Kuorodhesha kampuni za mawasiliano, madini kutakuza soko la hisa na mitaji

Maria Mtili
August 31, 2017

Julius Mganga, Mwananchi ; [email protected]

Kukiwa na zaidi ya watumiaji milioni 20 wa huduma za fedha na intaneti nchini, kampuni za mawasiliano zinapigana vikumbo kujiorodhesha Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE).

Wataalam wa masoko ya hisa na mitaji wanasema yapo maendeleo makubwa kwenye sekta hiyo na Tanzania ni miongoni mwao. Gazeti la Financial Times linaitaja Tanzania kama soko muhimu linalochipukia hasa baada ya Vodacom kuorodheshwa katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE). Vodacom ilikamilisha agizo la kuupa umma fursa ya kumiliki asilimia 25 ya hisa zake katikati ya mwezi huu.

Taasisi ya Morgan Stanley Capital International (MSCI) ambayo hutoa madaraja kwa maoko yanayochipukia (Frontier Markets au FMs), yanayokua (Emerging Markets au EMs) na makubwa huangalia mambo mengi kabla ya hivyo.

Mpaka sasa, bado Tanzania haina ushawishi mkubwa kwenye soko la kimataifa kutokana na kutokidhi viwango vya MSCI kwa sababu ya udogo wa mtaji wa soko ambao kabla ya usajili wa Vodacom ulikuwa Dola 4.6 bilioni za Marekani huku mauzo yakiwa ni chini ya Dola milioni moja (Sh2.2 trilioni) kwa siku zikichangiwa na benki pamoja na kampuni za vinywaji.

Pamoja na udogo wa mtaji na mauzo ya siku, usajili wa Vodacom utakaofuatiwa na kampuni nyingine za mawasiliano na za madini zinazotakiwa kuorodhesha asilimia 25 DSE, unaelezwa utalikuza soko la Tanzania zaidi ya mara mbili au tatu na kuongeza mvuto wake.

Hilo likifanyika, itajiweka sehemu nzuri kuwa miongoni mwa masoko yanayochipukia kwani itakuwa imekidhi vigezo vya MSCI.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Usimamizi wa Taaluma ya Benki (TIOB), Patrick Mususa anasema usajili wa Vodacom si umeongeza mtaji wa soko pekee bali hata ushiriki wa taasisi za fedha na hali ikiendelea hivyo benki nyingi zaidi zitashiriki kununua na kuuza bidhaa mbalimbali zinazopatikana DSE.

“Kadri kampuni zitakavyoongezeka ndivyo wawekezaji watakavyozihitaji zaidi hasa suala la uwazi wa taarifa za fedha,” anasema.

Anasema kukua kwa DSE kutaongeza mawakala mikoani na kuwapa fursa wananchi wa huko kushiriki kwenye soko hilo tofauti na sasa walivyojikita zaidi jijini Dar es Salaam pekee.

Mkurugenzi wa Shahada za juu wa Chuo cha Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory anasema uchache wa kampuni zilizoorodheshwa DSE haukuwa unatoa fursa kwa watafiti kulitathmini soko hilo.

“Baada ya serikali kuzilazimisha kampuni za mawasiliano na madini kujiorodhesha ni rahisi watafiti kufuatilia kwanini mwitikio umekuwa mdogo au masual amengine yanayohusiana na soko,” anasema.

Anasema changamoto nyingine ya kutafiti soko hilo ni uchache wa wabobezi wanaoweza kufanya hivyo. “Kuna wataalam wachache wa wanaoweza kutafiti soko la hisa nchini,” anasema Dk Pastory.

Meneja wa Fedha na Utafiti wa DSE, Ibrahim Mshindo anakiri kuwapo kwa changamoto ya upatikanaji wa taarifa hasa ndani kutokana na kutokuwa na wataalam wa kutosha hivyo kufanya ushiriki pia kuwa mdogo.

“Wawekezaji wengi wa soko ni wageni. Watafiti wengi ni kimataifa. Kuna uhaba wa watafiti wa ndani,” anasema na kufafanua kwamba tayari soko hilo linatekeleza mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa soko linalochipukia (FM) ifikapo mwaka 2020.

Simu

Wakati simu za mkononi zinaanza kutumika nchini mwanzoni mwa miaka ya 1990, wengi walikuwa wamezoea kutumia za mezani. Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) zinaonyesha mpaka mwaka 1995 kulikuwa na watumiaji 2,198 wa simu hizo zilizoanza kutumika duniani kote tangu mwaka 1983 baada ya kugunduliwa miaka 10 nyuma.

Mpaka mwaka 2005, idadi hiyo ilikuwa imeongezeka na kufika zaidi ya milioni 2.96 na hadi Juni, kulikuwa na watumiaji milioni 40.4.

Awali simu zilikuwa ni kwa ajili ya kupiga tu, tena ndani ya nchi lakini maendeleo ya teknolojia yakaruhusu kutuma ujumbe mfupi (SMS), baadaye kupiga nje ya nchi mpaka sasa miamala ya fedha na intaneti inayofanikisha taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Tangu mwaka 2002 zimu za kwanza zenye kamera zilipoanza kutumika duniani, kampuni za utengenezaji zimekuwa zikikabana koo kuhakikisha zinapata soko kubwa zaidi kwa akuongeza tochi za mwanga wa kawaida, kurekodi sauti na video huku zikitoa fursa ya vyombo vya habari hasa redio na televisheni kurusha taarifa zao moja kwa moja.

Ushindani haukuwa kwa watengenezaji pekee, hata kampuni za mawasiliano zilinyang’ana wateja waliokuwapo. Mpaka mwaka 2000, wakati Shirika la Simu (TTCL) lilipokuwa likiendelea kuongoza kwa wateja wengi wa simu za mezani, Tigo iliyokuwa na wateja 56,500 ilikuwa kinara kwa za mkononi ikifuatiwa na Vodacom 50,000 kisha Zantel 4,000.

Miaka saba baadaye, Vodacom ilikuwa inahudumia asilimia 50 ya wateja milioni 8.3 waliokuwapo ikifuatiwa na Celtel (Airtel ya sasa) kwa asilimia 28 na Tigo asilimia 12. Zantel ilikuwa na asilimia saba wakati TTCL ilipata asilimia mbili.

Waziri wa Fedha na Mipango, DK Philip Mpango (kulia akiwa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Ian Ferrao, katikati na Ofisa Mtendaji wa Soko la Hisa Dar es Salaam siku ya kuorodheshwa kwa Vodacon sokoni hapo. Picha ya Mtandao.

Baada ya kushindana kwa bei za kupiga na kutuma SMS kwa muda mrefu, hivi sasa Vodacom, Tigo na Airtel zina zaidi ya wateja milioni 10 kila mmoja huku ushindani ukihama kutoka maeneo hayo na kuelekezwa kwenye matumizi ya intaneti na huduma za fedha.

Intaneti

Kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya intaneti tangu utoaji wa leseni zilipoanz akutolewa mwaka 2005. Kwa sasa kuna kampuni 78 za uuzaji na usambazaji wa intaneti kutoka  68 zilizokuwa leseni mwaka 2010.

Kati ya kampuni hizo, 46 pekee zilikuwa zinatoa huduma husika wakati 20 hazikufahamika zilipo baada ya watafiti kutozikuta kwenye anuani zao za makazi na mbili zilikuwa hazifanyi kazi.

Kati ya 46 zilizokuwapo, 38 zilikuwa zinatoa huduma ya intaneti kwa wateja milioni 4.8 na zilizobaki zilijikita kwenye huduma nyingine kama vile sauti na SMS.

Licha ya kuongezeka kwa watumiaji, Manispaa ya Babati mkoani Manyara na Kampuni ya Jodeka zilishindw akutumia leseni zao kwa maelezo ya kushindwa kuhimili ushindani mkubwa uliokuwapo sokoni.

Wateja wengi wa intaneti mwaka huo zilikuwa ni kampuni na mashirika kwa asilimia 55 wakifuatiwa na watu binafsi asilimia 40 huku asilimia tano wakipata huduma hiyo kutoka kwenye internet café.

Mwanzoni, internet café ilikuwa biashara nzuri na utafiti uliofanywa na TCRA mwaka 2010 unasema zilikuwapo zaidi ya 300 jijini Dar es Salaam pekee na zaidi ya 20 huko Zanzibar zikitoa nafasi ya kuperuzi na kusoma baruapepe hata kupiga simu ya mtandao (VoiP). Vijana, wafanyabiashara, wafanyakazi na wasomi wanaelezwa ndiyo walikuwa wateja wakubwa na biashara hii.

Matumizi ya intaneti yanaelezwa kuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wa taifa. Utafiti wa Internet World Stat mwaka 2010 ulieleza ongezeko la asilimia moja ya watumiaji wa huduma hizo hupandisha usafirishaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kwa asilimia 4.3 hata kwa nchi zinazoendelea.

Kukiwa na zaidi ya watumiaji milioni 19.86 milioni wa intaneti mpaka mwaka jana wakiwa wameongezeka kutoka milioni 17.26, kasi ya kuenea kwa matumizi yake ni asilimia 40 kwa mwaka.

Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael anasema kasi ndogo ya matumizi ya intaneti kwa nchi nyingi zinazoendelea ni gharama kubwa ya vifaa vya mawasiliano hasa simu za kisasa za mkononi (smartphones).

“Jumuiya za kimataifa zinaangalia namna ya kupunguza bei walau simu hizo ziwe zinauzwa kwa Dola 30 za Marekani (zaidi ya Sh66,000). Tigo tunajitahidi kuleta za bei ndogo kadri iwezekanvyo,” anasema Woinde.

Huduma za fedha

Wakati ripoti ya mwaka jana ya GSM ijulikanayo kama ‘The Mobile Economy-Africa’ ikionyesha asilimia 46 ya Waafrika wote ambao ni zaidi ya watu nusu bilioni, taarifa za TCRA zinaonyesha mpaka Juni, zaidi ya Watanzania milioni 20.29 wanatumia huduma hizo.

Watuamiaji wa huduma za fedha ni takribani nusu ya laini milioni 45.52 zilizosajiliwa huku Vodacom, Tigo na Airtel zikichuana kugombea wateja waliopo sokoni. Wakati Vodacom ikihudumia nusu ya wateja wote, Tigo inafanya hivyo kwa wateja wawili katika kila 10 na Airtel ina wafikia asilimia 15 hivyo kufanya jumla ya asilimia 84 ya soko zima.

Ripoti ya wananchi wanaopata huduma za fedha ya Finscope mwaka 2013 inaonyesha kulikuwa na wananchi milioni 24.2 milioni wanaopata huduma za fedha kutoka. Kati ya wote hao, asilimia 44 ilikuwa ni kupitia simu za mkononi hivyo kuiweka Tanzania miongoni mwa nchi zenye watumiaji wengi wa huduma hizo.

Maria Mtili

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania