Nuzulack Dausen September 25, 2017
- Tunduma ina msongamano mkubwa wa watu kuliko halmashauri nyingine za mikoa ya Mbeya na Songwe.
- Mkuu wa Mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu Chiku Galawa asema kama kuna mtu anajipanga kwenda Tunduma kufanya biashara za magendo bora aihirishe safari.
- Msongamano wa watu Tunduma ni takriban mara 47 ya wastani wa msongamano kwa mikoa ya Songwe na Mbeya mwaka 2015.
Dar es Salaam. Kama ulifikiri maeneo yanayovutia watu wengi zaidi ni majiji pekee, badilisha fikra. Katika mikoa ya Mbeya na Songwe, Halmashauri ya Tunduma inaonekana kuvutia watu wengi zaidi kuishi baada ya kuwa na msongamano mkubwa wa watu kuzidi ule wa halmashauri ya jiji la Mbeya.
Taarifa ya mkoa wa Mbeya mwaka 2016 inaonyesha kuwa Tunduma ina kilomita za mraba 48.8 lakini mwaka 2015 ilikuwa na watu 106,852 jambo lililofanya watu 2,190 wabanane kwenye kilomita moja ya mraba, eneo ambalo ni dogo zaidi kwa idadi hiyo yawa watu.
Uwingi huo wa watu umefanya Tunduma iongoze kwa msongamano mkubwa wa watu ikilinganishwa na halmashauri nyingine kama Mbeya mjini, Kyela, Mbozi na Mbarali.
Watu wanaoishi Tunduma ni wengi kuliko ardhi iliyopo kiasi cha kuwa na msongano mkubwa wa takriban mara 47 ya wastani wa msongamano wa watu katika mikoa ya Mbeya na Songwe.
Halmashauri ya jiji la Mbeya ina msongamano wa watu wapatao 1,972 kwa kilomita ya mraba ikiwa ni halmashauri ya pili kwa kuwa na watu wengi zaidi kuliko eneo husika ikifuatiwa na Kyela yenye watu 183 kwa kilomita ya mraba.
Hata wakati watu wengi wakikimbilia Tunduma, halmashauri ya Chunya ndiyo yenye msongamano mdogo kuliko zote katika mikoa hiyo kwa kuwa na wastani wa watu 11 tu kwa kilomita moja ya mraba kiwango ambacho ni pungufu mara tano ya kile cha kitaifa ambacho ni watu 57 kwa kila kilomita ya mraba hadi mwaka jana.
Kwa mujibu wa watalaamu wa mipango miji na maendeleo, watu wengi hukimbilia mijini kama Tunduma na jijini Mbeya kwa sababu kuna fursa lukuki za kimaendeleo kama uwepo wa ajira, fursa za kiuwekezaji kibiashara na urahisi wa upatikanaji wa huduma za kijamii.
Halmashauri ya Tunduma ni maarufu kwa biashara katika mkoa wa Songwe kutokana na kupakana na nchi jirani ya Zambia. Ni lango la kibiashara kati ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika ya Kati na kusini mwa Afrika kama Zimbabwe na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na watu wengi hufanya biashara ya kubadilisha fedha.
Pia, inafikika kwa reli ya Tazara inayotoka Dar es Salaaam hadi Zambia na kwa barabara ya lami ya Tanzania-Zambia maarufu kama Tanzam.
Halmashauri hiyo kwa sasa ipo ndani ya mkoa wa Songwe baada ya Serikali kuugawa mkoa wa Mbeya mwaka 2015 ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi.
Sehemu kubwa ya wakazi wa mikoa ya Songwe na Mbeya ni wakulima na wafugaji.
Mapema mwezi huu, gazeti dada la The Citizen lilimnukuu Ofisa wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), David Omuzuofoh kuwa ili kukabiliana na msongamano wa watu katika miji nchini kama ilivyo kwa Dar es Salaam Serikali haina budi kuweka sera zitakazozingatia upanuaji wa maeneo mengine mikoani.
“Kama watu wa miji inayokua na vijijini watapata hudumu muhimu kama zile za kijamii katika maeneo yao, jiji linaweza kuwa na mazingira bora ya kuishi na hakuna mtu atakayetamani kukimbilia kwenye majiji kama Dar es Salaam,” amenukuliwa Omuzuofoh.
Soma zaidi: Simulizi ya mwandishi wa Mwananchi ndani ya lori Dar – Tunduma-1
MAKALA YA UCHUNGUZI: Simulizi ya mwandishi wa Mwananchi ndani ya lori 4
Hata hivyo, kwa mujibu wa chapisho la taasisi ya utafiti wa kijamii na kiuchumi (ESRF) na UNDP la mwaka 2014, msongamano wa watu unaweza pia kuwa fursa kwa Serikali katika utoaji wa huduma za kijamii.
“Msongamano wa watu mijini unaweza kuisaidia serikali kutoa huduma muhimu kama miundombinu na huduma za kijamii kwa gharama nafuu kwa mtu mmoja mmoja,” inasomeka sehemu ya chapisho hilo la utafiti uliofanywa na Profesa Alfred Agwanda na Profesa Haidari Amani.
Chapisho hilo linaloitwa ‘ongezeko la watu, muundo na mwenendo Tanzania (Population growth, structure and momentum in Tanzania) linaeleza kuwa kukua kwa miji ni sehemu ya mpito ya idadi ya watu hivyo mipango madhubuti inaweza kuisadia nchi kutumia fursa na kutokomeza changamoto zilizopo.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Luteni Mstaafu Chiku Galawa anasema Tunduma ni lango la nchi zote za Jumuiya ya Maendendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na inakimbiliwa na watu wengi kwa sababu ya kuwepo kwa fursa za kibiashara za haraka haraka hususan uchuuzi ambao hufanywa kwa waendesha malori.
“Tulichelewa kuupanga mji. Ni mwaka jana tu ndiyo imekuwa halmashauri kipindi chote hicho ulikuwa ukisimamiwa na halmashauri ya mbali. Hata miundombinu unaiona ilikuwa hovyo ila kwa sasa tunaupanga upya ili uendane na mahitaji halisi,” anasema Galawa.
Anasema mpango mji (masterplan) tayari umeshaandaliwa na leo (Jumatatu, Septembe 25) ulitakiwa uwe umeshatumwa na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kwenda kwa halmashauri kwa ajili ya utekelezaji.
Katika mpango huo mpya, Galawa anasema wametenga maeneo ya viwanda na uwekezaji kwa ajili ya sekta binafsi na katika kata ambazo ni za vijijini wamepanga kuhamasisha kilimo cha kisasa ili kulisha watu waliopo katika eneo hilo na maeneo mengine.
“Wengi wana dhana ya kuja huku kufanya biashara haramu hilo wasahau. Kama kuna mtu anakuja kufanya magendo ajipime kabisa bora asije kwa sababu kwa sasa tunausafisha mpaka na kuhakikisha biashara zote ni halali,” anasema Galawa.
Nuzulack Dausen
Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.