Vyakula, kuimarika kwa sarafu vyashusha mfumuko wa bei

Nuzulack Dausen
August 10, 2017

Dar/Zanzibar. Mfumuko wa bei kwa Julai umepungua hadi asilimia 5.2 kutoka 5.4, uliokuwapo Juni hali iliyochangiwa na kushuka kwa bei za vyakula.

Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim Kwesigabo alisema licha ya kupungua kwa bei ya vyakula,  kuimarika kwa sarafu ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani kumechangia. “Mfumuko wa bei kwa vyakula vya nyumbani na migahawa kwa Julai umepungua hadi asilimia 9.3 kutoka  9.8 Juni,” alisema.


Sh5,500: Bei ya kilo moja ya nyama inavyouzwa kwenye mabucha jijini Dar es Salaam.

Pia, Kwesigabo alisema thamani ya sarafu ya ya Tanzania imezidi kuimarika, uwezo wa Sh100  kununua bidhaa na huduma umefikia Sh91.87 kwa Julai ikilinganishwa na Sh91.66 ilivyokuwa Juni.

Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Takwimu wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Salama Saleh Ali alisema kushuka huko kutoka asilimia 5.4 hadi 4.1 kumechangiwa zaidi na kupatikana kwa wingi  bidhaa za kilimo.

(Imeandaliwa na Aurea Simtowe, Israel Mapunda na Haji Mtumwa)

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania