Magonjwa yanayoongoza kusababisha vifo Tanzania

Nuzulack Dausen
September 13, 2017

Mikoa yafanya tathmini ya kudhibiti hali hiyo

 Nuzulack Dausen na Jesse Mikofu, Mwananchi

[email protected]

Mwanza/Dar. Magonjwa ya malaria, maradhi yanayoathiri mfumo wa kupumua, Ukimwi, upungufu wa damu na magonjwa ya moyo ni miongoni mwa magonjwa yaliyochangia kwa kiwango kikubwa kuchukua uhai wa Watanzania  247,976  kwa miaka 10  iliyopita katika hospitali mbalimbali hapa nchini, utafiti waonyesha.

Katika ufunguzi wa warsha kuhusu sababu za vifo katika hospitali nchini iliyofanyika jijini Mwanza juzi, Mtafiti Mkuu Kiongozi wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Leonard Mboera alisema lengo la utafiti huo ni kutambua ongezeko la maradhi yanayoathiri jamii.

Dk Mboera alisema vifo hivyo vilitolewa taarifa kwa kipindi cha miaka 10 kati ya 2006 na 2015, huku vifo vingi vikiathiri wanaume kuliko wanawake.

Alisema katika kundi la watoto chini ya miaka mitano vilichangia asilimia 20 ya vifo vyote.

Utafiti
Mtafiti Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Mercy Chiduo akimuonyesha Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Leonard Subi (Kulia) aina ya magonjwa yanayoua zaidi wakati wa uwasilishaji wa tafiti za taasisi hiyo juzi jijini Mwanza. Tafiti hizo zilihusu sababu za vifo katika hospitali nchini. Picha na Jesse Mikofu

“Magonjwa yaliyoongoza kuua ni malaria vifo 28,219 sawa na asilimia 12.8, magonjwa ya mfumo wa kupumua vifo 22,316 sawa na asilimia 10.1, Ukimwi 17,790 sawa na asilimia 8, upungufu wa damu vifo 17,218 sawa na asilimia 7.8 na magonjwa ya moyo na mfumo wa damu vifo 13,981 asilimia 6.3,” alisema mtafiti huyo.

Utafiti huo unashabihiana na takwimu za vifo kitaifa za mwaka 2013 kutoka kituo huru cha takwimu cha umma cha opendata.go.tz zilizochapishwa katika tovuti ya Hurumap Tanzania. Takwimu hizo zinaonyesha kuwa ugonjwa wa malaria, homa ya mapafu na upungufu wa damu ni miongoni mwa magonjwa makubwa matatu yaliyochangia vifo vingi kwa zaidi ya asilimia 15 ya vifo vyote kwa watoto chini ya miaka mitano.

Kwa wakubwa wenye miaka mitano na kuendelea, takwimu hizo zinaonyesha magonjwa mengineyo, malaria, Ukimwi na upungufu wa damu yaliyongoza baada ya kuwa kwenye nne bora ya yaliyosababisha vifo vingi mwaka 2013.

Dk Mboera alisema vifo vingi vilitokea katika hospitali za mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza huku vingi vikiathiri kundi la watu wenye umri wa miaka 30 hadi 45.

Watu wengi waliokufa walikuwa na umri wa miaka 31 (wanaume miaka 33 na wanawake miaka 29).

Alisema katika vifo hivyo, 17,772 vilichangiwa na ajali kwa asilimia 5.32, huku mikoa ya Rukwa, Tabora Singida, Kigoma na Dar es Salaam ikiathirika zaidi.

Alisema utafiti huo uliofanyika Julai hadi Desemba 2016, ulihusisha hospitali 39 ikiwamo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), hospitali za rufaa za kanda na mikoa, hospitali maalumu za wilaya na kwamba taarifa hizo walizipata kwenye orodha ya hospitali na vibali vya mazishi kutoka kwa Wakala wa Usajili wa Vizazi, Vifo na Ufilisi (Rita) ofisi za wilaya.

Utafiti

Dk Mboera alisema licha ya taarifa za vifo vinavyotokea hospitalini kuwa vyanzo muhimu katika kupanga mipango na kuandaa Sera ya Afya  na kuanisha vyanzo na kufuatilia matukio ya vifo hivyo, kuna uhaba mkubwa wa takwimu za vifo vinavyotokea katika hospitali mbalimbali nchini.

Akifungua warsha hiyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,  Dk Leonard Subi aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, John Mongella, alisema katika mpango mkakati wa sekta ya afya namba IV, Serikali inachukua hatua mahsusi kuboresha mfumo wa utoaji taarifa za afya ili kukidhi mahitaji ya ufuatiliaji huduma.

“Ni dhamira ya Serikali kutumia mfumo wa kielektroniki katika ukusanyaji, uchanganuzi na matumizi ya takwimu ili kuongeza ubora,” alisema. Warsha hiyo ilishirikisha wataalamu wa afya kutoka mikoa minane ya Mwanza, Mara, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Geita, Kigoma na Kagera.

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania