Jinamizi la talaka linavyotafuna ndoa za Watanzania

Nuzulack Dausen
August 21, 2017

*Kiwango cha talaka kimeongezeka mara mbili Tanzania ndani ya miaka sita kiasi cha kutishia mustakabali wa taasisi hiyo muhimu.

[email protected]

Ndoto za wanandoa wengi wanapooana huwa ni kuishi pamoja hadi kifo kinapowatenganisha. Vivyo hivyo, wazazi wao, ndugu na jamaa hupenda kushuhudia wanandoa hao wakifanikiwa katika safari ya maisha yao ikiwamo kuwa na familia imara yenye watoto wenye afya bora.

Hata hivyo, siyo wanandoa wote hutimiza ndoto hizo. Kasi ya wanandoa nchini kupeana talaka imeongezeka mara mbili ndani ya miaka sita ya hivi karibuni, jambo linalotishia mustakabali wa ‘taasisi’ hiyo muhimu kwa maisha ya binadamu.

Utafiti wa kufuatilia kaya Tanzania (National Panel Survey) wa mwaka 2014/15 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) unaonyesha kuwa kiwango cha talaka kimeongezeka kutoka asilimia 1.1 mwaka 2008/09 hadi asilimia 2.1 mwaka 2014/15.

Hii ina maana kuwa kwa sasa kila watu 100 wenye umri wa kuoa au kuolewa waliopo nchini, wawili wametalakiwa kutoka mmoja mwaka 2008/09. Ikumbukwe kuwa utafiti huo unabainisha kuwa watu takriban 40 kwa kila 100 wanaopaswa kuoa au kuolewa bado hawajaingia kwenye ndoa.

Mbali na talaka, kuna wanandoa takriban wanne kwa kila 100 ambao wametengana, jambo linaloashiria huenda nao wakatalikiana siku zijazo iwapo hawatapata suluhu ya kudumu ya tofauti zao.

Kuvunjika kwa ndoa hizo kunawaweka watoto katika maisha magumu ya kukosa mapenzi ya wazazi wote wawili na hata baadhi yao kujikuta wakiingia mitaani kuwa ombaomba kutokana na kukosa huduma stahiki za malezi.

Wataalamu wa masuala ya saikolojia, takwimu na walimu wa dini wanaonya kuwa mwenendo huu ni hatari kwa mustakabali wa Taifa ikizingatia kuwa ndoa ni moja ya taasisi muhimu za kujenga upendo, amani na mshikamano.

Takwimu zinavyoeleza

Matokeo ya utafiti huo uliochapishwa mwaka huu yanakwenda sanjari na yale ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 yaliyobainisha kuwa watu 715,447 walikuwa wametalikiwa (sawa na watu watatu kwa kila 100) wenye umri wa kuoa au kuolewa.

Mikoa ya Kusini Unguja, Mtwara, Mjini Magharibi, Lindi na Kaskazini Unguja inaongoza kwa kiwango cha talaka huku kiwango kikiwa zaidi ya asilimia nne ambacho ni juu ya wastani wa kitaifa wa asilimia tatu kwa takwimu za Sensa mwaka 2012.

Soma zaidi: Takwimu za ndoa kuvunjika zaongezeka

Siyo wote wanaotalakiana mahakamani hupeleka matamko ya talaka kwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) baada ya takwimu za wakala huo kuonyesha idadi ndogo ya talaka, lakini mwenendo wake unapaa kwa kasi.

Pamoja na kuwa talaka zilizosajiliwa ni chache, Rita inabainisha kuwa zinaongezeka mwaka hadi mwaka kwa kuwa Dar es Salaam pekee zimeongezeka kutoka 106 mwaka 2014 hadi 149 mwaka jana jambo linalosadifu hali halisi iliyotolewa na NBS.

Rita, WLAC zinasemaje?

“Inawezekana kabisa talaka ni nyingi kuliko takwimu zetu kwa kuwa wengi hawaji kusajili matamko ya talaka kutoka mahakamani ili tuwapatie vyeti,” anasema Meneja wa Masoko, Habari na Elimu kwa Umma wa Rita, Josephat Kimaro.

“Tumeanza mchakato wa kuwasiliana na mahakama ili baada ya kutoa tu matamko ya talaka watuletee takwimu zote ili tupate picha kamili.”

Taarifa za Rita zinaonyesha kuwa baadhi ya ndoa zimedumu muda mfupi chini ya mwaka mmoja ikiwamo iliyochukua miezi minane iliyojumuisha kipindi cha mashauriano, kuendesha kesi mahakamani hadi kusajili tamko la talaka Rita. Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inaeleza kuwa tamko la kutengana au talaka hutakiwa kutolewa na mahakama pekee baada ya kujiridhisha na sababu za wanandoa kufanya hivyo.

Kifungu cha 100 cha sheria hiyo kinaeleza kuwa mahakama haiwezi kusikiliza shauri la talaka kwa ndoa zenye umri chini ya miaka miwili na ili isikilize ni lazima ijiridhishe kuwa kuna mmoja wa wanandoa anateseka kupindukia.

Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC) kinaeleza katika kijitabu cha ufafanuzi kuhusu sheria ya ndoa kuwa, “mazoea ya wanandoa kupeana talaka mitaani aidha kwa maandishi au kwa mdomo, hizo si talaka kwa mujibu wa sheria ya ndoa.”

“Ni lazima talaka itolewe na mahakama ili kila haki ya mwanandoa itamkwe bayana,” inaeleza sehemu ya kitabu hicho ya WLAC kilichotolewa mwaka 2013.

Kauli za mwathirika

Mwananchi limebaini kuwa ukosefu wa uaminifu na kubadilika tabia baina ya wanandoa ni miongoni mwa sababu kuu zinazofanya wanandoa kutalikiana.

Esther (siyo jina lake halisi) alitalikiana na mumewe mwaka jana baada ya kubaini kuwa alikuwa amebadilika tabia ikilinganishwa na wakati wa uchumba.

Kasi ya wanandoa nchini kupeana talaka imeongezeka mara mbili ndani ya miaka sita ya hivi karibuni, jambo linalotishia mustakabali wa ‘taasisi’ hiyo muhimu kwa maisha ya binadamu.

“Zamani alikuwa ananishirikisha kwa kila jambo, msikivu, mpole na mfanyakazi aliyeonekana kuwa baba bora wa familia. Lakini baada ya kuoana alianza kuwa mkali hata kwa vitu vidogo licha ya kumwambia kwa upole,” anasema Esther.

Esther (37) anaeleza kuwa kabla ya kuachana na mumewe waliyeoana baada ya kufahamiana kwa miezi tisa, aliwashirikisha wazee wa karibu, familia zao hadi viongozi wa dini lakini bado mwanaume huyo ‘hakuambilika’ jambo lililosababisha waachane.

“Sikupenda tutalikiane kwa kuwa tuna mtoto mmoja, lakini vitimbi vyake vilifanya maisha yawe ya mateso wakati wote. Angalau kwa sasa napumua na nasikia ameshaoa mke mwingine huenda huyo ndiye aliyekuwa akimsumbua,” anasema.

Viongozi wa dini

Viongozi wa dini ambao hufungisha ndoa na kutatua matatizo yanayowakuta wanandoa wanasema haishangazi kuona talaka zikiongezeka kutokana na kushuka kwa maadili miongoni mwa wanandoa ikiwamo uwapo wa muda mfupi wa wachumba kufahamiana vyema. Mwenyekiti wa Halmashauri ya Baraza Kuu la Kiislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka anasema kuongezeka kwa talaka ni matokeo ya udhaifu katika taasisi ya ndoa ambayo wahusika wake wanatakiwa wadumu kwa upendo na umoja hadi kifo kinapowatenganisha.

“Kabla ya ndoa unatakiwa uone uliyempata kuwa ana vigezo vinavyotakiwa ikiwamo kujiridhisha tabia na familia yake, uwezo wa kijamii na kama anaweza kuwa mwanajamii,” anasema.

“Bahati mbaya ndoa nyingi kwa sasa ni matokeo ya kukurupuka. Unakuta mwanandoa hajui hata historia ya mwenzie kitu wanachoangalia ni ana mali kiasi gani au anafanya kazi shirika gani.”

Kuingia kwenye ndoa wakati wanandoa wakiwa ‘vipofu’ wa historia ya kila mmoja, kwa mujibu wa Sheikh Mataka kunafanya ndoa ianze kuyumba mara tabia halisi zitakapoanza kujitokeza na kusababisha watalikiane.

Mbali na kutojua historia, Padri wa Kanisa Katoliki, Festo Liheta wa Parokia ya Mtakatifu Kamili ya Kiwalani jijini Dar es Salaam anaongeza kuwa kuongezeka kwa uelewa wa haki za wanawake, kukua kwa kipato miongoni mwa wanandoa na matatizo ya unyumba yanachangia ongezeko la talaka.

Padri Liheta anasema kiutamaduni wanaume wanapenda kutawala, lakini kwa sasa wanawake wengi wanazijua haki zao na hawataki zivunjwe kinyume na wenza wao ambao hawajafikia katika uelewa huo. “Mambo ya kiuchumi yanachangia sana ndoa kuvunjika. Mtu anavyokuwa na uwezo wa kifedha hawezi kukubali kunyanyasika kwa kuwa anaweza kujitegemea tofauti na zamani ambapo akina mama walivumilia kutokana na kipato duni,” anasema Padre Liheta ambaye alifanya utafiti kuhusu kuvunjika kwa ndoa wakati akihitimu Shahada ya Uzamili.

Mbali na masuala ya kipato, padri huyo anasema matatizo ya tendo la ndoa nayo yanachochea ukosefu wa uaminifu hasa pale mmoja anaposhindwa kumridhisha mwenzake.

“Zamani tendo la ndoa lilikuwa kwa ajili ya kuzaa tu, lakini kwa sasa ni pleasure (starehe) hivyo mtu asiporidhika anaenda kutafuta nje. Hapa wanaume wanabidi wajitahidi kuwaridhisha wake zao ili kumaliza mifarakano inayotokana na unyumba,” anasema.

Akifafanua jambo hilo, Sheikh Mataka ambaye ni mwalimu wa dini ya Kiislamu anaeleza kisa cha hivi karibuni alichosuluhisha kilichomhusisha kijana mmoja aliyemkuta mkewe akifanya mawasiliano ya mara kwa mara na mwanaume aliyekuwa na uhusiano naye miaka ya nyuma.

“Pamoja na kumuonya hakusikia. Yule mwanaume anayewasiliana naye alimwambia kuwa ni mwanamke aliyekuwa anamfuata na siyo yeye,” anasimulia Sheikh Mataka akitafsiri kesi hiyo kama mfano wa wanandoa kukosa uaminifu.

NBS yatia neno

Talaka zinazoongezeka kwa kasi haziathiri tu wanandoa husika, bali familia nzima ikiwamo zile zilizozalisha wanandoa.

“Kuongezeka kwa talaka kunahatarisha kuongezeka kwa familia za mzazi mmoja,” anasema Mtakwimu Mwandamizi wa NBS, Abbasy Mlemba . “Watoto wanakosa haki ya kuishi na wazazi wote wawili na hili litaongeza umaskini kwa watoto na kuwafanya wawe ombaomba mitaani, watumikishwe kazi na kuongeza uhalifu na mimba za utotoni.”

Mwarobaini wa talaka

Ili kupunguza tatizo la mifarakano ya awali, Padri Liheta anawasihi wachumba kupeana muda wa kufahamiana vyema kabla ya ndoa ikiwamo kujua asili ya wenza hao, eneo anapotoka kila mmoja, ukoo na wazazi kufahamiana.

Sheikh Mataka anasema uchumi hauwezi kuwa sababu ya wanandoa kutalikiana hivyo watu wanaotaka kuoa au kuolewa wanatakiwa kujitathmini vyema na kuwa na upendo na dhamira ya kweli ya kuingia kwenye ndoa ikiwamo kuwa tayari kuhimili changamoto.

Serikali inasema kuwa inafahamu suala hilo na imeshaanza kutekeleza mikakati ya kulipunguza ili kutengeneza ustawi bora wa familia na Taifa.

Msemaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto upande wa maendeleo ya jamii, Erasto Ching’oro anasema wamebaini kuwa mbali na madhara kwa familia, pia ukosefu wa utulivu baina ya wanandoa unapunguza uzalishaji na kurudisha nyuma jitihada za kuelekea nchi ya uchumi wa kati.

“Serikali inataka watoto walelewe na wazazi wote wawili ili kuongeza usalama wao katika kila nyanja ya maisha yao. Hivyo kwenye mpango kazi miaka mitano tumepanga kupunguza kiwango cha talaka kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2021,” anasema Ching’oro.

Katika mpango huo ulioanza kutekelezwa Julai mwaka huu hadi mwaka 2021, Ching’oro anasema wanawashirikisha viongozi wa dini na kimila, asasi za kiraia na maofisa ustawi na maendeleo ya jamii katika utoaji elimu ya uhusiano na ndoa ili kupunguza talaka na ukatili wa wanawake na watoto.

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania