Uhaba wa maji unavyowatesa wanawake wilayani Nachingwea

Nuzulack Dausen
October 5, 2017

Sehemu kubwa hutembea umbali mrefu na kupoteza muda wa kufanya shughuli za maendeleo

Hawajawahi kuona maji ya bomba au ya kisima cha pampu yakitoka karibu na makazi yao katika maisha yao yote.

Wale wachache waliobahatika kutumia maji ya bomba ni ama walikuwa hospitali iliyopo mbali na kijiji chao ama katika vijiji vya jirani vilivyobahatika kuwa na huduma hizo muhimu kwa mwanadamu.

Kwa wananchi wa Kijiji cha Litandamtama katika Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi upatikanaji wa maji safi na salama ni suala la kufa au kupona.

Maisha yao yote wamekuwa wakitumia maji ya chemchemi au visima vya wazi visivyokuwa na maji salama.

“Huwezi kupata maji ya bomba au kisima cha pampu hapa labda uende kijiji cha jirani cha Lionja kuna visima vya wazi au uende mabondeni huko porini.

“Ila mabondeni ni mbali sana ndiyo maana mimi huwa naenda kuchota maji katika visima vya Lionja A na huwa natumia saa tatu tu kwa baiskeli nakuwa nimesharudi pamoja na foleni ya kuteka maji iliyopo,” anasema Agness Machafu (31).

Agness, mama wa watoto wawili, anasema iwapo atakosa baiskeli, safari ya kufuata maji, kusubiri foleni na kurudi nyumbani humchukua wastani wa saa sita kwa miguu.

Ili ufike katika kisima cha Chengo katika Kijiji cha Lionja A ambako Agness huchota maji, unahitaji kutembea wastani wa kilomita tano au utumie umbali huo huo kwenda visima vya mabondeni vyenye maji ya chumvi.

Moja ya visima vinavyotumiwa na wakazi wa Kitongoji cha Nanyanga kilichopo katika Kijiji cha Litandamtama, Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.
Moja ya visima vinavyotumiwa na wakazi wa Kitongoji cha Nanyanga kilichopo katika Kijiji cha Litandamtama, Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.

Hata hivyo, muda anaotumia Agness kuchota maji ni zaidi ya mara tano ya malengo ya kipengele cha 4.4 cha Sera ya Maji ya Taifa ya mwaka 2002 kinachotaka mtu mmoja apate lita 25 za maji kwa siku na maji hayo yapatikane ndani ya mita 400 kwa nyumba zilizo mbali na kituo cha maji.

Pia, malengo ya Mkakati wa kwanza wa Kukuza Uchumi na Kupambana na Umaskini (Mkukuta I) yalikuwa ni kuongeza uwiano wa upatikanaji wa maji safi na salama vijijini kutoka asilimia 53 mwaka 2003 hadi asilimia 65 mwaka 2010/11 na mkazi asitumie zaidi ya dakika 30 kuteka maji.

Katika kijiji hicho cha Litandamtama chenye vitongoji viwili vya Nanyanga na Litandamtama, vyanzo vikuu vya maji ni visima vifupi vya wazi vilivyochimbwa kwa mkono au mabwawa mafupi ambayo hutumika pia kunyweshea wanyama wakati wa masika hadi kiangazi.

“Kama visima hivi vikikauka kiangazi kikuu huwa tunalazimika kwenda Lionja kama maili nne (kilomita 6.4) kutoka hapa au kwenda kuchota Mto Mbwemkuru ambao upo mbali kama maili sita (kilomita 9.6),” anasema Bakari Kaliwanji wa kitongoji cha Nanyanga, Litandamtama.

Kama ilivyo kwa sehemu nyingi nchini, wanawake hutaabika zaidi na uhaba wa maji kwa kuwa ndiyo wachotaji wakuu wa maji. Kadri uhaba wa maji safi na salama unavyoongezeka wakati wa kiangazi ndivyo wanavyopoteza muda mwingi waliotakiwa kuutumia kufanya shughuli za uzalishaji na kuathiri afya zao.

Wakazi wa vijiji vya Lionja A na Lionja B wakichota maji kwenye kisima ambacho maji yake yana chumvi kidogo. Kisima hicho kilichopo katika Kijiji cha Lionja A katika Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi huhudumia vijiji takriban vinane.
Wakazi wa vijiji vya Lionja A na Lionja B wakichota maji kwenye kisima ambacho maji yake yana chumvi kidogo. Kisima hicho kilichopo katika Kijiji cha Lionja A katika Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi huhudumia vijiji takriban vinane.

 

“Japo natumia baiskeli kwenda kuchota maji bado nateseka,” anasema Mwajuma Swalehe mkazi wa kijiji hicho niliyekutana naye akitoka kuteka maji.

“Mgongo, kichwa na kifua vinaniuma kwa sababu nabeba madumu mawili kila safari na umbali ni mrefu kutoka kisimani,” anasema.

Mwajuma wakati wa masika huenda kuchota maji katika visima vya jirani walivyochimba lakini wakati wa kiangazi analazimika kwenda kuchota maji Lionja, Kijiji cha Namikango au Mto Mbwemkuru ambavyo vyote vinapatikana zaidi ya kilomita sita kutoka nyumbani kwake.

Safari ya kwenda Mto Mbwemkuru kutoka kwa Mwajuma kwa wale ambao hawana baiskeli kama Khadija Omar (75) wanalazimika kupita katika njia nyembamba iliyozungukwa na vichaka virefu.

Hifadhi ya wanyama, nyoka

Wanyama wadogo kama digidigi, vicheche na kenge wanakatiza mara kwa mara barabarani wakikimbia pindi wanaposikia vishindo vya miguu ya watu au mlio wa baiskeli au pikipiki inayoelekea mtoni.

Katika njia ya upande wa mashariki mwa mto kabla ya kuingia kuchota maji unatakiwa kupita katika eneo oevu ambalo sehemu kubwa zisizo na matete zinaonekana kuwa na michirizi ya nyoka wakubwa wanaopita eneo hilo.

Kuna harufu nzito kama ya wali ambayo wenyeji wanasema inatokana na nyoka kujichubua magamba.

Matete yameshonana juu katika sehemu ya kuchotea maji na kutengeneza mwanga hafifu licha ya kuwa ni saa 6 mchana na maji hayatembei kwa kuwa mto umeshaanza kukauka.

“Huwa naenda pekee yangu kila siku kuchota maji Mbwemkuru au kisimani… sasa nikiogopa nitafanyaje labda nikubali kufa na kiu,” anasema Khadija.

“Juzi walipita tembo kwenda kisimani (mtoni) lakini hawakumdhuru mtu ila ni kawaida kupishana na wanyama unavyoenda kuteka maji. Mungu anatunusuru,” anasema.

Tofauti na wanawake wengine wenye waume ambao huwachotea au kuwasindikiza kuteka maji wakati mwingine, Khadija hana mume na watoto wake wakubwa na wajukuu hawaishi naye. Mtoto aliyebaki nae ni mdogo ambaye hawezi kubeba hata ndoo ya lita 10.

Mkazi wa Kijiji cha Litandamtama wilayani Nachingwea, Sofia Said akichota maji kwenye kisima ambacho maji yake si safi na salama. Picha zote na Nuzulack Dausen
Mkazi wa Kijiji cha Litandamtama wilayani Nachingwea, Sofia Said akichota maji kwenye kisima ambacho maji yake si safi na salama. Picha zote na Nuzulack Dausen

Siku ambayo Khadija anahitaji kuchota maji kwa wingi kuanzia lita 40 au zaidi hulazimika kusimamisha shughuli zake zote za kujiingizia kipato hususan za kilimo kutokana na umbali mrefu wa kuchota maji.

“Sina biashara kama wengine nategemea kilimo. Kama kusingekuwa na shida ya maji ningekuwa nawahi kupalilia mikorosho yangu na kupulizia salfa kwa wakati na huenda ningepata gunia tano kwa eka badala ya gunia tatu za sasa,” anasema Asia Abdallah.

Serikali ipo wapi?

Abbas Mussa (78) mkazi wa kijiji hicho anasema muda unasonga bila ya matumaini ya kupata maji safi karibuni na kina mama wanaenda kuchota maji pekee yao kila siku jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao.

“Tunahitaji Serikali itujengee kisima hapa chochote kile kiwe kikubwa au kidogo, cha kupampu na mkono au cha ringi ili mradi tuepuke na shida hii,” anasema Mussa.

Matumaini ya wanakijiji hiki kupata maji safi na salama yamebaki kwa Serikali au msamaria mwema atakayewapelekea kisima.

Serikali ya kijiji inasema haina uwezo wa kuchimba kisima cha maji safi na salama kwa kuwa mapato ni wastani wa Sh500,000 kwa mwaka kutokana na ushuru wa mazao ya mbaazi, korosho na ufuta.

Hii ina maana kuwa itachukua miaka 20 kwa kijiji hicho chenye watu 900 kuchimba kisima cha kisasa cha pampu ya mkono cha gharama ya wastani wa Sh10 milioni iwapo mapato yote ya kijiji yatagharamia mradi huo wa maji.

Kilio cha mwenyekiti

Mwenyekiti wa Kijiji cha Litandamtama, Bakari Libea anasema mwaka 2015 aliwasilisha shida hiyo kwa mbunge wa Nachingwea, Hassan Masala aliyeahidi kuwaletea maji katika bajeti ya mwaka 2016/17, lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika.

“Hatuna mpango wa kuchimba kisima kirefu kwa mashine kwa sababu zaidi ya robo tatu ya wananchi ni maskini sana hivyo tunasubiri Serikali au wafadhili,” anasema Libea.

Uhaba wa maji safi na salama hauwakabili tu wananchi wa Kijiji cha Litandamtama, bali sehemu kubwa ya vijiji vya jirani kama Namikango, Lionja A na B, Nangunde na Mpute.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Lionja, Ernest Ng’onye anasema katika kitongoji cha Litandamtama mwaka jana walichimba bwawa fupi kwa ushirikiano na Tasaf linalowasaidia kupunguza adha ya kwenda kuchota maji katika mto Mbwemkuru.

Hata hivyo, wakati mwandishi wetu anatembelea eneo hilo mwanzoni mwa Agosti, bwawa hilo lilikuwa limeshakauka hivyo kuwafanya wakazi hao kwenda kwenye visima vifupi vya udongo vilivyosalia au kisima cha chengo kilichopo kijiji jirani cha Lionja umbali wa zaidi ya kilomita sita.

Hata alipoulizwa kwanini kijiji hicho na vingine havina maji safi na salama hadi sasa, diwani wa Lionja, Joachim Mnungu anasema huwa anaomba fedha kutoka halmashauri lakini changamoto ni utoaji wa fedha husika.

“Unaweza kuomba fedha ukapata asilimia 48 tu kwa kuwa mapato ni kidogo na Serikali haitoi ruzuku kama ilivyopanga. Mwaka 2017/18 kuna fedha zimetengwa kwa ajili ya kujenga mradi wa maji, mtandao wa mabomba na kufufua miradi ya zamani ila kwa sasa ni mapema kujua tutazipata zote ama la japo matumaini ni makubwa,” anasema.

Uhaba wa maji safi na salama ni tatizo la wilaya nzima. Takwimu za Mkoa wa Lindi za hadi Juni mwaka huu zinabainisha kuwa watu 55 kati ya 100 waishio vijijini wilayani Nachingwea hawana maji safi na salama ikilinganishwa na wastani wa kitaifa wa watu 28 kwa kila 100 hadi Machi mwaka huu.

Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea inasema kuwa inaendelea kuboresha huduma za maji japo changamoto kubwa ni ukosefu wa vyanzo vya maji kutokana na kutegemea maji ya ardhini kama chanzo kikuu na sehemu kubwa yana chumvi.

Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Nachingwea, Bartholomew Matwiga anasema Kijiji cha Litandamtama ni miongoni mwa vijiji vitakavyochimbiwa visima vya maji na asasi ya kiraia ya Gain ili kupunguza adha ya uhaba wa maji safi na salama.

“Vilevile tulipeleka ombi kwa mbunge aliyetaka tuainishe maeneo mawili ama matatu hivi yenye shida ya maji kwa kuwa kuna mtu alikuwa tayari kufadhili. Moja ya vijiji tulivyoainisha Litandamtama na tunategemea kama mbunge atafanikiwa basi tatizo litaanza kupungua,” anasema.

Hata hivyo, jitihada za kuzungumza na mbunge wa Nachingwea, Hassan Masala ziligonga mwamba baada ya kuahirisha mazungumzo mara kwa mara na kutojibu ujumbe wa maandishi aliotumiwa.

Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Arbogast Kiwale anasema kuna juhudi zinafanywa na Serikali na wadau wengine kuhakikisha wananchi wote wa vijijini wanapata maji safi na salama.

Anasema kuna mradi wa vijiji 10 uliofanywa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia ambapo vijiji saba vilifanikiwa kuwa na maji yanayofaa kwa matumizi ya mwanadamu na maeneo hayakufanikiwa wameyajumuisha kwenye miradi mipya.

“Tunazidi kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuongeza upatikanaji wa maji vijijini kama Gain waliochimba visima 81 kati ya 100 walivyopanga kuchimba vijijini wilaya yote.

Taarifa za bajeti ya miradi ya maji za halmashauri hiyo zinaonyesha kuwa mwaka 2016/17 wizara ilipitisha Sh779.87 milioni, lakini Serikali haikuzitoa fedha hizo kama ilivyopangwa.

“Ila tulipokea Sh74.42 milioni kwa ajili ya shughuli nyingine kama vile kuunda na kusajili jumuiya za maji, usafi wa mazingira na Payment by results (malipo kwa utendaji), usimamizi na ufuatiliaji,” anasema Msafiri Tematema, Mhandisi mwandamizi wa halmashauri hiyo.

Mwaka huu Serikali imetenga Sh585.6 milioni kwa ajili ya miradi ya maji pungufu kwa Sh194.3 milioni kwa zile za mwaka jana.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge anasema tatizo kubwa linalosumbua maeneo kama Nachingwea ni ugumu wa kupata vyanzo vya uhakika vya maji jambo linalofanya watumie maji ya ardhini ambayo sehemu nyingi hushuka kiwango wakati wa kiangazi.

Anasema kwa sasa wamewekeza kwenye maeneo yenye uhaba mkubwa wa maji kama Nachingwea na wamebaini visima pekee havitoshelezi mahitaji hivyo wanaangalia vyanzo vingine kwa ama kutoa maji katika mito au ziwa.

“Tutatoa maji Mto Ruvuma na kuyapeleka Mtwara na kuhudumia wananchi wote wa pembezoni mwa mradi na kule kanda ya Ziwa tutaoa maji Ziwa Victoria kuyapeleka hadi Tabora,” anasema Lwenge.

Kuhusu halmashauri kutopewa au kucheleweshewa fedha za miradi ya maji, Lwenge anasema “baada ya kuingia Serikali ya Awamu ya Tano hakuna tena ucheleweshaji na fedha zinatoka zote.”

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania