Sababu ya baadhi ya visima vya maji kutotoa huduma Tanzania

Nuzulack Dausen
October 15, 2017

 

  • Kiwango cha visima vinavyochimbwa na wakala wa uchimbaji visima na mabwawa (DDCA) kimeongezeka zaidi ya mara tatu ndani ya miaka minne.
  • Hata hivyo, mwaka 2015/16 kisima kimoja kwa kila vitano vilivyochimbwa hakikufanya kazi na kusababisha wananchi wa maeneo husika kukosa maji.

[email protected]

Dar es Salaam. Pamoja na kasi ya uchimbaji visima vya maji kuongezeka nchini ndani ya miaka minne iliyopita, baadhi ya wananchi huishia kutazama tu mitambo ikichimba vyanzo hivyo bila kupata maji kutokana na baadhi ya visima kutotoa huduma hiyo.

Uchambuzi wa takwimu za visima vilivyochimbwa na Wakala wa uchimbaji visima na mabwawa (DDCA) uliofanywa na MwananchiData unaonyesha idadi ya visima vilichimbwa na wakala huo imeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka 83 mwaka 2012/13 hadi visima 270 mwaka 2015/16.

Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya maji, visima huchimbwa mara nyingi katika maeneo ambayo hayana vyanzo vikubwa vya maji kama mito na maziwa ili kuongeza upatikanaji wa majisafi na salama.

Maji ya visima hivyo huwa ni safi na salama hivyo hupunguza uwezekano wa watu kupata magonjwa ya tumbo au kupoteza muda wa kuzalisha wakati wakisaka huduma hiyo muhimu.

Miongoni mwa halmashauri zilizoipa DDCA kandarasi nyingi zaidi za kuchimba visima, kwa mujibu wa takwimu hizo zilizochapishwa katika kituo huru cha takwimu rasmi cha www.opendata.go.tz, katika kipindi hicho ni Kinondoni, Temeke, Bagamoyo na Ilala.

Katika mwaka wa fedha wa 2015/16 pekee, robo ya visima vilivyochimbwa na wakala huo ulio chini ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji vilikuwepo katika Manispaa ya Kinondoni.

Halmashauri nyingine zilizokuwa na idadi kubwa ya visima hivyo vilivyochimbwa na DDCA ambavyo vilizidi zaidi ya 10 ni Bagamoyo, Ilala, Mlele, Dodoma, Kibaha, na Temeke.

Hata hivyo, visima 50 kati ya 270 za vilivyochimbwa mwaka 2015/16 havifanyi kazi.

Hii ina maana kuwa katika kila visima vitano vilivyochimbwa katika mwaka huo ulioshia Juni 2016 havitoi maji kama ilivyotarajiwa jambo linalofanya wakazi wa maeneo hayo waendelee kutaabika kuisaka huduma hiyo muhimu.

Halmashauri zilizokuwa na idadi kubwa ya visima ambavyo havitoi maji mwaka huo ni Kinondoni ambayo kisima kimoja kati ya 10 hakikutoa maji, ikifuatiwa na Bagamoyo visima vitano, Chemba mkoani Dodoma (5) na Kisarawe mkoani Pwani vitatu. Nusu ya visima vilivyokuwa vimechimbwa Kisarawe havikufanikiwa kutoa huduma.

Temeke na Ilala licha ya kuwa na idadi kubwa ya visima vilivyochimbwa zilifanikiwa kuwa na visima vyote vinavyofanya kazi.

Uchunguzi umebaini kuwa wanaotaabika zaidi baada ya visima hivyo kutotoa maji ni wananchi wa vijijini ambao kwa sehemu kubwa nchini wanakabiliwa na uhaba wa majisafi na salama.

Katika vijiji vya Lionja A na Lionja B vilivyopo katika halmashauri ya Nachingwea mkoani Lindi wananchi kwa sasa wanatumia visima vya wazi baada ya vile vya kisasa kushindwa kufanya kazi ipasavyo kutokana na maji kuwa mbali na pampu wakati wa kiangazi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Lionja A Said Juma anasema kisima cha kisasa cha madukani kilishindwa kutoa maji ipasavyo baada ya maji kuwa chini zaidi na kufanya kitumike wakati wa masika pekee.

Kisima hicho cha pampu kwa sasa kimeharibiwa baada ya nati za kushikilia upande wa juu kuibwa.

Halmashauri ya Nachingwea, ambayo mwaka 2012 ilikuwa na watu 169,327 kwa mujibu wa takwimu za Sensa zilizochapishwa kwenye tovuti huru ya takwimu ya Hurumap, ni halmashauri ya mwisho kwa kuwa na idadi ndogo ya wananchi wanaopata huduma za maji safi na salama.

Takwimu za hadi Juni mwaka huu zilizotolewa na ofisi ya mkoa wa Lindi zinabanisha kuwa ni watu 45 tu kati ya 100 wanaoishi vijijini hupata maji safi na salama ikilinganishwa na 71 kati ya 100 wanaoishi mjini.

Soma zaidi:Uhaba wa maji unavyowatesa wanawake wilayani Nachingwea 

Tofauti na wakazi wa Manispaa za Temeke au Kinondoni ambao huwa kidogo na uwezo wa kifedha na mbadala wa kupata maji hata kwa kununua kwa watu binafsi waliochimba visima, watu wa vijijini wengi ni maskini na kuyapata maji hulazimika kutembea umbali mrefu.

Wataalamu wa masuala ya afya wanasema uhaba wa majisafi na salama unachangia kwa kiwango kikubwa magonjwa ya tumbo hususan kuhara.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa DDCA, Jonath Mgaiwa aliiambia MwananchiData kuwa baadhi ya visima ambavyo vimechimbwa huwa havifanyi kazi kutokana na maji ya ardhini kutokuwa na kiwango cha kutosha licha ya utafiti wa awali kuonyesha kuwa palikuwa na maji ya mengi.

“Jambo jingine ni ubora hafifu wa maji yanayopatikana baada ya kuchimba kisima. Kuna baadhi ya miamba mifumo yake ya kikemikali au madini huaribu maji na kuyafanya yawe na chumvi nyingi au sumu kiasi cha kutofaa kwa matumizi ya na binadamu,” anasema.

Hata hivyo, bosi huyo hakuweza kubainisha kiwango halisi cha idadi ya watu ambao waliathirika baada ya baadhi ya visima kutofanikiwa kutoa maji kama ilivyokuwa imepangwa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uchimbaji Visima na Mabwawa Tanzania (DDCA) Jonath Mgaiwa. Picha ya Mtandao.

Hata hivyo, Sera ya Maji ya mwaka 2002 inaeleza kuwa kituo cha maji hutakiwa kutoa huduma kwa watu 250 katika eneo husika.

Hii ina maana kuwa kama visima 50 vilichimbwa na Serikali kwa ajili ya wananchi basi wakazi 12,500 wamekosa huduma hiyo muhimu kwa maisha ya mwanadamu.

Aliyekuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwenge aliiambia MwananchiData kuwa wastani wa asilimia 30 ya visima ambavyo huchimbwa nchini huwa havitoi huduma kutokana na sababu za kijiolojia.

Lwenge alieleza kuwa hali hiyo huighalimu Serikali na kuchelewesha wananchi wa vijijini kupata maji hivyo ili kuhakikisha watu wote wanapata maji kwa sasa wanawekeza katika miradi mikubwa ya kutoa maji katika mito mikubwa au maziwa.

Alisema kwa mikoa ya kusini watatoa maji kutoka Mto Ruvuma hadi Mtwara wakati mikoa ya kanda ya ziwa hadi Tabora watanufaika na mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria.

 

 

 

 

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania