Nuzulack Dausen September 12, 2017
*Wachambuzi wasema iwapo halmashauri zitachelewa kuyalipa yataiongezea Serikali hasara
Dar es Salaam. Manispaa tatu zilizopo Dar es Salaam za Temeke, Kinondoni na Ilala ni miongoni mwa halmashauri tano zinazodaiwa madeni makubwa nchini jambo litakalofanya ziingie kulipa gharama kubwa ya riba iwapo ulipaji utacheleweshwa.
Ripoti ya ukaguzi wa taarifa za fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa mwaka 2015/16 ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Juma Assad inaonesha Manispaa ya Kinondoni inaongoza nchini kwa kuwa na deni kubwa la Sh16.64 bilioni ikifuatiwa na Ilala iliyokuwa na deni la Sh10.53 bilioni na Temeke iliyokuwa na deni la Sh5.78 bilioni.
Halmashauri nyingine zilizobainishwa kuwa vinara wa madeni ni Manispaa ya Dodoma iliyokuwa inadaiwa Sh5.18 bilioni na Halmashauri ya wilaya ya Karagwe mkoani Kagera iliyokuwa na deni la 4.84 bilioni.
Profesa Assad, katika ripoti hiyo aliyoisoma bungeni miezi ya hivi karibuni, anaitaka Ofisi ya Rais-Tamisemi kuhakikisha kuwa halmashauri zote zinazodaiwa zinalipa madeni yote pale muda wa kulipa unapowadia.
“Zaidi ya hayo, halmashauri zinapaswa kuanzisha mfumo wake wa ndani wa kudhibiti na kuratibu madeni ili kuhakikisha kwamba menejimenti za halmashauri zinawajibishwa kwa kuwa na madeni yasiyokuwa na manufaa za Serikali za mitaa husika,” anasema.
Wachambuzi wa masuala ya uchumi na fedha wanaeleza kuwa iwapo madeni yatachelewa kulipwa yatafanya taasisi husika kuwa na madeni makubwa yanayotokana na kuongezeka kwa riba kiasi cha kufanya fedha zilizotakiwa kutekeleza miradi ya maendeleo kutumika kuwalipa wadeni.
Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi anasema halmashauri zinatengeneza madeni kwa sababu kama taasisi nyingine hununua bidhaa na huduma kutoka kwa makandarasi kama ujenzi wa miundombinu hivyo malipo yakichelewa huwa madeni.
Soma zaidi: CAG aibua madudu Benki ya Posta
Anasema baadhi ya madeni huwa na riba yanapochelewa kulipwa ndani ya ukomo wake hivyo kufanya huduma au bidhaa iliyonunuliwa kuwa na gharama kubwa kuliko uhalisia.
Mbali na madeni, anasema baadhi ya makandarasi wanaweza kusitisha huduma husika jambo linaloweza kuwaathiri wananchi wanaozitegemea katika halmashauri husika.
“Iwapo halmashauri zitachelewa kulipa madeni baada ya ukomo kufika zitasababisha taswira yao na Serikali kuu kuonekana ni ya wababaishaji. Pia, riba inafanya bidhaa badala ya kununuliwa Sh100 ya awali inakuja kununuliwa kwa Sh120…hii siyo nzuri kwa sababu inaiingizia Serikali hasara,” anasema Profesa Ngowi.
Halmashauri zimesema zimeshalipa sehemu kubwa ya madeni hayo na kwamba si rahisi taasisi kukosa madeni kabisa kutokana na mikopo kuwa sehemu ya vyanzo vya fedha vya Serikali za Mitaa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke, Nassib Mmbaga anasema kuwa sehemu kubwa ya madeni yaliyokuwepo wameshalipa na yaliyobaki ni yale ambayo ukomo wake haujafika.
“Kuna deni kubwa tulilokopa kutoka benki ya CRDB kulipa fidia kwa ajili ya miundombinu iliyopo chini ya mradi wa uendelezaji jiji la Dar es Salaam(DMDP). Mengine yaliyobaki ni madogo madogo ila kimsingi madeni mengi niliyoyakuta tumeshayalipa,” anasema Mmbaga.
Mweka Hazina wa halmashauri hiyo, Tumaini Mrango anasema deni la CRDB lilikuwa Sh19.5 bilioni na wanaendelea kulilipa na kila robo mwaka hurejesha Sh1.2 bilioni.
“Riba zilizopo ni zile zilizopo kwenye mikataba na hakuna madeni tuliyochelewa na kusababisha riba kubwa,” anasema Mrango.
Nuzulack Dausen
Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.