lakini huko chooni siyo kuzuri,” anasema.
“Kuna wakati hapa baadhi yetu hubanwa na kushindwa kujizuia hivyo hulazimika kujisaidia nje ya choo au kuingia wawili choo kimoja na kila mtu kugeukia upande wake.”
Rooney (siyo jina lake kamili) anasema kuna wakati mtu unaweza shindwa kuingia chooni kutokana na maji machafu kutapakaa kila kona na wakati mwingine chemba iliyopo chooni inakua na maji machafu ya kijani kutokana na kutofanyiwa usafi kwa muda mrefu.
Licha ya kuwa vyoo hivyo husafishwa na moja ya wahudumu, Rooney anasema; “mtu mwenyewe anaesafisha vyoo mara nyingi amekuwa akisafisha vya walimu na kuacha vya wanafunzi.”
Foleni anayopanga Rooney wakati wa kwenda msalaani siyo ya bahati mbaya. Shule hiyo ni miongoni mwa zenye uhaba mkubwa wa vyoo nchini ikiwa na wanafunzi 2,155 wanaotumia matundu saba tu yanayofanya kazi kwa sasa.
Kati ya hayo, matundu matano ni kwa ajili ya wasichana huku wavulana zaidi ya 1,000 wakipambana katika mawili yaliyosalia jambo linalopoteza muda wa masomo na kuhatarisha afya zao.
Hii ina maana kuwa tundu moja la choo linatumiwa na wastani wa watoto 307 kinyume na utaratibu wa tundu moja kwa wavulana 25 na kwa wasichana 20.
Kilomita saba kutoka shule anayosoma Rooney, ipo shule ya Msingi Buguruni iliyopo kwenye eneo linalofahamika kukaliwa na watu wenye kipato cha chini.
Katika shule hiyo ya Buguruni anayosoma Omar Suleiman Omar, hali ni tofauti kidogo.
Tofauti na Bunge, Buguruni ina matundu 40 ya vyoo huku wanafunzi wakiwa 1,477 tu.
Hapa Buguruni tundu moja linatumika na wastani wa watoto 36 ikiwa ni ahueni takriban mara tisa ya wale wa Bunge licha ya kuwa bado kiwango hicho kipo juu kidogo ya utaratibu unaotakiwa.
“Ni mara chache sana kukuta foleni chooni kwetu,” anasema Omar.
“Matundu ya vyoo yapo na tunajitahidi kuyafanyia usafi kila siku kuendana na ratiba iliyowekwa tukisimamiwa na mwalimu wa zamu.”
Uhaba wa vyoo unaikabili Bunge angalau kidogo siyo miujiza kwa kuwa mkoa wa Dar es Salaam ni miongoni mwa yenye uhaba mkubwa wa vyoo katika shule za msingi za umma nchini ikishika nafasi ya pili baada ya Geita kwa mujibu wa Takwimu za msingi za elimu mwaka 2016.
Mikoa ya Kilimanjaro na Iringa Pekee ndio mikoa inayoonekana kuwa na afadhali katika idadi ya matundu ya choo huku kiwango cha watumiaji ikikikaribia kile kilichowekwa na Serikali yaani tundu moja la choo kutumiwa na wasichana 20 na 25 kwa wavulana.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Bunge, Radhia Mfalingundi anasema ukosefu wa matundu ya vyoo kwa wavulana ndiyo jambo kubwa analopambana nalo kwa sasa kwa kuwa tundu moja hulazimika kutumiwa na zaidi ya wanafunzi 400 ikiwa ni mara 16 zaidi ya kiwango kilichowekwa na Serikali.
“Matundu mengine matatu yapo lakini kwa sababu miundombinu ni ya tangu 1957 inahitaji kufanyiwa marekebisho na mpaka sasa kuna kampuni ambayo ililetwa ili kuangalia ni jinsi gani wanaweza kuyatengeneza matundu hayo ili yaweze kutumiwa na wavulana,” anasema Radhia.
Pamoja na kuwa wasichana nao wanakabiliwa na uhaba wa huduma hiyo, anasema angalau wao kwa kuwa wana matundu matano japo wapo zaidi ya 1,000.
“Hata Mkurugenzi wa Manispaa (Ilala) anatambua adha hiyo na amewahi kutuma watu ili waweze kuangalia ni jinsi gani watatatua tatizo hili,” anaeleza.
Vyoo vyote katika shule hiyo ya ghorofa mbili vimejengwa katika orofa ya chini na kwa mujibu wa Mwalimu Radhia ni vigumu kujenga vipya kutokana na ufinyu wa eneo na usanifu wa jengo husika.
Ndani ya vyoo hivyo, kuna mabomba yasiyotoa maji hivyo wanafunzi hulazimika kuchota katika bomba zilizofungwa karibu na vyoo. Maji machafu yaliyoshindwa kuingia shimoni yametapakaa hadi mlangoni na kuwafanya wanafunzi wanaoingia kuyakanyaga.
Buguruni yenyewe pamoja na upungufu, Mwalimu Mkuu shule hiyo Ally Hassani anasema ina upungufu wa matundu 27 ya vyoo ili kuwa sawa na kiwango cha idadi wa wanafunzi wanaotakiwa kutumia tundu moja la choo.
Kama ilivyo kwa Bunge, Mwalimu Hassani anasema Serikali inafahamu upungufu wa matundu ya vyoo walionao kwa sababu kila mwisho wa mwezi huwa wanapeleka tathmini ya kuonyesha vitu vilivyopo na vitu vinavyohitajika.
“Hakuna hatua zozote zilizochukuliwa mpaka sasa lakini tumejitahidi kuomba ufadhili kutoka makampuni mbalimbali ambao ni wadau wa elimu lakini bado hatujajibiwa,” anasema Hassani.
Anasema upatikanaji wa maji katika vyoo ni wa uhakika kwani shuleni hapo kuna kisima ambacho maji yake yanapatikana muda wote.
Mwalimu Gaigije Kiberenge wa Shule ya msingi Buguruni anasema katika kunusuru hali za kiafya za watoto mwalimu wa zamu ni lazima ahakikishe usafi chooni unafanyika kila asubuhi kulingana na zamu ilivyopangwa.
“Tunazo sabuni tunazotumia kusafisha na kuna ndoo ambazo zimewekwa chooni kwa ajili ya kuwekea maji mtu anapohitaji kujisaidia anakuja kuchukua maji kisimani,” anasema Gaigije.
Pamoja na Mwalimu Gaigije kueleza kuwa wameweka maji kwa ajili ya wanafunzi kunawa wanapotoka kijisaidia lakini mwandishi wetu alizikuta ndoo zikiwa hazina maji jambo linalowafanya watoto watoke bila kunawa.
Mwalimu huyo anakiri kuwa suala la wanafunzi kunawa kila wanapotoka kujisaidia bado ni tatizo kwa sababu awali waliwekewa matanki madogo madogo wakayaharibu na baadae waliwekewa ndoo mbili ili wakitoka chooni waweze kunawa lakini hali ikawa sivyo ilivyotegemewa.
“Ndoo mbili haziwezi kutosha idadi ya watoto waliopo na badala yake hata sabuni tulizokuwa tumewawekea walikuwa wakizifinyanga finyanga na kuzitupa hovyo na ukiwa kama mwalimu huwezi kujua ni nani alietoka kujisaidia muda huo,”anasema Gaigije.
Maoni ya wazazi
Ni wazazi wachache wanafahamu masaibu wanayokumbana nayo shuleni katika kupata huduma za vyoo.
Jackson Peter anasema ni mara chache sana mzazi kuanza kuangalia shule ina matundu mangapi ya choo au vyoo vina hali gani na badala yake wazazi wengi huwa wanaangalia ufaulu wa shule upoje na walimu wake wanajituma kiasi gani katika ufundishaji.
“Mara nyingi mzazi akishajua mambo hayo anaridhika na kumuandikisha mtoto na kuondoka akiamini sehemu aliyofika ni salama,” anasema Peter anayefanya biashara katika soko la Kisutu jijini hapa.
Alipoulizwa iwapo anajua ni watoto wangapi wanatakiwa kutumia tundu moja, Peter anasema hatambui chochote ila anachofahamu kuwa ni hatari sana kama idadi kubwa ya wanafunzi watatumia tundu moja la choo.
Anasema Serikali ifanye jitihada za kuzinusuru shule zenye hali mbaya ya vyoo ili afya za watoto zisiwe hatarini.
Hata hivyo, baadhi ya wazazi wanaona kuilalamikia Serikali pekee yake katika kuboresha huduma za vyoo si jambo jema.
“Wazazi kwanini tusichangishane na kujenga vyoo vingi ili watoto wanapoenda mapumziko wasisubiriane kwenda msalani hili jambo linafanya baadhi yao kujisaidia pembeni,” anasema Yunus Mremi anayasema ana mtoto mmoja anayesoma shule ya msingi jijini hapa.
Mremi anasema mbali na wazazi kukagua hali ya vyoo, wakaguzi wanapopita katika shule wasiangalie madaftari na ufundishaji wa walimu bali wakague na hduuma kama vyoo kwa sababu afya ndio kitu cha msingi kuliko kitu chochote.
Anasema inawezekana pia walimu huwa wanahakikisha usafi nyakati za asubuhi tu lakini sio kila muda watapita kukagua.
Hatari kwa afya
Wataalamu wa afya wanasema kuna hatari kubwa kwa watoto kupata magonjwa ya maambukizi ya njia za mkojo iwapo vyoo vitakuwa vichafu kutokana na watoto kujisaidia hovyo kwa sababu ya uhaba.
“Kama choo ni kichafu muda mwingi kuna uwezekano wa kupata maambukizi ya magonjwa ya mara kwa mara hasa ya njia ya mkojo na fangasi kutokana na mpishano wa watu kuingia kujisaidia kabla hakujafanyiwa usafi baada ya mtu kutoka,” anasema Dk Katoto Nestory kutoka mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Anasema magonjwa mengi yanaweza kuenea kutokana na uchafuzi wa makopo yanayotumika lakini pia hata maji wanayotumia kunawa lazima yawe katika hali ya usafi.
Dk Sajjad Fazel, Mtaalamu wa Dawa na Tiba anaeleza zaidi kuwa maambukizi ya njia ya mkojo yasipotibiwa kwa haraka yanaweza kusababisha madhara kwani husambaa na kufika kwenye figo na kusababisha matatizo mengine.
“Watoto wapo katika hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi haya kutokana na kinga ya miili yao kuwa ndogo kuliko watu wazima,” anasema Dk Fazel.
Meneja wa Utafiti na uchambuzi wa Shirika la HakiElimu, Godfrey Bonaventure anasema tatizo hilo ni kubwa na mwaka huu walijaribu kulizungumzia ili Serikali iweze kuliweka katika bajeti kwa sababu kuna upungufu wa matundu ya vyoo karibu asilimia 50.
“Choo ni huduma muhimu na sio shuleni kwa watoto tu bali hata maofisini na ni huduma ambayo mtu asipoipata anaathirika kisaikologia,” anasema Bonaventure.
“Hivyo ni lazima kuhakikisha huduma hii inapatikana kwa watoto, vyoo viwe na mazingira mazuri na safi, matundu ya kutosha ili waweze kupata huduma kwa muda na choo kinapohudumia watu wachache kuna uwezekano mkubwa wa kufanyiwa usafi kila mara.
Takwimu za Best 2016 zinaeleza kuwa uwiano wa tundu la choo kwa wanafunzi nchini katika shule za msingi za umma ni mbaya.
“Tundu moja la choo linatumika na wastani wavulana 57 kinyume na kiwango cha wavulana 25. Pia tundu moja linatumika na wastani wa wasichana 56 kinyume na wasichana 20 kwa tundu,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Uwiano wa matumizi ya vyoo nchini kwa shule za umma na binafsi ni watoto 50 kwa tundu moja takwimu ambazo sio nzuri na inaweza kuleta athari kwa kuwa ni mara mbili zaidi ya kiwango kinachotakiwa.
Manispaa Ilala yazungumza
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Elizabeth Thomas anasema licha ya Serikali kutowatengea bajeti katika kukabiliana na baadhi ya changamoto zinazowakabili wametenga kiasi cha fedha kutoka katika makusanyo yao na wafadhili kuboresha huduma ya vyoo shuleni.
“Katika bajeti binafsi tumetenga Sh 2.2 bilioni ambayo pamoja na kutatua changamoto nyingine tutaongeza matundu 200 ya vyoo pia kupitia wafadhili tutaweza kujengewa matundu 80 ya vyoo,” anasema.
Wizara ya Nchi, ofisi ya Rais-Tamisemi inayohusika na kutoa fedha za miradi ya maendeleo katika shule za msingi nchini inasema kazi yake kubwa ni kutenga fedha zilizoombwa katika bajeti zilizopitishwa na halmashauri zote nchini kwa kuzingatia vipaumbele iliyojiwekea na siyo kuwaamulia cha kufanya.
“Kama wizara ni ngumu kuelewa kuwa mkoa una mahitaji kiasi gani lakini kupitia vipaumbele vyao tunaweza kufahamu na kuwapatia fedha ili waweze kutatua changamoto zinazowakabili,” anasema Msemaji wa Tamisemi, Rebbeca Kwandu.
Anasema mapendekezo yakikusanywa sehemu husika hutolewa fungu kwa kila halmashauri halafu mkoa husika ndio hupanga bajeti yake kutokana na vipaumbele iliyojiwekea.
Nuzulack Dausen
Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.