Usafirishwaji mizigo sekta ya anga nchini umeporomoka ndani ya miaka mitatu

Maria Mtili
October 5, 2017

Ephrahim Bahemu, Mwananchi, [email protected]

Takwimu za Mamlaka ya usafiri wa anga nchini (TCAA), zinaonyesha  kushuka kwa shehena inayosafirisha kutoka tani 32,410 mwaka 2012 hadi tani 30,022 mwaka 2015.

Wakati takwimu hizo zikionyesha hivyo, usafishaji wa abiria unatia faraja kwani idadi ameongezeka kutoka milioni 3.027 mwaka 2011 hadi milioni 4.85 mwaka 2015.

Sababu za kuporomoka huko zinatajwa kuwa za kisera na kiuchumi ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi haraka ili sekta hiyo iwe na mchango mzuri kwenye Pato la Taifa (GDP).

Hata hivyo inaelezwa kuwa shehena kubwa inayotoka nchini hupelekwa Kenya na Uganda kabla ya kusafirishwa kwenda nchi nyingine nje ya Afrika.

Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Wakulima wa Maua na Mbogamboga Tanzania (Taha), Aman Temu anasema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017, uzalishaji wa mazao hayo ulikuwa tani 6.2 milioni  za ujazo na kati ya hizo asilimia 50 zilisafirishwa kwa ndege kwenda masoko ya nje ya nchi.

Anasema, asilimia 20 ya mzigo huo ulisafirishwa kupitia Kenya na asilimia 30 Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

“Kampuni za ndani zinapaswa kujipambanua na kwenda nje. Ni muhimu kuimarisha miundombinu ya viwanja na uhifadhi wa mizigo,” anasema Temu.

Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Precision Air, Hillary Mremi  anasema shehena ni chanzo muhimu cha mapato kwenye biashara ya usafiri wa anga lakini hayavunwi vizuri kutokana na kukosekana kwa ndege za moja kwa moja zinazoenda kwenye mataifa ya mbali.

“Ukiacha abiria, mzigo huongeza mapato ya kampuni nyingi lakini katika viwanja vyetu huwezi kupata ndege ya moja kwa moja kwenda mataifa ya mbali. Vilevile aina ya ndege tunazo tumia si rafiki kwa usafirishaji wa mizigo,” anasema Mremi.

Mshauri wa masuala ya usafiri wa anga na mfanyabiashara ya kusafirisha mizigo, Jimray Nangawe  anasema miundombinu ya viwanja vya ndege inahusika kwa kiasi kikubwa katika kustawisha bishara hiyo.

“Kuna vitu wateja wanavizingatia ili kuweza kutumia uwanja wa ndege fulani kama huduma na mifumo ya kuwahisha shughuli na usalama wa eneo hilo lakini sisi viwanja vyetu vingi vipo katika hatua ya kuendelezwa bado havijafikia huko,” anasema Nangawe.

Anasema ni mhimu kuwa na uwanja ambao ni njia panda ya wasafiri wengi pamoja na kuzingatia mambo mengine muhimu kama mazingira ya biashara na kuondoa vikwazo visivyo vya lazima ili kuongeza kasi ya uwekezaji.

“Mwanza kuna wawekezaji wanachukua ngozi za samaki ambazo ni tiba kwa binadamu lakini vibali vyake havitolewi pale uwanja wa ndege. Comoro kuna soko kubwa la nyama lakini taratibu zilizopo nchini zinaongeza gharama za biashara,” anasema Nangawe.

Meneja wa Operesheni wa Kampuni Swissport, Noel Kasako anasema hali hiyo nchini inachangiwa na kupungua kwa shughuli za utafiti wa mafuta na gesi kweny ekina bahari.

“Mzigo unaoingia ndiyo umeshuka zaidi kuliko usafirishaji na hakuna sababu za hivi karibuni za kimazingira zilizosababisha hilo. Wakati wa utafiti wa mafuta na gesi tulikuwa na uwezo wa kusafirisha wastani wa tani 700 kwa wiki,” anasema Kasako.

Anasema mitambo iliyokuwa ikiletwa kwa ajili ya kufanyia utafiti ilikuwa na uzito mkubwa na ilikuwa inakodiwa kwa saa hivyo lazima isafirishwe kwa ndege ili ifanye kazi haraka na kurudishwa kwa muda.

Kadhalika anasema kutoongezeka kwa mizigo katika viwanja vyetu halisababishwi na miundombinu ya uhifadhi wa mizigo tu, bali uwapo wa ndege zenye uwezo wa kubeba mizigo mikubwa kuelekea nchi ambazo wafanyabiashara wengi wanauza na kununua bidhaa.

Hata hivyo, kuporomoka kwa shehena ilikuwa ni miongoni mwa agenda zilizojadiliwa katika mkutano wa kwanza wa wadau wa sekta ya usafiri wa anga nchini uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TCAA, Hamza Johari alisema ongezeko la abiria lilipaswa kwenda sambamba na mizigo.

“Wafanyabiashara wa samaki wanatoka Mwanza wanapeleka mzigo Uwanja wa Entebe kwenda nje wakati Mwanza nako kuna uwanja. Au mfanyabiashara wa maua anayasafirisha kutoka Kilimanjaro hadi Nairobi wakati kuna uwanja wa  Kilimanjaro. Kuna tatizo mahali,” anasema Johari.

Wadau katika mkutano huo walipendekeza namna nzuri ya kuiinua sekta hiyo ni kuuboresha JNIA kuwa njia panda ya kwend anchi nyingine duniani.

Mpaka sasa kuna maboresho kadhaa yamefanyika katika sekta ya anga nchini, Kama upanuzi wa viwanja vya ndege na ununuzi wa rada mpya nne ambazo zimegharimu Sh63.1 bilioni kwa lengo la kuimarisha ukusanyaji wa mapato na usalama.

Pia kuna upanuzi unaendelea katika uwanja wa ndege wa JNIA ambapo ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria milioni 6.4 tofauti na milioni 2.5 wa sasa.

Mradi huo unaotarajia kukamilika mwaka ujao, unatekelezwa na kampuni ya Kiholanzi ya Bam International kwa gharama ya Sh560.

Licha ya miundombinu hiyo, Serikali inalifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), pamoja na mambo mengine, lengo likiwa ni kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini.

Licha ya kuwa na vivutio vingi kuliko nchi nyingi duniani isipokuwa Brazil, Tanzania inapokea chini ya watalii milioni mbili.

Takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii zinaonyesha mwaka jana, idadi yao ilikuwa milioni 1.284 likiwa ni ongezeko la asilimia 12.1.

Malengo yaliyopo ni kufikisha watalii milioni tatu mpaka mwakani.

Maria Mtili

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania