Simba, Yanga zaibeba Dar

Maria Mtili
October 4, 2017

Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa kuwa na timu nyingi zaidi zilizopo katika mashindano yanayotambuliwa na TFF

Charles Abel, Mwananchi , [email protected]

Dar es Salaam. Kama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lisipochukua hatua za dhati, soka litamezwa na Jiji la Dar es Salaam kutokana na utitiri wa timu katika mashindano matatu wanayoyasimamia.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini ugumu uliopo kwa mikoa mingine kuangusha ‘ufalme wa Dar es Salaam’ kwenye soka, hali inayochangiwa na uwepo wa idadi kubwa ya timu zake kwenye Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na la Pili ambazo husimamiwa na TFF.

Katika idadi ya jumla ya timu 64 zinazoshiriki ligi hizo tatu zinazotambulika kama za kulipwa, Dar es Salaam pekee ina timu 16, idadi ambayo ni kubwa zaidi mara tatu ya mkoa unaoshika nafasi ya pili, ambayo pia ni sawa na 25% ya timu zote.

Kati ya timu hizo 16 zinazotokea jijini, tatu zipo Ligi Kuu, saba za Daraja la Kwanza, wakati sita zikiwa za Daraja la Pili.

Timu zinazoshiriki Ligi Kuu kutoka mkoani Dar es Salaam ni Yanga, Azam FC na Simba, wakati zilizopo Daraja la Kwanza ni JKT Ruvu, KMC, Polisi Dar, Friends Rangers, Mshikamano, Ashanti United na African Lyon.

Ligi Daraja la Pili ina timu sita kutoka Dar es Salaam, ambazo ni Reha, Changanyikeni, Abajalo, Villa Squad, Cosmopolitan na The Green Warriors.

Mikoa inafuata kwa kuwa na idadi kubwa ya timu ni Mbeya na Morogoro ambayo kila mmoja una timu tano. Mbeya wana timu za Mbeya City na Prisons zinazoshiriki Ligi Kuu, Mbeya Kwanza (Daraja la Kwanza), wakati Boma na Ihefu zinashiriki Ligi Daraja la Pili wakati  Morogoro wana Mtibwa Sugar (Ligi Kuu), Mawenzi Market na Polisi Tanzania (Ligi Daraja la Kwanza), huku Bukinafaso na Mkamba Rangers zikiwa Daraja la Pili.

Mchezaji wa klabu ya Yanga (kushoto) akifurahia jambo na nahodha wa klabu ya Simba Michael Mwanjali. PICHA |MAKTABA
Mchezaji wa klabu ya Yanga (kushoto), Thaban Kamusoko akifurahia jambo na nahodha wa klabu ya Simba Michael Mwanjali. PICHA |MAKTABA

Mwanza, Shinyanga na Arusha kila mmoja una timu nne katika madaraja hayo matatu, Tabora, Ruvuma na Tanga kuna timu tatu kwa kila mkoa wakati mikoa yenye timu mbili kila mmoja ni Dodoma, Kigoma,Pwani, Iringa, Kilimanjaro.

Mikoa ya Mtwara, Njombe, Kagera, Singida, Mara, Manyara na Lindi kila mmoja una timu moja inayoshiriki ama Ligi Kuu, Daraja la Kwanza au Daraja la Pili.

Katika hali ya kushangaza, mikoa ya Songwe, Simiyu, Geita, Katavi na Rukwa haina timu hata moja ambayo inashiriki katika madaraja hayo ya ligi hizo tatu za juu nchini hali inayofanya iwe kama visiwa.

Akizungumzia mlundikano wa timu za soka mkoani Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Dodoma (Dorefa), Mulamu Nghambi alisema inachangiwa na namna ligi zinavyoendeshwa.

“Nadhani hivi suala kama hili linaweza kuepukika iwapo wenye mamlaka ya kusimamia soka wataamua kwa dhati kwani inawezekana kabisa kutengeneza mfumo ambao utazibana timu za mkoa mmoja kujaa kama ilivyo sasa,” alisema Nghambi.

Ofisa Habari wa Toto Africans, Cuthbert Japhet alisema mpangilio usioridhisha wa makundi ya ligi za chini ndio unachangia kuzibeba timu za Dar es Salaam.

“Kwa mfano unakuta sasa hivi timu za Mwanza zinazoshiriki Daraja la Kwanza zote tatu zimepangwa kundi moja wakati huo timu sita za Dar es Salaam zimepangwa katika makundi tofauti.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema shirikisho limepokea changamoto hiyo ya utitiri wa timu kutoka Dar es Salaam na wataangalia namna ya kushughulika nayo.

Maria Mtili

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania