Nuzulack Dausen August 26, 2017
* Wataalamu wa afya wanasema unaweza kutokomezwa kwa kuzingatia usafi wa mazingira
Dar es Salaam. Japo hautajwi mara kwa mara kama Malaria na Ukimwi, ugonjwa wa kuhara ni miongoni mwa magonjwa yanayoendelea kuwatesa Watanzania kimya kimya jambo linalotishia mustakabali wa afya na nguvu kazi nchini.
Takwimu za mwaka 2014 kutoka kituo huru cha takwimu cha Serikali (opendata) zilizochapishwa kwenye tovuti ya Hurumap zinaonyesha kuwa ugonjwa wa kuhara ni miongoni mwa magonjwa matano makubwa ambayo wagonjwa wengi hubainika baada ya kupimwa.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, ugonjwa wa kuhara unawatesa watu wa rika zote–watoto wa chini ya miaka mitano na wale wenye miaka mitano na kuendelea.
Katika kundi la wagonjwa wa kulazwa, ugonjwa huo ni wa nne kwa watoto chini ya miaka mitano baada ya wagonjwa 10 kwa kila 100 waliopimwa kubainika wanaharisha.
Kwa wakubwa wenye miaka mitano na kuendelea waliolazwa, ugonjwa huo ulikuwa ni wa tano ukiwa nyuma ya Malaria, homa ya mapafu, Anaemia na ugonjwa wa maambukizi njia ya mkojo (UTI).
Hali hiyo ipo sanjari na kundi la wagonjwa wanaoenda hospitali na kutibiwa bila kulazwa. Katika kundi hilo la wasiolazwa wenye umri wa chini ya miaka mitano, ugonjwa wa kuhara mwaka 2014 ulikuwa ni wa pili wakati kwa wale wenye miaka mitano na kuendelea ukiwa wa tano.
Wataalamu wa masuala ya afya wanasema ugonjwa huo kwa sehemu kubwa unasababishwa na uchafu wa mazingira.
Daktari wa hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk Christopher Peterson anasema kuwa ugonjwa huo ni “muuaji wa kimyakimya” kwa kuwa unamaliza maji mwilini hivyo wananchi wajihadhari kwa kuzingatia mbinu za usafi katika mazingira yote wanayozunguka.
“Kuhara ni ugonjwa unaotokana na uelewa mdogo wa usafi. Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa asilimia 80 ya kinachosababisha ugonjwa huo ni uchafu uliopo katika mazingira yanayomzunguka mtu,” anasema Dk Peterson.
Ili kuondoa ugonjwa huo moja kwa moja, anasema ni vyema wananchi wakapatiwa elimu ya usafi katika uandaaji wa chakula, usafi wa vyoo, na namna ya kutibu maji ili kujiepusha na vimelea vya kuhara.
Anasema vimelea vya kuhalisha (Amoeba) hujizalisha kwenye vyakula vya baridi vyenye nyuzi joto sifuri hivyo ni bora kabla ya kula watu wakapasha vyakula vyao na kuosha matunda na mikono yao vyema baada ya kutoka msalani.
“Usipotibiwa vizuri ugonjwa wa kuhara ni hatari kwa sababu unamaliza maji mwilini ambayo ni muhimu kwa maisha ya mwanadamu na kusababisha kifo,” anasema.
Kwa mujibu wa takwimu za kituo hicho huru cha takwimu, mwaka 2013 ugonjwa wa kuhara ulikuwa ni wa sita kwa kuua watoto wengi chini ya miaka mitano nchini baada ya kuwepo vifo vitano kwa kila 100 vilivyosababishwa kwa magonjwa ya kuhara.
Wakati kwa watu wenye miaka mitano na zaidi, ugonjwa huo ulikuwa wa tisa kwa kuwa na vifo viwili kwa kila 10 mbele ya kisukari.
Serikali imesema inaendelea kuwapatia elimu wananchi namna ya kuishi kwa usafi ili kuepuka na magonjwa yote yakiwemo ya kuhara.
Msemaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Nsacris Mwamaja anasema kuwa Serikali ilishatoa miongozo kwa halmashauri namna ya kukabiliana na magonjwa ya kuhara kwa kutoa elimu za usafi wa mazingira.
“Kazi yetu ni kuhakikisha wananchi wanapata elimu stahiki ya afya. Kwa pamoja idara ya afya, wizara ya maji na umwagiliaji na taasisi nyingine za umma na asasi za kiraia tunashirikiana kuhakikisha wanachi wote wana vyoo, wanatibu maji kwa kuchemsha, wanaandaa chakula katika mazingira salama ili kupunguza magonjwa hayo,” anasema Mwamaja.
Video: Usafi ni muhimu kwa afya ya mwanadamu ili kuepuka magonjwa kama kipindupindu.
Nuzulack Dausen
Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.