Mambo ambayo huenda huyajui kuhusu mchele wa Kyela

Nuzulack Dausen
October 19, 2017

  • Shirika la Chakula  na Kilimo Duniani (FAO) laeleza kuwa mchele wa Kyela unaaminika kuwa bora zaidi nchini ukifuatiwa na ule unaotoka wilaya nyingine za Mbeya.
  • Licha ya umaarufu huo wa Kyela, bado eneo la ardhi ni dogo takriban mara 19 pungufu wa lile la wilaya ya Mbarali.

[email protected]

Dar es Salaam. Pamoja na Mbeya kusifika kwa kuzalisha mchele bora nchini, moja ya halmashauri za wilaya zinazozalisha zao hilo kwa kiwango kikubwa mkoani humo ina eneo dogo la kilimo jambo linaloonyesha bado kuna fursa lukuki kwa wakulima kuzalisha zaidi mazao kwa wingi.

Shirika la Kilimo Duniani (FAO) mwaka 2015 lilieleza kuwa mchele wa Kyela ndiyo unaofahamika kuwa bora zaidi Tanzania ukifuatiwa na ule unaotoka wilaya nyingine za Mbeya.

Uchambuzi wa taarifa ya mkoa wa Mbeya ya mwaka 2016 unabainisha kuwa Halmashauri ya Kyela ni wilaya ya pili kutoka mwisho kwa kuwa na eneo dogo la nchikavu baada ya kuwa na kilomita za mraba 872 tu kutokana na sehemu nyingine kutwaliwa na maji hususan ya Ziwa Nyasa. Kilomita 450 za mraba nyingine zipo majini.

Kyela na Mbarali ndiyo wilaya zinazoongoza kwa kilimo cha mpunga katika mkoa huo na hata Nyanda za Juu Kusini inayohusisha mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, na Njombe.

Eneo la nchikavu lililopo chini ya Kyela ni mara 19 pungufu ya lile lililopo katika wilaya ya Mbarali ambayo nayo hulima zaidi mpunga katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya Chimala, Ubaruku na Madibira.

Licha ya udogo huo wa halmashauri ya Kyela,  eneo hilo ambalo linahusisha hifadhi ya misitu bado linazalisha mpunga kwa wingi. Wilaya hiyo ilikuwa na watu 208,453  wakati wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa katika tovuti inayokusanya takwimu huru ya Hurumap.

Mbarali ina kilomita 16,632 za mraba za ardhi iliyopo nchikavu ambayo sehemu moja wapo inafaa kwa kilimo.

Mbarali yenye takriban nusu (asilimia 46.9) ya ardhi mkoani humo ndiyo inayoongoza kwa ukubwa wakati jiji la Mbeya likiwa ni la mwisho kwa kuwa na eneo dogo ambalo ni asilimia 0.6 tu ya ardhi yote ya mkoa.

Tofauti na Kyela na Mbarali, jiji la Mbeya ni makao makuu ya mkoa na kitovu cha biashara katika ukanda wa nyanda za juu kusini na linatumika kama sehemu ya soko la mazao mengi yanayozalishwa wilayani.

Maeneo mengine yanayolima mpunga kwa kiwango kikubwa nchini ni pamoja na Morogoro katika maeneo ya bonde la kilombero, Ifakara, Dakawa, Malolo; Shinyanga katika wilaya ya Kahama; Mwanza na bonde la Mto Ruvu mkoani Pwani.

Kilimo ndiyo shughuli kuu ya kiuchumi inachangia kwa sehemu kubwa vipato vya wakazi wa Mbeya ambayo kwa mujibu wa ofisi ya mkuu wa mkoa.

Pamoja na udogo wake, Kyela imebarikiwa kuwa katika eneo lenye fursa kubwa za kilimo kutokana na upande wa kusini kuwa na mvua zaidi ya wastani wa milimita 2,500 kwa mwaka tofauti na maeneo mengine yanayopata mvua kidogo.

Hali hiyo ya hewa ndiyo inayowafanya wakulima wa eneo hilo kupata fursa za kulima zaidi mpunga na mazao mengine ikilinganishwa na wenzao wa Chunya ambao sehemu kubwa wapo kwenye ukanda wa chini wenye wastani wa chini ya milimita 1,000 kwa mwaka.

“Fursa za uwekezaji mkoani Mbeya zinatofautiana kutoka wilaya hadi wilaya kwa mfano Kyela na Mbarali ni maalum kwa kuzalisha mpunga wakati Mbeya vijijini na Rungwe zinafaa kwa uzalishaji wa kahawa, mahindi, maharage, na kilimo cha matunda,” inasomeka taarifa ya mkoa iliyochapishwa katika tovuti yao.

Mpunga ukiwa katika hatua za mwisho za kukomaa. Mpunga ndiyo huzalisha mchele unaohitajika kwa kiwango kikubwa nchini. Picha ya Mtandao.

Profesa wa masuala ya uchumi wa kilimo wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Damian Gabagambi anasema uwekezaji mzuri wa huduma za ugani na uwepo wa maji ya kutosha ni moja ya njia zinazoongeza uzalishaji hata katika maeneo madogo kama Kyela.

Anasema pamoja na kwamba baadhi ya maeneo yanaonekana kuzalisha sana mazao fulani bado kiwango hicho ni nusu tu ya kile kilichotakiwa kuzalishwa kwa kuwa kuna changamoto lukuki zinazowakabili wakulima.

“Wastani wa uzalishaji mpunga duniani kote ni tani sita kwa hekta lakini hapa Tanzania ni wastani wa tani tatu tu kwa hekta na kiwango hicho ni kwa wakulima wale ambao wamejitahidi kuzalisha sana,” anasema Profesa Gabagambi ambaye amefanya tafiti mbalimbali za kilimo na masoko nchini.

Anasema ili wakulima wa wilaya zote nchini wazalishe kwa wingi wanapaswa kutatuliwa changamoto zao kama kuwekewa miundombinu mizuri ya umwagiliaji na kupatiwa huduma stahiki za pembejeo kama mbegu na dawa za kutibu mimea.

Hata hivyo, anaeleza kuwa uzalishaji mwingi bila soko itakuwa ni kuongeza maumivu kwa wakulima hivyo ni lazima Serikali kwa kushirikiana na wadau wajenge mfumo imara wa masoko ya mazao nchini.

“Wakulima wajiunge kwenye vikundi kuongeza nguvu halafu waende kwa waziri husika kuomba kibali kusafirisha nje mimi naamini watapata kuliko sasa ambavyo kila mkulima anataka kupeleka pekee yake. Serikali inaelewa changamoto za masoko, itawasikiliza,” anasema Profesa Gabagambi.

FAO inaeleza kuwa mahitaji ya mchele yanazidi kuongezeka nchini hasa Dar es Salaam na kuongeza fursa zaidi kwa wakulima.

Pamoja na kwamba Tanzania bado ni muingizaji mkubwa wa mchele, ILO inaeleza bado kuna fursa kubwa kwa kuwa nchi za jirani zinazohitaji kuingiza zao hilo kwa wingi.

 

 

 

 

 

 

Nuzulack Dausen

Nuzulack Dausen ni Mkuu wa dawati la habari za takwimu wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti. Mwaka 2015 alishinda tuzo ya Mwandishi bora wa habari za Uchunguzi kwa upande wa magazeti zinazotolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT). Amejikita zaidi katika habari za biashara, uchumi, teknolojia na data.

MWANANCHIDataLab by Code for Tanzania