Ufuatiliaji unavyoweza kudhibiti ‘vifo’ vya miradi ya maji vijijini

Maria Mtili
October 2, 2017

Maeneo mengi yenye miradi iliyokufa wananchi wake wanachota maji katika vyanzo visivyo safi na salama

Nuzulack Dausen, Mwananchi; [email protected]

Zaidi ya mwaka mmoja sasa wananchi wa vijiji vya Namikango A, Nangunde na Namikango B hawana chanzo chochote cha maji safi na salama.

Ili kuyapata maji ya kutumia majumbani mwao, wanavijiji hao wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, kwa sasa wanalazimika kwenda kuchota maji kwenye visima vya wazi vilivyochimbwa katika maeneo yenye asili ya chemchemi.

Kwa baadhi ya wanavjiji wa kata hiyo ya Namikango, ili kufikia visima au chemchemi hizo wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita tatu hadi tano kupata maji hayo ambayo si salama.

Mabomba yaliyowekwa kwenye baadhi ya maeneo katika vijiji hivyo ikiwamo ya zahanati ya Nangunde yamezungukwa na nyasi na baadhi yakiwa na kutu kuashiria kuwa huduma ya maji haijapatikana maeneo hayo kwa muda mrefu.

“Maji yote tunayoyatumia huwa tunaenda kuchota mabondeni kwenye chemichem ambako tunatumia zaidi ya saa mbili kuyapata kutokana na foleni,” anasema Telesia Daniel mkazi wa Namikango A.

Tofauti na vijiji vingine vya wilaya hiyo ambavyo havijawahi kuwa na vyanzo vyovyote vya maji safi na salama kama Litandamtama na Lionja B, vijiji vya Namikango A, Nangunde na Namikango B na Kijiji cha Mpute vilikuwa na miundombinu ya kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama muda wote mwaka mmoja uliopita.

Vijiji hivyo vimebarikiwa kuwa na chanzo kikubwa cha maji yasiyo na chumvi nyingi cha Namichiu kilichopo eneo hilo na mtandao wa mabomba na matanki makubwa ya kuhifadhi maji wakati wote likiwemo la lita 40,000.

Huduma za bomba zilifika hadi kwenye maeneo ya taasisi muhimu za shule na zahanati ya vijiji hivyo.

“Zamani wakati bomba zinatoa maji tulikuwa tunatumia nusu saa tu kuchota maji na kurudi nyumbani. Japo tulikuwa tunalipia Sh100 kwa ndoo na kituo kilikuwa kimoja kwa kila kijiji bado umbali haukuwa mrefu sana kufuata maji kama ilivyo sasa,” anasema Telesia.

Hata hivyo, ukosefu wa mipango madhubuti ya kuendeleza miradi ya maji umefanya wananchi wa vijiji hivyo warudi katika kipindi cha shida kama zamani.

“Tuliambiwa mashine ni mbovu viongozi wanaitengeneza na siyo muda itatengemaa. Lakini tuna zaidi ya mwaka hatupati maji licha ya kwamba tulikuwa tunachangia gharama za ukarabati kwa kununua maji Sh100 kwa ndoo,” anasema Juma Mohammed mkazi wa Namikango B.

Uhaba wa maji wanaokabiliana nao kwa sasa umekuja baada ya mashine na pampu ya umeme iliyokuwa inatumika kuzalisha maji kuharibika na serikali za vijiji kushindwa kumudu gharama za matengenezo au kununua nyingine.

Tatizo la usimamizi mbovu wa miundombinu ya maji safi na salama linaviandama vijiji vingi vya wilaya hiyo vikiwemo Lionja A na Lionja B.

Lionja B ilikuwa na kisima cha pampu ya mkono walichojengewa na asasi ya kiraia ya Gain ambacho kiliharibika ndani ya miaka miwili baada ya kuzinduliwa. Serikali ya kijiji ilishindwa kufanyia marekebisho na sasa wananchi wamerudi kuchota maji kwenye visima vya wazi visivyotibiwa na chemchemi.

“Gain walikuja kukiangalia kisima wakasema kuna mpira umeharibika hivyo walituahaidi watarudi kufanya matengenezo,” anasema Rajab Mpunga, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Lionja B.

Lionja A nao walishawahi kuwa na kisima kikubwa na mashine ya dizeli ya kuzalisha maji na kusambaza kijijini hapo tangu miaka ya 1980, lakini kwa sasa jengo ilimokuwemo mashine hiyo limebaki gofu. Kisima kimebaki wazi na maji yamechafuka. Mashine imehifadhiwa kwenye ofisi ya Mtendaji wa kata wa Lionja.

Matenki yaliyokuwa yanahifadhi maji hayo hayatumiki tena na wataalamu wa maji wanahofu kuwa mabomba yaliyokuwa yanatumika zamani huenda yasifae tena kwa sasa.

Kisima kidogo cha pampu ya mkono kilichokuwepo katika kitongoji cha Madukani kijijini hapo kilishang’olewa.

“Watu wabaya (waharibifu) waliking’oa kisima cha Madukani baada ya kufungua nati zote zinazoshikilia mikono ya kupampu ya maji. Ilibidi tubebe na kuhifadhi sehemu ya juu kwa ajili ya usalama na hadi sasa hatumjui aliyefanya uovu huu kwa sababu ulifanywa usiku,” anasema Said Juma, Mwenyekiti wa Kijiji cha Lionja A.

Tatizo la kutelekeza miundombinu ya maji ni la kitaifa. Kwa mujibu takwimu za vituo vya maji nchini za mwaka 2015 zilizochapishwa katika kituo huru cha takwimu (www.opendata.go.tz) zinaonyesha kuwa takriban vituo vya maji vinne katika kila 10 (asilimia 39.6) havifanyi kazi.

Nini kinaua miradi?

Viongozi wa serikali za mitaa wanalia ukata kuwa ni chanzo cha kushindwa kurekebisha miundombinu ya maji iliyochakaa.

Pia, wanawanyooshea vidole baadhi ya wananchi wasiopenda kuchangia huduma za maji na waharibifu wa miundombinu kuwa chanzo kikubwa cha miradi kutokuwa endelevu.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Namikango, Bakir Ngawanje anasema huduma ya majisafi na salama ilisitishwa mapema mwaka jana kwa sababu ya uchakavu wa mashine ya kusukuma maji iliyopo katika chanzo cha maji cha Namichiu ambayo inawagharimu fedha nyingi kwa ajili ya marekebisho kiasi cha kuzidi hata michango ya wananchi.

“Baada ya mashine yetu kuharibika tulilazimika kukodi mashine chakavu kutoka katika kanisa la Mrumba, Mnero kwa mkataba wa masharti nafuu ya Sh600, 000 kwa mwaka lakini bado gharama za mafuta na matengenezo ni kubwa,” anasema.

“Baada ya mafundi wa Halmashauri kuja ilibainika pampu nayo ni mbovu na kutokana na ufinyu wa bajeti tulilazimika kusubiri tupate fedha kwa ajili ya matengenezo,” anasema.

Anasema ili kununua mashine mpya ya dizeli kama iliyopo sasa inahitajika Sh60 milioni kiwango ambacho mapato ya kata wala michango ya wananchi haiwezi kufanikisha ununuzi huo.

“Katika bajeti ya 2017/18 tumepangiwa Sh50 milioni kwa ajili ya kufanya ukarabati na Sh160 milioni kwa ajili ya kuongeza mtandao wa vituo vya kutoa maji mitaani.

“Japo mwaka huu hatuna wasiwasi sana ila tatizo limekuwa ni utekelezaji kwa sababu mwaka jana tulitenga pia fedha kwa ajili ya ukaratabati lakini ruzuku kutoka Serikali Kuu haikutosha,” anasema Emmanuel Mhagama diwani wa Namikango.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Namikango A, Wilfred Maolo anasema kwa kushirikiana na halmashauri walishapata pampu na mashine kutoka Kijiji cha Nanjihi, Kata ya Kilimarondo wilayani humo baada ya kubadilishana na mifuko ya saruji yenye thamani ya Sh4 milioni kwa ajili ya kujengea madarasa.

“Tutaenda kuichukua hiyo mashine na pampu tuifunge huku na halmashauri imesharidhia kwa sababu wao Nanjihi hawana shida ya maji kama sisi,” anasema Maolo.

Siku chache kabla ya makala haya kuchapishwa gazetini, Maolo alisema kuwa wameshaichukua mashine ya pampu ya maji kutoka Nanjihi na maji yanatoka kwa takriban wiki mbili sasa kwa wananchi kulipia Sh100 kwa ndoo.

Hata hivyo, anahofu kuwa uchakavu wa mfumo wa bomba huenda ukakwamisha utoaji mzuri wa huduma za maji safi na salama kwa wakazi wa vijiji hivyo.

Mradi wa maji wa Lionja uliokuwa ukitumia mashine ya mafuta ya dizeli huenda usiamke tena na badala yake Serikali inapanga kujenga mradi mpya katika eneo jingine.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge.

Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Nachingwea, Bartholomew Matwiga anasema baada ya kufanya utafiti wamebaini kuwa Lionja wanahitaji kuchimba kisima kirefu cha kudumu na siyo kufufua kile cha zamani.

Ukiachana na wananchi wa Namikango A na B walio tayari kuchangia maji, Lionja A wamegomea kuchangia fedha za mfuko wa maji ambazo zinatakiwa kutumika kufanya ukarabati wa miundombinu ya kisima kipya cha pampu ya mkono kilichojengwa na Gain miezi mitatu iliyopita.

“Katika mkutano ulioitishwa na viongozi wa vijiji wananchi wengi walikataa kwa sababu hali ya kipato ni ngumu. Wananchi walisema kwa sasa tusinunue maji kwa makubaliano kuwa tutachanga kitakapoharibika,” anasema Issa Matete mkazi wa Lionja.

Sera ya Maji ya 2002 inamtaka kila mwananchi kuchangia maji ili fedha zisaidie kuendesha utoaji wa huduma hiyo muhimu kwa uhai wa mwanadamu.

Gazeti hili limebaini kuwa baadhi ya wananchi hubamiza pampu za visima wakati wa kuchota maji na wengine huwaacha watoto wachezee miundombinu ya bomba jambo linalochochea miundombinu kuharibika na kuchakaa haraka.

Hata hivyo, wananchi wengi wanasema kuwa hawawajui waharibifu wa miundombinu hiyo kwa kuwa ni “jukumu la Serikali kusimamia mambo hayo.”

Kamati za maji hazikuwa na nguvu ya kusimamia ipasavyo miradi na hivi sasa Serikali inaratibu uundwaji wa jumuiya mpya za watumiaji maji (COWSO) zitakazosimamia jukumu la kukusanya fedha na kuendesha miradi yote ya maji vijijini.

Suluhu ya kudumu

Wadau wa sekta ya maji wanasema miradi mingi ya maji inakufa kwa sababu ya udhaifu katika usimamizi hususan uchangiaji na ukarabati wa mara kwa mara wa miundombinu.

“Wastani wa gharama za kukarabati kisima kwa mwaka ni kati ya Sh250, 000 hadi Sh300,000 hivyo wananchi wakichangia vyema na kukarabati visima vyao mara kwa mara miradi mingi itakuwa endelevu na itatua tatizo la maji vijijini,” anasema Geofrey Kemiti, Mkurugenzi Mtendaji wa asasi ya kiraia ya Gain inayosaidia kutoa huduma za maji vijijini.

Kemiti anasema lazima kuwe na mafundi bora ndani ya vijiji husika ili iwe rahisi kukarabati miundombinu ikiharibika badala ya kusubiri mafundi kutoka wilayani ambako katika baadhi ya maeneo ni mbali.

Serikali inasema katika bajeti ya mwaka 2017/18 inaendelea kukarabati na kufufua miradi ya maji iliyokufa ili kuongeza upatikanaji wa maji vijijini huku ikieleza kuwa suala la wananchi kuchangia maji ni la lazima.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nachingwea, Arbogast Kiwale anasema wameshatoa Sh4 milioni ikiwemo Sh1 milioni kutoka mfuko wa jimbo kutoka kwa mbunge kwa ajili ya kukarabati mradi wa Namikango.

“Hadi sasa tumeshakarabati visima 127 kati ya 232 vilivyopo kwenye halmashauri yetu. Mahitaji ni makubwa lakini changamoto kubwa ni rasilimali fedha za kufanikisha yote hayo kwa sababu lengo letu ni kuhakikisha kituo kimoja cha maji kinahudumia wananchi 250,” anasema Kiwale.

Kauli ya waziri

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge anasema Cowso haziwezi kuendesha miradi ya maji bila fedha hivyo inabidi wananchi wachangie kwa kununua maji kwa Sh50 au Sh100 kwa ndoo ili fedha hizo ziende kwenye mfuko wa maji na kuufanya mradi kuwa endelevu.

“Kama kuna sehemu hawachangii kutakuwa kuna tatizo la uhamasishaji kwa sababu asilimia 95 ya Watanzania wapo tayari kulipia na kuifanya miradi endelevu hivyo tutaendelea kuwafuata waliosalia kuwapa elimu ya kuchangia ili miradi iwe endelevu,” anasema Lwenge.

Kuhusu kufufua miradi iliyokufa Waziri huyo anasema katika bajeti ya mwaka huu kuna mpango wa malipo kwa matokeo ambao kazi yake kubwa ni kufufua miradi iliyokufa na zimeshatengwa zaidi ya Sh240 bilioni kwa miaka mitatu kutoka Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID).

“Hivyo kila kituo cha maji kitakachofufuliwa halmashauri husika itapewa fedha na halmshauri nyingi wameshaanza kuzipata na mwaka huu miradi mingi itaanza kufufuliwa,” anasema.

Maria Mtili

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania