Nuzulack Dausen September 13, 2017
*Wakulima kuanzia Septemba 15 wataanza kununua mbolea kwa bei mpya ambazo nyingi ni nafuu kuliko ilivyo sasa.
Dar es Salaam. Wakulima wa Kyela mkoani Mbeya ni miongoni mwa watakaonufaika kwa kiasi kikubwa na bei elekezi za mbolea zilizotangazwa na Serikali baada ya bei hizo mpya kuonyesha kuwa wataokoa wastani wa zaidi Sh22,000 kwa mfuko wa kilo 50.
Katika bei hizo mpya zitakazoanza kutumika Ijumaa Septemba 15, wakulima wa Kyela watanunua mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya DAP kwa bei ya rejareja ya Sh54,289 ikilinganishwa na wastani wa bei ya sasa ya Sh79,375.
Kwa mujibu wa bei hizo elekezi zilizotangazwa jana Septemba 12 na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba wauzaji wa pembejeo watatakiwa kuuza mbolea ya Urea wilayani Kyela kwa Sh41,710 kutoka wastani wa Sh64,285 kwa mfuko wa kilo 50.
Takwimu za bei za sasa zilizotolewa na wizara hiyo zinaonyesha wakulima wilayani Kyela ndio waliokuwa wakinunua mbolea kwa bei ghali zaidi katika kanda ya Nyanda ya Juu Kusini inayojumuisha mikoa ya Mbeya, Iringa, Ruvuma, Rukwa na Njombe.
Soma zaidi: Wakulima walianzisha na Tizeba
Kwa bei hizo mpya, Serikali inatarajia iwapo mbolea ya Dap itanunuliwa kwa kutumia mfumo wa ununuzi wa pamoja (PBS), gharama za ununuzi wa mbolea hiyo Kyela itapungua kwa asilimia 32 wakati Urea itapungua kwa asilimia 35.
Dk Tizeba amesema ibara ya 56 ya Kanuni za Mbolea na marekebisho yake ya mwaka 2017 inataka mbolea za aina zote ziuzwe kwa bei iliyopangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).
“Kwa jumla bei elekezi ya mbolea imepangwa kwa kuzingatia gharama za ununuzi wa mbolea kutoka kwenye chanzo, usafirishaji wake kwa meli, tozo mbalimbali na faida ya wafanyabiashara. Gharama ya uingizaji kutoka nje ya nchi imejumlishwa na gharama za usafirishaji mbolea nchini,” amesema Dk Tizeba katika taarifa kwa vyombo vya habari.
Iwapo mbolea zitauzwa kama Serikali ilivyopanga, wakulima wa Halmashauri ya Lindi watakuwa na ahueni kubwa kitaifa kwa kuwa bei ya sasa ya mbolea ya Dap ni Sh100,000 kwa mfuko wa kilo 50 lakini Serikali imeagiza iuzwe kwa Sh51,621. Wakulima wa halmashauri hiyo ndiyo wanaonunua mbolea kwa bei ya juu zaidi nchini.
Soma zaidi: Matumizi ya mbolea nchini sasa yadaiwa kuongezeka
Hii ina maana kuwa mkulima wa Lindi baada ya kuanza kutumika bei mpya Ijumaa hii wataweza kununua mifuko miwili ya mbolea ya Dap kwa kuongeza Sh3,250 tu badala ya mfuko mmoja wanaonunua sasa.
Hata hivyo, baadhi ya wadau mkoani Songwe wameomba Serikali kuangalia upya bei hizo kutokana na kutompa ahueni mkulima kwa kuwa bei elekezi ni kubwa kuliko ile iliyokuwa ikiuzwa mwaka jana.
Mapema mwezi huu, gazeti hili lilimnukuu mjumbe kutoka wilaya ya Songwe, Samwel Jeremiah kuwa bei ya mbolea aina ya Dap msimu uliopita wa 2016/17 ilikuwa ikiuzwa kati ya Sh52,000 na Sh62,000.
Bei elekezi iliyotolewa kwa sasa na Serikali wilayani Mbozi katika kituo cha Vwawa, mfuko wa kilo 50 wa Dap utauzwa kwa Sh54,014.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFRA, Lazaro Kitandu ameiambia MwananchiData kuwa bei walizorekodi sokoni kwa sasa ni za wastani na sahihi.
“Hakuna eneo ambalo bei elekezi ipo juu kuliko ile tuliyoirekodi kuwa ndiyo inatumika sokoni,” amesema Kitand
Nuzulack Dausen
Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.