Tanzania yakabiliwa na upungufu wa wataalamu dawa za usingizi

Maria Mtili
October 4, 2017

Waliopo ni asilimia 1.2 tu ya mahitaji yote ya madaktari hao muhimu katika utoaji huduma za upasuaji

Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Saalam. Tanzania inakabiliwa na uhaba wa madaktari bingwa wa dawa za usingizi, ikiwa na wataalamu 24 tu kati ya 2,000 wanaohitajika nchi nzima.

Katibu mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya, ambaye pia ni mtaalamu wa nyanja hiyo, aliwaambia wanahabari jana kuwa madaktari 24 waliopo hawatoshelezi mahitaji ya huduma hiyo muhimu wakati wa upasuaji.

Miongoni mwa taasisi zinazohitaji idadi kubwa ya wataalamu hao ni vitengo vya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) vya Mifupa (MOI) na Moyo cha Jakaya Kikwete (JKCI).

“Tunahitaji tuwe na wataalamu hawa kama 2,000 nchini,” alisema katibu huyo.

“MOI pekee inahitaji watalaamu 20 ili kuweza kufanya kazi bila yeyote kujiona anafanya ziada bila kuwa na sababu yoyote.

“Muhimbili inahitaji wataalamu 60, hapa nazungumzia wataalamu waliobobea. JKCI wanahitajika 15 na haya ndiyo mahitaji halisi.”

Dk Ulisubisya alisema hayo wakati wa kutoa mafunzo kwa madaktari bingwa wa dawa za usingizi, maarufu kwa jina la nusu kaputi, wa nchi za Afrika Mashariki ambao wako jijini Dar es Salaam kwa mafunzo ya siku nne.

Hata hivyo, Mwananchi imebaini kuwa hadi sasa MNH ina madaktari wanne tu wa nyanja hiyo, huku MOI ikiwa na wataalamu watano, sawa na asilimia 20 ya mahitaji. JKCI yenye vyumba vinne vya upasuaji, ina madaktari wanne wa nusu kaputi kati ya 15 wanaohitajika.

MOI, MNH na JKCI ni hospitali za kitaifa zinazohudumia wagonjwa waliopata rufaa kutoka hospitali zote nchini.

Dk Ulisubisya alisema fani hiyo imepewa kisogo na wataalamu wengi nchini, hivyo kuna kila sababu ya kuwakumbusha wajibu wao.

“Tunatoa wito kwa madaktari waliohitimu shahada ya kwanza, waone wajibu wa kujifunza fani hii ili wataalamu wetu waweze kutoa huduma ambazo ni salama na zinazopatikana kwa urahisi,” alisema.

Mkurugenzi mtendaji wa JKCI, Profesa Mohammed Janabi aliliambia gazeti hili kuwa kutokana na uhaba uliopo nchini, kwa sasa hao wanne waliopo wanatosheleza mahitaji.

DAWA ZA USINGIZI: Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Afya Kwazulu Natal, Afrika Kusini, Dk Christian Kampik (aliyevaa nguo nyekundu) akitoa mafunzo kwa madaktari bingwa wa dawa za usingizi kutoka nchi za Afrika Mashariki katika Kitengo cha Mifupa (MOI), jijini Dar es Salaam jana. Mafunzo hayo ya siku nne yanahusisha wataalamu kutoka Tanzania, Kenya, Rwanda, Uganda na Burundi. Picha na Herieth Makwetta.
DAWA ZA USINGIZI: Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Afya Kwazulu Natal, Afrika Kusini, Dk Christian Kampik (aliyevaa nguo nyekundu) akitoa mafunzo kwa madaktari bingwa wa dawa za usingizi kutoka nchi za Afrika Mashariki katika Kitengo cha Mifupa (MOI), jijini Dar es Salaam jana. Mafunzo hayo ya siku nne yanahusisha wataalamu kutoka Tanzania, Kenya, Rwanda, Uganda na Burundi. Picha na Herieth Makwetta.

Ofisa habari wa Wizara ya Afya, Catherine Sungura alisema katika kutatua tatizo hilo, wizara imekuwa ikifanya utaratibu wa kuwajengea uwezo wauguzi na matabibu kwa kuwapa mafunzo ya ndani ili kuweza kumudu uhaba wa wataalamu hao nchini.

Sungura alisema katika maeneo yenye uhaba wa watumishi wamekuwa wakiwachukua wachache kwa ajili ya mafunzo ya miezi minne hadi mwaka mmoja. Alisema mafunzo hayo hutolewa na watalaamu kutoka nje ya nchi na hufanyika Hospitali ya Ifakara.

“Kwa vituo vya afya nchini ambavyo vinatoa huduma ya upasuaji, tumekuwa tukifundisha wauguzi na matabibu namna ya kuwahudumia wagonjwa na jinsi ya kutoa huduma ya usingizi wakati wa upasuaji ili kukabiliana na upungufu uliopo,” alisema.

Mkurugenzi mtendaji wa MOI, Dk Respicius Boniface alisema katika fani ya dawa za usingizi, kuna vitu vinavyohatarisha maisha ya mgonjwa, hivyo njia bora zaidi ya kufundisha watalaamu ni kwa vitendo zaidi.

Daktari bingwa wa dawa za usingizi kwa watoto kutoka Hospitali ya Taifa Rwanda, Rosemary Mukunzi alisema mafunzo hayo ni ya kwanza kutolewa Afrika Mashariki, lakini yamekuwa yakitolewa katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Ni mafunzo muhimu kwa wataalamu wa dawa za usingizi kwa kuwa ni sekta nyeti na muhimu,” alisema  Dk Mukunzi.

“Hata hivyo, duniani wataalamu wake ni wachache.”

Maria Mtili

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania