Uwanja wa Uhuru waokoa ligi za TFF

Maria Mtili
September 28, 2017

Uwanja wa Uhuru umefanyiwa marekebisha na kuruhusiwa kutumika kwa michezo kadhaa na unaonekana kuwa msaada

Charles Abel, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Uwanja wa Uhuru umeandika rekodi mpya ya kuwa uwanja utakaokuwa na idadi kubwa ya mechi za ligi kubwa tatu nchini msimu huu ukifuatiwa na Azam Complex na ule wa Sokoine mkoani Mbeya.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini jumla ya mechi 45 za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili zitachezwa kwenye uwanja wa Uhuru, idadi ambayo ni kubwa zaidi kuliko uwanja mwingine wowote.

Kitendo cha Uwanja wa Taifa kufungwa kwa muda ili kupisha matengenezo ambayo yanakadiriwa kuchukua miezi mitatu, kimezifanya timu za Simba na Yanga kuchezea baadhi ya mechi zake za Ligi Kuu katika Uwanja wa Uhuru, jambo lililouongezea idadi ya mechi uwanja huo msimu huu.

Mwonekano mpya wa sehemu ya kuchezea ya Uwanja wa Taifa baada ya nyasi zilizopandwa hivi karibuni kuanza kuota. Uwanja huo ulichimbuliwa, ukabadilishwa udongo na nyasi mpya kupandwa katika ukarabati uliogharimiwa na kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa.

Yanga itacheza mechi nane katika uwanja huo, Simba itacheza michezo saba (7) wakati timu nyingine zitakazoutumia uwanja huo na idadi ya mechi zitakazocheza kwenye mabano ni African Lyon (7), Mshikamano (7), Mvuvumwa (7), Ashanti (7) na Ruvu Shooting (2).

Katika kile kinachoonekana Uwanja wa Azam Complex unaomilikiwa na Azam FC, thamani yake imeanza kutambulika, unashika nafasi ya pili kwa kuandaa idadi kubwa ya mechi.

Jumla ya mechi 41 zitachezwa hapo msimu huu, kwa timu za Azam FC, Green Warriors, KMC, Polisi Dar na Friends Rangers ambazo zinautumia kwa mechi za nyumbani katika Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza pamoja na Ligi Daraja la Pili.

Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya wenyewe utaandaa mechi 30 wakati nafasi ya nne inashikiliwa na uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga ambao mashabiki watashuhudia jumla ya mechi 29 za timu za Stand United, Mwadui FC na Transit Camp.

Nafasi ya tano ni Uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma utakaondaa mechi 27 wakati viwanja vya Highland Estate na Mwakangale (Mbeya), Ilulu  (Lindi), Mkamba (Morogoro) na Lake Tanganyika (Kigoma) vikiwa kwenye nafasi tano za mwisho kwa kuandaa idadi chache za mechi ambapo kila mmoja utashuhudia mechi tano ambazo ni za ligi daraja la pili kwa timu za nyumbani.

Uwanja wa Highland Estate unatumiwa na timu ya Ihefu, Mwakangale unatumiwa na Boma FC, Ilulu unatumiwa na Namungo FC, Mkamba unatumiwa na Mkamba Rangers wakato Lake Tanganyika unatumiwa na Mashujaa FC.

Pamoja na ukweli kwamba viwanja vyenye nyasi bandia vikitumika zaidi ndivyo vinazidi kuwa bora, huenda wingi wa michezo ukatoa nafasi finyu kwa kuvifanyia marekebisho. kutokana na kutumika kila wakati.

Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffary Iddi alisema klabu yake imeamua kuziruhusu klabu nyingine kuutumia uwanja huo kwa sababu iliujenga kwa kengo la kuleta maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu.

“Kuna klabu ziliomba kutumia uwanja wetu na uongozi ukaona sio vibaya kuwakubalia maombi yao. Hivyo tunaendelea kuwakaribisha Watanzania hapa Azam Complex na wajisikie wapo nyumbani, ingawa wanapaswa kuhakikisha wanautumia vizuri ili miundombinu yake, ambayo ni bora isiharibiwe kwa faida ya vizazi vijavyo,” alisema Iddi.

Kocha wa Mbeya Kwanza, ambaye timu yake inautumia Uwanja wa Mabatini, Pwani badala ya Sokoine Mbeya, Anthony Mwamlima, alisema klabu yake imefanya hivyo kusaidia kumudu gharama za uendeshaji.

Maria Mtili

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania